Add parallel Print Page Options

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mt 3:1-12; Lk 3:1-9,15-17; Yh 1:19-28)

Mwanzo wa Habari Njema za Yesu Masihi,[a] Mwana wa Mungu,[b] zilianza kama vile Nabii Isaya alivyosema zitaanza, aliandika,

“Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
    Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.”(A)
“Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
    nyoosheni njia kwa ajili yake.’”(B)

Naye Yohana akaja, akiwabatiza watu huko nyikani huku akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani.

Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi.

Yeye alitangaza yafuatayo: “Yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.[c] Mimi nawabatiza katika maji, lakini yeye huyo atawabatiza katika Roho Mtakatifu.”

Yohana Ambatiza Yesu

(Mt 3:13-17; Lk 3:21-22)

Ikatokea katika siku hizo Yesu alikuja toka Nazareti uliokuwa mji wa Galilaya akabatizwa na Yohana katika mto Yordani. 10 Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, Yesu aliona mpasuko ukitokea angani, akamwona Roho akishuka chini kuja kwake kama njiwa. 11 Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.”

Yesu Ajaribiwa na Shetani

(Mt 4:1-11; Lk 4:1-13)

12 Kisha baada ya kutokea mambo haya Roho Mtakatifu alimchukua Yesu na kumpeleka nyikani,[d] 13 naye akawa huko kwa siku arobaini, ambapo alijaribiwa na Shetani. Yesu alikuwa nyikani pamoja na wanyama wa porini, na malaika walimhudumia.

Yesu Aanza Kazi yake Galilaya

(Mt 4:12-17; Lk 4:14-15)

14 Baada ya Yohana kuwekwa gerezani, Yesu akaja katika wilaya karibu na Ziwa Galilaya, huko aliwatangazia watu Habari Njema kutoka kwa Mungu. 15 Akasema, “Wakati umefika. Ufalme wa Mungu umewafikia.[e] Mbadili mioyo yenu na maisha yenu, na kuiamini habari njema!”

Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi

(Mt 4:18-22; Lk 5:1-11)

16 Alipokuwa akitembea kando kando ya Ziwa Galilaya, Yesu alimwona Simoni[f] na Andrea ndugu yake. Hao walikuwa wavuvi na walikuwa wakizitupa nyavu zao ziwani kukamata samaki. 17 Yesu akawaambia, “njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine, nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” 18 Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata.

19 Kisha Yesu akaendelea mbele kidogo na akawaona ndugu wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na kaka yake Yohana. Yesu aliwaona wakiwa kwenye mashua wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. 20 Naye akawaita mara moja. Hivyo wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua na watu waliowaajiri na kumfuata Yesu.

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu

(Lk 4:31-37)

21 Kisha Yesu na wafuasi wake waliingia Kapernaumu. Siku ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na akaanza kuwafundisha watu. 22 Walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[g] 23 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Naye mara alipiga kelele na kusema, 24 “Unataka nini kwetu, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.”

25 Lakini Yesu akamkemea na kumwambia, “Nyamaza kimya, na kisha umtoke ndani yake.” 26 Ndipo roho yule mchafu akamfanya mtu yule atetemeke. Kisha akatoa sauti kubwa na kisha akamtoka.

27 Kila mmoja akashangazwa sana kiasi cha kuwafanya waulizane, “Hii ni nini? Ni mafundisho ya aina mpya, na mtu yule anafundisha kwa mamlaka! Yeye huwapa amri pepo wachafu nao wanamtii!” 28 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea haraka katika eneo lote la Galilaya.

Yesu Awaponya Watu Wengi

(Mt 8:14-17; Lk 4:38-41)

29 Wakaondoka kutoka katika sinagogi na mara hiyo hiyo wakaenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mara Yesu alipoingia ndani ya nyumba watu wakamweleza kuwa mama mkwe wake Simoni alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amepumzika kitandani kwa sababu alikuwa na homa. 31 Yesu akasogea karibu na kitanda, akamshika mkono na kumsaidia kusimama juu. Ile homa ikamwacha, na yeye akaanza kuwahudumia.

32 Ilipofika jioni, baada ya jua kuzama waliwaleta kwake watu wote waliokuwa wagonjwa na waliokaliwa na mashetani. 33 Mji mzima ulikusanyika mlangoni pale. 34 Naye akawaponya watu waliokuwa na magonjwa ya kila aina, na kufukuza mashetani wengi. Lakini yeye hakuyaruhusu mashetani kusema, kwa sababu yalimjua.[h]

Yesu Aenda Katika Miji Mingine

(Lk 4:42-44)

35 Asubuhi na mapema, ilipokuwa giza na bado hakujapambazuka, Yesu aliamka na kutoka kwenye nyumba ile na kwenda mahali ili awe peke yake na kuomba. 36 Lakini Simoni na wale wote waliokuwa pamoja naye waliondoka kwenda kumtafuta Yesu 37 na walipompata, wakamwambia, “kila mmoja anakutafuta.”

