Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Paulo Aenda Makedonia na Uyunani
20 Ghasia zilipokwisha, Paulo aliwaalika wafuasi wa Bwana kuja kumtembelea. Baada ya kuwatia moyo, aliwaaga na kuondoka kwenda Makedonia. 2 Katika safari yake kupitia Makedonia alikuwa na maneno mengi ya kuwatia moyo wafuasi sehemu mbalimbali. Kisha alikwenda Uyunani 3 na alikaa huko kwa miezi mitatu.
Alipokuwa tayari kutweka tanga kwenda Shamu, baadhi ya Wayahudi walikuwa wanapanga kitu kinyume naye. Hivyo aliamua kurudi nyuma kwenda Shamu kupitia Makedonia. 4 Watu hawa walikuwa wanasafiri pamoja naye: Sopata, mwana wa Piro, kutoka mji wa Berea; Aristarko na Sekundo, kutoka mji wa Thesalonike; Gayo, kutoka mji wa Derbe; Timotheo; na watu wawili kutoka Asia, Tikiko na Trofimo. 5 Watu hawa walimtangulia Paulo. Walitusubiri katika mji wa Troa. 6 Baada ya Siku kuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu tulitweka tanga kutoka katika mji wa Filipi. Tuliwakuta watu hawa katika mji wa Troa siku tano baadaye na tulikaa pale kwa siku saba.
Paulo Atembelea Troa Mara ya Mwisho
7 Siku ya Jumapili[a] sote tulikusanyika pamoja kula Meza ya Bwana.[b] Paulo alizungumza na kundi. Kwa sababu alipanga kuondoka siku iliyofuata, aliendelea kuzungumza mpaka usiku wa manane. 8 Tulikuwa wote kwenye chumba ghorofani na kulikuwa taa nyingi chumbani. 9 Alikuwepo kijana mmoja aliyekuwa amekaa dirishani aliyeitwa Eutiko. Paulo aliendelea kuzungumza, na Eutiko alianza kuchoka na kusikia ungungizi. Mwishowe alisinzia na kuanguka. Alianguka chini, nje kutoka ghorofa ya tatu. Watu walipokwenda kumnyenyua alikuwa amekwisha kufa.
10 Paulo alishuka, akaenda mahali alipokuwa Eutiko, akapiga magoti, na akamkumbatia. Akawaambia waamini wengine, “Msiwe na hofu. Ni mzima yuko hai sasa.” 11 Kisha Paulo akapanda ghorofani, akamega baadhi ya mikate na kula. Alizungumza nao kwa muda mrefu. Alimaliza kuzungumza mapema asubuhi na akaondoka. 12 Wafuasi wa Bwana walimpeleka Eutiko nyumbani akiwa hai, walifarijika sana wote.
Safari Kutoka Troa kwenda Mileto
13 Tulimtangulia Paulo, tukatweka tanga kwenda Asso, tulipanga kumkuta huko. Alitwambia tufanye hivi kwa sababu alitaka kusafiri kwa nchi kavu. 14 Alipotukuta Asso, aliungana nasi na tulipanda meli pamoja naye, na sote tulitweka tanga kwenda Mitelene. 15 Siku iliyofuata, tulitweka tanga kutoka pale na kufika karibu na kisiwa cha Kio. Kisha siku iliyofuata tulitweka tanga kwenda kwenye kisiwa Samosi. Baada ya siku moja tukafika kwenye mji wa Mileto. 16 Paulo alikwisha amua kutosimama Efeso. Hakutaka kukaa Asia kwa muda mrefu. Alikuwa anaharakisha kwa sababu alitaka ikiwezekana awe Yerusalemu siku ya Pentekoste.
© 2017 Bible League International