Book of Common Prayer
Tahadhari Kutokana na Yaliyotokea Zamani
10 Ndugu zangu, sitaki mshindwe kutambua umuhimu wa kile kilichowatokea baba zetu waliokuwa na Musa. Walifunikwa na wingu,[a] na walipita katika bahari. 2 Walibatizwa[b] wote katika Musa katika wingu na katika bahari. 3 Wote walikula chakula kilichotolewa na Roho wa Mungu, 4 na wote walikunywa kinywaji kinachotolewa na Roho wa Mungu. Kinywaji walichokunywa kilitoka katika mwamba wa roho uliokuwa pamoja nao, na mwamba huo ni Kristo. 5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, na hivyo waliangamizwa jangwani.
6 Mambo haya yaliyotokea ni tahadhali kwa ajili yetu. Mifano hii itufanye tuache kutamani maovu kama baadhi yao walivyofanya. 7 Msiabudu sanamu kama ambavyo baadhi yao walifanya. Na kama Maandiko yanavyosema, “Waliketi chini kula na kunywa kisha wakasimama kucheza.”(A) 8 Tusifanye dhambi ya uzinzi kama baadhi yao walivyofanya na watu ishirini na tatu elfu miongoni mwao wakafa. 9 Tusimjaribu Kristo[c] kama vile baadhi yao walivyofanya. Kwa sababu hiyo, waliuawa na nyoka. 10 Na msinung'unike kama baadhi yao walivyofanya na wakauawa na malaika anayeangamiza.
11 Mambo yaliyowapata wale watu ni mifano na yaliandikwa ili kututahadharisha sisi tunaoishi nyakati hizi za mwisho. 12 Hivyo kila anayedhani kuwa yuko imara katika imani yake, basi awe mwangalifu asianguke. 13 Majaribu mliyonayo ni yale yale waliyonayo watu wote. Lakini Mungu ni mwaminifu maana hataacha mjaribiwe kwa kiwango msichoweza kustahimili. Mnapojaribiwa, Mungu atawapa mlango wa kutoka katika jaribu hilo. Ndipo mtaweza kustahimili.
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mt 15:1-20)
7 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Sheria waliokuja kutoka Yerusalemu walikusanyika mbele zake. 2 Hao wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula chao kwa mikono michafu (yaani bila kuosha mikono yao). 3 Kwani Mafarisayo na Wayahudi wengineo wote hawawezi kula isipokuwa wameosha mikono yao kwa njia maalumu, kulingana na desturi ya wazee. 4 Na wanaporudi kutoka sokoni, hawali chakula kwanza mpaka wamenawa. Na zipo desturi nyingi wanazozishika, kama vile kuosha vikombe, magudulia na mitungi ya shaba.[a]
5 Kwa hiyo Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, badala yake wanakula chakula chao kwa mikono isiyo safi?”
6 Yesu akawaambia, “Isaya alikuwa sahihi alipotoa unabii juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa:
‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
7 Ibada wanayonitolea haifai,
kwa sababu wanawafundisha watu amri
zilizotungwa na wanadamu kana kwamba ndizo itikadi zao.’(A)
8 Mmezipuuza amri za Mungu, na mnashikilia desturi za binadamu.”
9 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wazuri katika kuzikataa amri za Mungu ili kuanzisha desturi yenu. 10 Kwa mfano Musa alisema, ‘Mheshimu baba yako na mama yako,’(B) na yule mtu atakayesema maneno mabaya juu ya ‘mama au baba yake itampasa auwawe.’(C) 11 Lakini ikiwa mtu atamwambia baba au mama yake, ‘Nilikuwa na kitu ambacho ningekupa kikusaidie, lakini nimeahidi kukitoa wakfu kwa Mungu, nacho sasa ni kurbani.[b]’ 12 Kisha, anasema, hivyo hawezi kufanya kitu chochote kwa ajili ya kumsaidia baba au mama yake. 13 Kwa hiyo unalifanya neno la Mungu kuwa batili kwa desturi mlizozirithishana. Na mnafanya mambo mengi mengine yanayofanana na hayo.”
14 Yesu akaliita lile kundi kwake na kuwaambia, “Kila mmoja anisikilize na kunielewa. 15 Hakuna kitu kilicho nje ya mtu kinachoweza kumchafua kwa kumwingia. Lakini vitu vinavyotoka ndani ya mtu ndivyo vinavyomchafua.” 16 [c]
17 Na alipoliacha lile kundi na kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza juu ya fumbo lile. 18 Na akawaambia, “Hata nanyi hamuelewi pia? Je, hamuelewi ya kuwa hakuna kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumchafua mtu? 19 Kwa sababu hakiingii ndani ya moyo wake bali kinaenda tumboni mwake na kasha kinatoka na kwenda chooni.” Kwa kuyasema hayo alivifanya vyakula vyote kuwa safi.
20 Na Yesu akasema, “Ni kile kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomchafua. 21 Kwani mambo hayo yote mabaya hutoka ndani ya moyo wa mwanadamu; yaani mawazo mabaya na uasherati, wizi, mauaji, 22 zinaa, ulafi, kufanya mabaya kwa watu, udanganyifu, kufanya uhuni, wivu, kutukana, kujivuna, na ujinga. 23 Mambo haya yote yanatoka ndani ya mtu nayo ndiyo yanayomfanya asikubalike kwa Mungu.”
© 2017 Bible League International