38 Lakini Yesu akawaambia, “Lazima twende kwenye miji mingine iliyo karibu na hapa, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hilo ndilo nililokuja kulifanya.” 39 Hivyo Yesu alienda katika wilaya yote iliyoko mashariki mwa ziwa la Galilaya akihubiri Habari Njema katika masinagogi na kuwafungua watu kutoka katika nguvu za mashetani.

Yesu Amponya Mgonjwa

(Mt 8:1-4; Lk 5:12-16)

40 Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.”

41 Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika.[i] Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” 42 Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi.

43 Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. 44 Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze,[j] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru[k] watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” 45 Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko.

Yesu Amponya Aliyepooza

(Mt 9:1-8; Lk 5:17-26)

Siku chache baadaye Yesu alirudi Kapernaumu na habari zikaenea kuwa yupo nyumbani. Hivyo watu wengi walikusanyika kumsikiliza akifundisha na haikuwapo nafasi iliyobaki kabisa ndani ya nyumba, hata nje ya mlango. Yesu alipokuwa akifundisha, baadhi ya watu walimleta kwake mtu aliyepooza amwone. Mtu huyo alikuwa amebebwa na rafiki wanne. Watu hao hawakuweza kumfikisha mgonjwa kwa Yesu kwa sababu ya umati wa watu ulioijaza nyumba yote. Hivyo walipanda na kuondoa paa juu ya sehemu aliposimama Yesu. Baada ya kutoboa tundu darini[l] kwenye paa, wakateremsha kirago alimokuwa amelala yule aliyepooza. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo wale waliomleta na yule mwenye kupooza, alimwambia, “Mtoto wangu, dhambi zako zimesamehewa.”

Baadhi ya walimu wa sheria walikuwa wamekaa pale. Nao waliona kile alichokifanya Yesu na wakawaza miongoni mwa wenyewe, “Kwa nini mtu huyu anasema maneno kama hayo? Si anamtukana Mungu! Kwani hakuna awezaye kusamehe dhambi ila Mungu.”

Mara moja Yesu alifahamu walichokuwa wakikifikiri wale walimu wa sheria, hivyo akawaambia, “Kwa nini mna maswali kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza ‘Dhambi zako zimesamehewa,’ kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kirago chako na utembee’? 10 Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina!” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? 11 Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kirago chako uende nyumbani!’”

12 Yule mtu aliyepooza alisimama na bila kusita, akabeba kirago chake na akatoka nje ya nyumba wakati kila mmoja akiona. Matokeo yake ni kuwa wote walishangazwa na mambo hayo. Wakamsifu Mungu na kusema, “Hatujawahi kuona kitu kama hiki!”

Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu

(Mt 9:9-13; Lk 5:27-32)

13 Mara nyingine tena Yesu akaelekea kandoni mwa ziwa, na watu wengi walikuwa wakimwendea, naye akawafundisha. 14 Alipokuwa akitembea kando ya ufukwe wa ziwa, alimwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi katika mahala pake pa kukusanyia kodi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Hivyo Lawi akainuka na kumfuata.

15 Baadaye Yesu na wafuasi wake wa karibu walikuwa wakila chakula cha jioni nyumbani kwa Lawi. Wakusanya kodi wengi na watu wengine wenye sifa mbaya nao wakamfuata Yesu. Hivyo wengi wao walikuwa wakila pamoja na Yesu na wanafunzi wake. 16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa pamoja na Mafarisayo walipomwona Yesu akila na wenye dhambi na wanaokusanya kodi, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Yesu anakula na wenye kukusanya kodi na watu wengine wenye dhambi?”

17 Yesu alipolisikia hili akawaambia, “Wale walio wagonjwa ndio wanaomhitaji daktari si wale walio wazima wa afya. Mimi nimekuja kuwakaribisha wenye dhambi waje kwangu sikuja kwa ajili ya wale wanaotenda kila kitu kwa haki.”

Swali Kuhusu Kufunga

(Mt 9:14-17; Lk 5:33-39)

18 Siku moja wafuasi wa Yohana Mbatizaji na Mafarisayo walikuwa wanafunga. Baadhi ya watu walimjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wafuasi wa Yohana na wafuasi wa Mafarisayo wanafunga, lakini kwa nini wanafunzi wako hawafungi.”

