Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Msaada kwa Watu wa Mungu Katika Uyahudi
8 Na sasa, kaka na Dada zetu, tunataka kuwaambia kile ambacho neema ya Mungu imefanya katika makanisa ya makedonia. 2 Waamini hawa wamepitia katika masumbufu makubwa, na ni maskini sana. Lakini furaha yao kubwa iliwafanya kuwa wakarimu zaidi katika kutoa kwao. 3 Ninaweza kuwaambia kwamba walitoa kulingana na uwezo wao na hata zaidi ya uwezo wao. Hakuna mtu yeyote aliyewaambia kufanya hivyo. Hilo lilikuwa wazo lao. 4 Walituuliza tena na tena na walitusihi tuwaruhusu kushiriki katika huduma hii kwa ajili ya watu wa Mungu. 5 Na walitoa kwa namna ambayo sisi wenyewe hatukutegemea: kwanza walijitoa wenyewe kwa Mungu na kwetu kabla ya kutoa fedha zao. Hili ndilo Mungu anataka. 6 Kwa hiyo tulimwomba Tito awasaidie ninyi kuikamilisha kazi hii maalum ya kutoa. Tito ndiye aliyeianzisha kazi hii kwanza miongoni mwenu. 7 Ninyi ni matajiri kwa kila kitu; katika imani, katika uwezo wa kuzungumza, katika maarifa, katika utayari wa kusaidia kwa njia yo yote, na katika upendo mliojifunza kutoka kwetu. Hivyo sasa tunawataka muwe matajiri katika kazi hii ya kutoa pia.
© 2017 Bible League International