Book of Common Prayer
3 Je, mmesahau kwamba sisi sote tulifanyika sehemu ya Kristo Yesu tulipobatizwa? Katika ubatizo wetu tulishiriki katika kifo chake. 4 Hivyo, tulipobatizwa, tulizikwa pamoja na Kristo na kushiriki katika kifo chake. Na kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa nguvu ya ajabu ya Baba, ndivyo nasi tunaweza kuishi maisha mapya sasa.
5 Kristo alikufa, nasi tumeunganishwa pamoja naye kwa kufa kama yeye alivyokufa. Kwa hiyo tutaunganishwa pamoja naye kwa kufufuka kutoka katika kifo kama yeye alivyofanya. 6 Tunajua kuwa utu wetu wa zamani ulikufa msalabani pamoja naye. Hivyo ndivyo maisha ya utumwa tuliyokuwa nayo yalivyoangamizwa ili tusiendelee kuitumikia dhambi tena. 7 Yeyote aliyekufa amewekwa huru kutoka katika nguvu za dhambi.
8 Ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunajua kwamba tutaishi pamoja naye pia. 9 Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na tunajua kuwa hawezi kufa tena. Sasa mauti haina nguvu juu yake. 10 Ndiyo, Kristo alipokufa, alikufa ili aishinde nguvu ya dhambi mara moja, na siyo mara nyingine tena. Sasa anao uzima mpya, na uzima wake huo upo kwa nguvu za Mungu. 11 Kwa namna hiyo hiyo, mnapaswa kujiona kama mliokufa kwa dhambi na mlio hai kwa nguvu za Mungu kupitia Kristo Yesu.
12 Mwili mlionao katika uhai wenu wa sasa hapa duniani utakufa. Msiruhusu dhambi iutawale na kuwafanya ninyi kuzitumikia tamaa zake. 13 Msiitoe sehemu ya miili yenu kwa dhambi kwa ajili ya kutumika kutenda maovu. Jitoeni kwa Mungu, kama watu waliokufa lakini walio hai. Toeni sehemu za miili yenu kwa Mungu ili zitumiwe kwa kutenda mema. 14 Dhambi haitakuwa mtawala wenu, kwa sababu hamko chini ya sheria. Sasa mnaishi chini ya neema ya Mungu.
Yesu Anayo Mamlaka ya Mungu
19 Lakini Yesu akajibu, “Hakika nawaambieni kuwa Mwana hawezi kufanya chochote peke yake. Bali hufanya tu yale anayoona Baba yake anayafanya. Kwa maana Mwana hufanya mambo ambayo Baba huyafanya. 20 Baba anampenda Mwana na humwonesha kila kitu anachofanya. Pia Baba atamwonesha Mwana mambo makuu ya kufanya kuliko hili. Kisha nyote mtashangazwa. 21 Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima. Kwa njia hiyo hiyo, Mwana pia huwapa uzima wale anaowataka.”
22 “Vile vile, Baba hamhukumu mtu. Bali amempa Mwana nguvu ya kufanya hukumu zote. 23 Mungu alifanya hivi ili watu wote waweze kumheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Mtu yeyote asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba. Kwani Baba ndiye aliyemtuma Mwana.
24 Kwa hakika nawaambia, yeyote anayesikia ninayosema na kumwamini yule aliyenituma anao uzima wa milele. Hawa hawatahukumiwa kuwa na hatia. Kwani tayari wameshaivuka mauti na kuingia ndani ya uzima.
© 2017 Bible League International