19 Yesu akawajibu, “Katika sherehe ya arusi hutarajii marafiki wa bwana arusi wawe na huzuni wakati yeye mwenyewe yupo pamoja nao. Hakika hawatafunga ikiwa bwana arusi bado yuko pamoja nao. 20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, na wakati huo ndipo watakapofunga.

21 Hakuna anayeshona kiraka kipya cha nguo kwenye vazi la zamani. Ikiwa atafanya hivyo kiraka hicho kipya kitajikunjakunja na kulinyofoa vazi hilo zee nalo litachanika vibaya zaidi. 22 Vivyo hivyo hakuna awekaye divai mpya ndani ya viriba vya zamani[m] vilivyozeeka. Akifanya hivyo, divai ile itachacha na hewa yake itavipasua vibuyu hivyo vya ngozi na kuviharibu kabisa pamoja na divai yenyewe. Badala yake mtu anaweka divai mpya ndani ya vibuyu vipya vya ngozi vya kuwekea divai.”

Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato

(Mt 12:1-8; Lk 6:1-5)

23 Ikatokea kwamba katika siku ya Sabato Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakipita katika mashamba ya nafaka. Wanafunzi wake walianza kuchuma masuke ya nafaka ile walipopita. 24 Baadhi ya Mafarisayo walipoliona hilo wakamwambia Yesu, “Tazama, kwa nini wanafunzi wako wanafanya hivi? Ni kinyume cha sheria kuchuma masuke ya nafaka katika siku ya Sabato?”

25 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma kile alichofanya Daudi pale yeye pamoja na watu aliokuwa nao walipopata njaa na kuhitaji chakula. 26 Ilikuwa wakati wa Abiathari Kuhani Mkuu. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu na kula mkate uliotolewa kwa Bwana. Sheria ya Musa inasema ni makuhani peke yao ndio watakaoweza kuula mkate ule. Daudi aliwapa pia ule mkate mtakatifu watu waliokuwa pamoja naye.”

27 Ndipo Yesu akawaambia mafarisayo, “Siku ya Sabato ilifanywa kwa faida ya watu. Watu hawakuumbwa ili watawaliwe na Sabato. 28 Kwa hiyo Mwana wa Adamu ambaye ni Bwana juu ya kila kitu, pia ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”

Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato

(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)

Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[n] ili wapate sababu ya kumshitaki. Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”

Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.

Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.

Wengi Wamfuata Yesu

Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake hadi Ziwa Galilaya, na kundi kubwa la watu kutoka Galilaya likawafuata, pamoja na watu kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumea, na katika maeneo yote ng'ambo ya Mto Yordani na yale yanayozunguka Tiro na Sidoni. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. Wote walimjia Yesu kwa sababu walikuwa wamesikia mambo aliyokuwa anafanya.

Kwa sababu ya kundi, aliwaambia wanafunzi wake, kumtayarishia mashua mdogo, ili kwamba wasiweze kumsonga na kumbana. 10 Yesu alikuwa ameponya watu wengi. Hivyo wote wale waliokuwa na magonjwa waliendelea kujisogeza mbele kumwelekea ili wamguse. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona Yesu, walianguka chini mbele yake, na kulia kwa sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” 12 Lakini yeye aliwaamuru kila mara wasimwambie mtu yeyote yeye ni nani.

Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili

(Mt 10:1-4; Lk 6:12-16)

13 Kisha Yesu akapanda juu kwenye vilima na akawaita baadhi ya wanafunzi wake, hasa wale aliowataka wajiunge naye pale. 14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume. Aliwachagua ili waambatane pamoja naye, na kwamba aweze kuwatuma sehemu mbalimbali kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu. 15 Pia aliwapa mamlaka ya kufukuza mashetani toka kwa watu. 16 Yafuatayo ni majina ya mitume kumi na wawili aliowateuwa Yesu:

Simoni ambaye Yesu alimwita Petro,

17 Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake (ambao wote Yesu aliwaita Boanergesi), yaani “wana wa ngurumo yenye radi”,

18 Andrea,

Filipo,

Bartholomayo,

Mathayo,

Thomaso,

Yakobo mwana wa Alfayo,

Thadayo,

Simoni Mzelote

19 na Yuda Iskariote,[o] ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu

(Mt 12:22-32; Lk 11:14-23; 12:10)

20 Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. 21 Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili.

22 Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli[p] ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!”

23 Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? 24 Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. 25 Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. 26 Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake.

27 Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo.

28 Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. 29 Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.”

30 Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.”

Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi

(Mt 12:46-50; Lk 8:19-21)

31 Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. 32 Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako[q] nje wanakusubiri.”

33 Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” 34 Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! 35 Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.”

Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu

(Mt 13:1-9; Lk 8:4-8)

Kwa mara nyingine Yesu akaanza kufundisha kando ya ziwa. Umati wa watu ukakusanyika kumzunguka, naye akapanda ndani ya mtumbwi ili akae na kufundisha huku mtumbwi ukielea. Yesu akawafundisha mambo mengi kwa simulizi zenye mafumbo. Katika mafundisho yake alisema:

“Sikilizeni! Mkulima mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akitupa na kuzisambaza mbegu hizo nyingine ikaanguka katika njia, na ndege wakaja na kuila. Mbegu nyingine ikaanguka juu ya uwanja wenye miamba, mahali ambapo hapakuwa na udongo wa kutosha. Hiyo mbegu ilichanua haraka kwani udongo ule haukuwa na kina cha kutosha. Lakini jua lilipochomoza, ule mmea uliungua na kwa sababu haukuwa na mizizi ya kutosha ulinyauka. Mbegu nyingine ilianguka kwenye magugu yenye miiba, na miiba ile ilikua na hatimaye kuibana sana na hivyo haikuzaa chochote. Mbegu nyingine ilianguka kwenye udongo mzuri, nayo ikaota, ikakua na kuzaa matunda; ikazaa mara thelathini, sitini na hata mia zaidi.”

Kisha akasema, “Kila mwenye masikio mazuri ayasikie haya.”

Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha

(Mt 13:10-17; Lk 8:9-10)

10 Yesu alipokuwa peke yake, wale waliomzunguka na wale kumi na wawili walimuuliza kuhusu mifano hiyo.

11 Akawaambia, “Ni ninyi tu mliojaliwa kuzifahamu siri juu ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje nanyi mambo yote yatasemwa kwa simulizi zenye mafumbo, 12 Ili kwamba,

‘japo watatazama
    sana hawataona,
na kwamba japo watasikia
    sana hawataelewa;
vinginevyo,
    wangegeuka na kusamehewa!’”(C)

Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu

(Mt 13:18-23; Lk 8:11-15)

13 Akawaambia, “Hamuelewi mfano huu? Sasa je mtaelewaje mfano wowote nitakaowapa? 14 Mkulima ni badala ya yule anayepanda lile neno la Mungu. 15 Watu wengine ni kama ile mbegu zilizoanguka juu ya njia pale ambapo neno la Mungu limepandwa. Baada ya kulisikia lile neno la Mungu, ndipo Shetani huja haraka na kuyaondoa yale mafundisho ya Mungu yaliyopandwa ndani yao.

16 Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa kwenye eneo lenye mawe mengi. Wanapolisikia neno wanalipokea haraka kwa furaha. 17 Lakini wao wenyewe wanakuwa bado hawajaliruhusu lizame zaidi katika maisha yao. Shida au mateso yanapotokea kwa sababu ya lile neno, kwa haraka sana wanaiacha imani.

18 Watu wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika miiba. Hawa ndio wale wanaolisikia neno, 19 lakini mahangaiko ya maisha haya ya sasa, kuvutiwa na mali, na tamaa mbalimbali zingine huja na kulibana sana lile neno, nalo haliwezi kuwa na matokeo mazuri.[r]

20 Wengine ni kama mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri. Hawa ni wale wanaolisikia neno, na kulipokea na hivyo kuwa na matokeo mazuri; wengine kutoa thelathini, wengine sitini na wengine mia moja zaidi.”

Zingatieni Nuru

(Lk 8:16-18)

21 Yesu akawaambia, “Unapoileta taa ndani[s] je unaiweka chini ya bakuli ama uvungu wa kitanda? Au unaileta ndani na kuiweka juu ya kitako cha taa? 22 Kwani kila kilichofichika kitafunuliwa, na kila kilicho cha siri kitatokea kweupe kwenye mwanga. 23 Yeyote mwenye masikio mazuri ni bora asikie.” 24 Kisha akawaambia, “Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. 25 Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.”[t]

Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Mbegu Inayokua

26 Yesu akasema, “Hivi ndivyo Ufalme wa Mungu unavyofanana: Mtu mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu zake katika udongo shambani. 27 Usiku alienda kulala na asubuhi aliamka na zile mbegu zikiota na kukua; na hakujua jinsi gani hiyo ilifanyika. 28 Ardhi yenyewe inatoa nafaka; kwanza hutoka shina, kisha kinafuata kichwa na mwishoni hutokea nafaka kamili katika kichwa. 29 Nafaka ile inapokuwa imekomaa, basi mkulima huikata kwa fyekeo kwani wakati wa mavuno umekwishafika.”

