Book of Common Prayer
Kuhusu Ndoa
7 Sasa nitazungumza kuhusu mambo yale mliyoniandikia. Mliuliza ikiwa ni bora mwanaume asimguse mwanamke kabisa. 2 Lakini dhambi ya uzinzi ni ya hatari, hivyo kila mwanaume anapaswa kumfurahia mke wake, na kila mwanamke anapaswa kumfurahia mume wake. 3 Mume anapaswa kumtosheleza mkewe, vivyo hivyo mke amtosheleze mume wake. 4 Mke hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mume ana mamlaka juu ya mwili wa mkewe. Mume hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mke ana mamlaka juu ya mwili wa mumewe. 5 Msinyimane miili yenu. Lakini mnaweza kukubaliana kutojamiiana kwa muda ili mtumie muda huo katika maombi. Kisha mkutane tena ili Shetani asiwajaribu kutokana na kushindwa kujizuia tamaa zenu. 6 Ninasema hivi ili kuwaruhusu mtengane kwa muda tu. Lakini hii siyo amri. 7 Mimi ningependa kila mtu angekuwa kama mimi nilivyo. Lakini Mungu amempa kila mtu uwezo tofauti. Huwafanya wengine kuwa hivi na wengine kuwa vile.
8 Sasa kwa ajili ya wale ambao hawajaoa ama hawajaolewa na kwa ajili ya wajane ninawaambia ya kwamba ni vizuri mkae bila kuoa au kuolewa kama mimi. 9 Lakini ikiwa mtashindwa kudhibiti tamaa zenu, basi mwoe au muolewe. Ni vyema kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Lk 8:22-25)
35 Siku ile ilipofika jioni aliwaambia, “Hebu tuvuke kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.” 36 Kwa hiyo wakaliacha lile kundi. Wakamchukua pamoja nao alipokuwa amerudi katika mtumbwi. Wakati ule ule palikuwepo na mitumbwi mingi mingine ziwani. 37 Dhoruba kubwa ikatokea na mawimbi yalikuwa yanakuja katika pembe zote za mtumbwi. Mtumbwi nao ulikaribia kujaa maji kabisa 38 lakini Yesu alikuwa amelala nyuma ya mtumbwi akiegemea mto. Wakamwaamsha na kumwambia, “Mwalimu je wewe hujali kwamba tunazama?”
39 Kisha akainuka, akaukemea upepo, na akaliamuru ziwa, “Nyamaza Kimya! Tulia!” Upepo ule ukatulia na ziwa nalo likatulia kabisa.
40 Kisha akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Je! Bado hamna imani yoyote?”
41 Lakini walikuwa na woga sana, na wakasemezana wao kwa wao, “Ni nani basi huyu ambaye hata upepo na ziwa vinamtii?”
© 2017 Bible League International