Simulizi Nyingine ya Ufalme

(Mt 13:31-32,34-35; Lk 13:18-19)

30 Yesu akasema, “Niufanananishe na kitu gani ufalme wa mbinguni? Au tutumie mfano gani kuuelezea? 31 Ni kama mbegu ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko zote inapopandwa ardhini. 32 Lakini inapokuwa imepandwa, inakua na kuwa kubwa sana kuliko mimea yote ya bustanini, na pia hubeba matawi makubwa, kiasi kwamba ndege wa angani wanaweza kupumzika katika kivuli chake.”

33 Kwa mifano mingi kama hii aliendelea kuwafundisha kila kitu kwa kuzingatia uwezo wao wa kuelewa. 34 Yesu hakusema kitu kwao bila kutumia mfano. Lakini alipokuwa peke yake pamoja na wanafunzi wake, alifafanua kila kitu kwao.

Yesu Atuliza Dhoruba

(Mt 8:23-27; Lk 8:22-25)

35 Siku ile ilipofika jioni aliwaambia, “Hebu tuvuke kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.” 36 Kwa hiyo wakaliacha lile kundi. Wakamchukua pamoja nao alipokuwa amerudi katika mtumbwi. Wakati ule ule palikuwepo na mitumbwi mingi mingine ziwani. 37 Dhoruba kubwa ikatokea na mawimbi yalikuwa yanakuja katika pembe zote za mtumbwi. Mtumbwi nao ulikaribia kujaa maji kabisa 38 lakini Yesu alikuwa amelala nyuma ya mtumbwi akiegemea mto. Wakamwaamsha na kumwambia, “Mwalimu je wewe hujali kwamba tunazama?”

39 Kisha akainuka, akaukemea upepo, na akaliamuru ziwa, “Nyamaza Kimya! Tulia!” Upepo ule ukatulia na ziwa nalo likatulia kabisa.

40 Kisha akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Je! Bado hamna imani yoyote?”

41 Lakini walikuwa na woga sana, na wakasemezana wao kwa wao, “Ni nani basi huyu ambaye hata upepo na ziwa vinamtii?”

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu

(Mt 8:28-34; Lk 8:26-39)

Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi.[u] Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe.

Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!”

Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?”

Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi,[v] kwa sababu tuko wengi.” 10 Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile.

11 Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. 12 Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, 13 Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe.[w] Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama.

14 Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. 15 Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. 16 Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. 17 Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile.

18 Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. 19 Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.”

20 Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli[x] mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu.

Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa

(Mt 9:18-26; Lk 8:40-56)

21 Kisha, Yesu alivuka kurudi upande wa magharibi wa ziwa. Pale kundi kubwa la watu lilikusanyika kwake. Yeye alikuwa kando ya ziwa, na 22 mmoja wa viongozi wa sinagogi, aliyeitwa Yairo, alifika pale. Naye alipomwona Yesu, alipiga magoti miguuni pake. 23 Kisha akamwomba kwa msisitizo, akisema, “Binti yangu mdogo yu karibu kufa. Ninakuomba ufike na kumwekea mikono, ili kwamba apone na kuishi.”

24 Hivyo Yesu alienda pamoja naye. Na kundi kubwa la watu lilimfuata; nao walikuwa wakimsonga pande zote kumzunguka.

25 Alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa akitoka damu (kama ilivyo desturi ya wanawake kila mwezi) kila siku kwa miaka kumi na miwili. 26 Huyu alikuwa ameteseka sana akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wengi. Yeye alikuwa ametumia vyote alivyokuwa navyo. Hata hivyo hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi.

27 Wakati aliposikia juu ya Yesu, alimwendea kwa nyuma akiwa katika kundi lile na kuligusa joho lake. 28 Kwani alikuwa akijisemea mwenyewe, “Ikiwa nitagusa tu vazi lake, nitapona.” 29 Mara moja chanzo cha kutoka kwake damu kikakauka, na akajisikia mwilini mwake kwamba amepona matatizo yake. 30 Naye Yesu akatambua mara moja kwamba nguvu zilimtoka. Aligeuka nyuma na kuuliza “Nani aliyegusa mavazi yangu?”

31 Wanafunzi wake wakamwambia, “Uliliona kundi likisukumana kukuzunguka, nawe unauliza, Nani aliyenigusa?”

32 Lakini Yesu aliendelea kuangalia kumzunguka kuona ni nani aliyeyafanya haya. 33 Yule Mwanamke akiwa anatetemeka kwa hofu akijua nini kilichotokea kwake, alikuja na kuanguka mbele yake, akamweleza ukweli wote. 34 Kisha Yesu akamwambia, “Binti yangu imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, na uendelee kupona matatizo yako.”

35 Wakati alipokuwa akizungumza haya watumishi walikuja kutoka nyumbani kwa afisa wa sinagogi. Nao wakamwambia yule afisa, “Binti yako amefariki kwa nini uendelee kumsumbua huyo mwalimu?”

36 Lakini Yesu aliyasikia yale waliyokuwa wakisema, na akamwaambia yule afisa wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”

37 Naye hakumruhusu mtu yeyote kumfuata isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, 38 nao wakaenda katika nyumba ya yule afisa wa sinagogi, na Yesu akaona vurugu na watu wakilia kwa sauti. 39 Yesu aliingia ndani na kuwaambia, “Za nini vurugu zote hizi na vilio hivi? Mtoto hajafa; amelala tu.” 40 Nao wakamcheka.

Yeye aliwatoa nje watu wote, akamchukua baba na mama wa mtoto na wale waliokuwa pamoja naye, akaenda hadi pale alipokuwepo mtoto, 41 akaushika mkono wa mtoto yule na kumwambia “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana mdogo, ninakuambia amka usimame!”) 42 Yule msichana aliinuka mara moja na kuanza kutembea mahali pale. Naye alikuwa na miaka kumi na miwili. Nao mara moja wakaelemewa na mshangao mkubwa. 43 Yeye akawapa amri kuwa mtu yeyote asijue juu ya jambo hili. Kisha akawaambia wampatie msichana yule chakula ale.

Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao

(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)

Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.

Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.

Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake

(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)

Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”

12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[y] wagonjwa wengi na kuwaponya.

Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji

(Mt 14:1-12; Lk 9:7-9)

14 Mfalme Herode alisikia habari hii kwani umaarufu wa Yesu ulikuwa umeenea mahali pote. Watu wengine walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana ana uwezo wa kufanya miujiza.”

15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”

Wengine walisema, “Yeye ni nabii kama mmoja wa manabii wa zamani.”

16 Lakini Herode aliyasikia haya na kusema, “Yohana, yule mtu niliyemkata kichwa, amefufuka kutoka kifo.”

Yohana Mbatizaji Alivyouawa

17 Kwa kuwa Herode mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kumkamata Yohana na kumweka gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mkewe Filipo kaka yake ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Kwani Yohana alizidi kumwambia Herode, “Si halali kwako kisheria kumwoa mke wa kaka yako.” 19 Herodia alikuwa na kisa na Yohana. Hivyo alitaka auwawe, lakini hakuweza kumshawishi Herode kumuua Yohana. 20 Hii ni kwa sababu Herode alimhofu Yohana. Herode pia alifahamu ya kuwa Yohana alikuwa ni mtu mtakatifu na mwenye haki, hivyo akamlinda. Herode alimpomsikia Yohana, alisumbuka sana; lakini alifurahia kumsikiliza.

21 Lakini muda maalumu ukafika; katika siku ya kuzaliwa kwake. Herode aliandaa sherehe ya chakula cha jioni kwa maafisa mashuhuri wa baraza lake, maafisa wake wa kijeshi, na watu maarufu wa Galilaya. 22 Binti ya Herodia alipowasili ndani ya ukumbi alicheza na kumpendeza Herode na wageni aliowaalika katika sherehe hiyo.

Mfalme Herode akamwambia yule msichana, “Uniombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” 23 Akamuahidi: “Nitakupa chochote utakachoniomba, hata nusu ya ufalme wangu!”

24 Naye akatoka na kumwambia mama yake, “Niombe kitu gani?”

Mama yake akasema, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”

25 Yule msichana mara moja aliharakisha kuingia ndani kwa mfalme na kuomba: “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji katika sinia.”

26 Mfalme alisikitika sana. Lakini kwa sababu ya viapo vyake alivyovifanya mbele ya wageni wake chakulani hakutaka kumkatalia ombi lake. 27 Kwa hiyo mfalme mara moja akamtuma mwenye kutekeleza hukumu za kifo akiwa na amri ya kukileta kichwa cha Yohana. Kisha akaenda kukikata kichwa cha Yohana, 28 na kukileta katika sinia na kumpa yule msichana, na msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yohana waliposikia haya walikuja na kuchukua mwili na kuuweka ndani ya kaburi.

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000

(Mt 14:13-21; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)

30 Mitume walikusanyika kumzunguka Yesu, na wakamweleza yote waliyofanya na kufundisha. 31 Kisha Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate peke yenu hadi mahali patulivu na palipo mbali na watu wengine ili mpumzike kidogo”, kwani pale walikuwepo watu wengi wakija na kutoka, nao hawakuwa na nafasi ya kula.

32 Kwa hiyo wakaondoka na mtumbwi kuelekea mahali patulivu na mbali na watu wakiwa peke yao. 33 Lakini watu wengi waliwaona wakiondoka na waliwafahamu wao ni kina nani; kwa hiyo walikimbilia pale kwa njia ya nchi kavu kutoka vitongoji vyote vilivyolizunguka eneo hilo wakafika kabla ya Yesu na wanafunzi wake. 34 Alipotoka katika mashua, Yesu aliona kundi kubwa, na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35 Kwa sasa ilikuwa imekwisha kuwa jioni sana. Kwa hiyo wanafunzi wake walimwijia na kusema, “Hapa ni mahali palipojitenga na sasa hivi saa zimeenda. 36 Uruhusu watu waende zao, ili kwamba waende kwenye mashamba na vijiji vinavyozunguka na waweze kujinunulia kitu cha kula.”

37 Lakini kwa kujibu aliwaambia, “Ninyi wenyewe wapeni kitu cha kula.”

Wao Wakamwambia, “Je, twende kununua mikate yenye thamani ya mshahara wa mtu mmoja[z] wa miezi minane na kuwapa wale?”

38 Yesu akawambia, “Ni mikate mingapi mliyonayo? Nendeni mkaone.”

Walienda kuhesabu, wakarudi kwa Yesu na kusema, “Tunayo mikate mitano na samaki wawili.”

39 Kisha akawaagiza wakae chini kila mmoja kwenye majani mabichi kwa vikundi. 40 Nao wakakaa kwa vikundi vya watu mia na mmoja na vya watu hamsini.

41 Akachukua ile mikate mitano na samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akashukuru na akaimega. Akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. Pia aligawanya samaki wawili miongoni mwao wote.

42 Wakala na wote wakatosheka. 43 Wakachukua mabaki ya vipande vya mikate na samaki na kujaza vikapu kumi na viwili. 44 Na idadi ya wanaume waliokula ile mikate ilikuwa 5,000.

Yesu Atembea Juu ya Maji

(Mt 14:22-33; Yh 6:16-21)

45 Mara Yesu akawafanya wafuasi wake wapande kwenye mashua na wamtangulie kwenda Bethsaida upande wa pili wa ziwa, wakati yeye akiliacha lile kundi liondoke. 46 Baada ya Yesu kuwaaga wale watu, alienda kwenye vilima kuomba.

47 Ilipotimia jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 Naye akawaona wanafunzi wake wakihangaika kupiga makasia, kwani upepo uliwapinga. Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi Yesu aliwaendea akitembea juu ya ziwa. Yeye akiwa karibu kuwapita, 49 wanafunzi wake wakamwona akitembea juu ya ziwa,[aa] na wakafikiri kuwa alikuwa ni mzimu, ndipo walipopiga kelele. 50 Kwa kuwa wote walimwona, na wakaogopa. Mara tu alizungumza nao na kuwaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Usiogope.” 51 Kisha alipanda kwenye mtumbwi pamoja nao, na upepo ukatulia. Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa bado hawajauelewa ule muujiza wa mikate. Kwani fahamu zao zilikuwa zimezibwa.

Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa

(Mt 14:34-36)

53 Walipolivuka ziwa, walifika Genesareti na wakaifunga mashua. 54 Walipotoka katika mashua, watu wakamtambua Yesu, 55 Wakakimbia katika lile jimbo lote na kuanza kuwabeba wagonjwa katika machela na kuwapeleka pale waliposikia kuwa Yesu yupo. 56 Na kila alipoenda vijijini, mijini na mashambani, waliwaweka wagonjwa kwenye masoko, na wakamsihi awaache waguse pindo la koti lake. Na wote walioligusa walipona.

Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu

(Mt 15:1-20)

Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Sheria waliokuja kutoka Yerusalemu walikusanyika mbele zake. Hao wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula chao kwa mikono michafu (yaani bila kuosha mikono yao).

Footnotes

  1. 1:1 Masihi Yaani “Kristo”, tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”. Tazama Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 20 na katika kitabu chote hiki.
  2. 1:1 Mwana wa Mungu Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya.
  3. 1:7 viatu vyake “Mimi sistahili kuwa hata kama mmoja wa watumishi wake anayeinama kumfungua kamba za viatu vyake.”
  4. 1:12 Roho Mtakatifu … nyikani Yaani Yesu aliondoshwa kwa nguvu na kupelekwa nyikani.
  5. 1:15 umewafikia Au “unakuja upesi”, au “umekwisha kuja”.
  6. 1:16 Simoni Jina lingine la Petro lilikuwa Simoni. Pia katika mistari wa 29,30,36.
  7. 1:22 mamlaka Hakuhitaji mamlaka yoyote zaidi ya kwake. Kinyume chake waandishi daima waliwanukuu walimu wa kale wa Kiyahudi kama mamlaka ya mafundisho yao.
  8. 1:34 mashetani … yalimjua Mashetani yalifahamu kuwa Yesu alikuwa ni Masihi, mwana wa Mungu. Tazama Mk 3:11-12.
  9. 1:41 akakasirika Nakala nyingi za Kiyunani zimetumia “Akajawa na huruma …”. Lakini ni vigumu kuelezea kwa nini tafsiri za Kiyunani na zile za Kilatini zimekuwa na “Akijawa na hasira …”, Kwa hiyo wasomi wengi zama za leo hudhani hivyo ndivyo ilivyosomeka awali.
  10. 1:44 akakuchunguze Ama akakukague. Sheria ya Musa iliagiza kwamba kuhani anapaswa kuthibitisha kama mwenye ukoma sasa amepona.
  11. 1:44 aliamuru Yaani alizoagiza Musa tazama Law 14:1-32.
  12. 2:4 kutoboa tundu darini Au “wametoboa tundu darini”.
  13. 2:22 viriba vya zamani Vya kuwekea divai: mfuko uliotengenezwa kwa ngozi za mnyama na kutumika kutunzia divai na mvinyo.
  14. 3:2 Walitaka … siku ya Sabato Haikuruhusiwa kwa Wayahudi kufanya kazi siku ya Sabato na wengi waliamini kumponya mtu ambaye hakuwa katika hatari ya kufa ilikuwa ni kazi.
  15. 3:19 Iskariote Yaweza kuwa “kutoka Kirioti”, mji kusini mwa Yuda.
  16. 3:22 Beelzebuli Kwa maana ya kawaida, “Shetani”. Jina hili limetumika badala ya lile la Shetani.
  17. 3:32 na dada zako wako Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya.
  18. 4:19 haliwezi kuwa na matokeo mazuri Kwa maana ya kawaida, “inakuwa haina matunda”, kwa maana kwamba watu hawa hawafanyi yale mambo mazuri ambayo Mungu anataka watu wafanye.
  19. 4:21 taa ndani Yesu anafananisha mafundisho yake kama taa iliyoletwa chumbani penye giza.
  20. 4:25 Kwa kuwa … nao “Mtu anapoleta taa chumbani, haiweki chini ya kikapu au chini uvunguni mwa kitanda! Badala yake, anaiweka mahali pa juu chumbani. 24 Mzingatie kwa makini kile mnachokisikia. Jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa. Na Mungu atawawezesha muelewe zaidi. 25 Watu walio na uelewa kidogo watapokea zaidi, lakini wale ambao hawakusikiliza vizuri, hata ule uelewa mdogo waliyonao nao utaondolewa kwao. Watasahau kidogo walichoelewa.”
  21. 5:1 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”.
  22. 5:9 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi.
  23. 5:13 nguruwe Watu kijijini walikuwa wakiwatunza nguruwe katika kundi moja kubwa. Kundi hilo lilikuwa chanzo muhimu cha mapato kwa kijiji.
  24. 5:20 Dekapoli Eneo wanaloishi wasio Wayahudi mashariki mwa Galilaya inaloitwa pia Eneo la Miji Kumi.
  25. 6:13 kuwapaka mafuta ya mizeituni Mafuta ya mizeituni yalitumika kama dawa. Ilikuwa pia ni alama ya uponyaji wa Mungu aliopewa Yesu na baadaye wanafunzi wake na Roho Mtakatifu.
  26. 6:37 thamani ya mshahara wa mtu mmoja Kwa Kiyunani vipande 200 vya fedha vimelinganishwa na TKU kama kiasi cha mshahara wa mtu mmoja kwa miezi minane.
  27. 6:49 akitembea juu ya ziwa Watu zama za Marko waliamini kwamba mizimu isingeweza kutembea juu ya maji, lakini waliamini miungu wangeweza kutembea juu ya maji. Watu hao wangeshangaa kuona mitume wa Yesu wakiwa tayari kuamini kitu potovu kabla ya kuamini kuwa Yesu alisimama mbele yao ni Mungu kwani ametembea majini.