Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mt 12:22-30; Mk 3:20-27)
14 Wakati mmoja Yesu alikuwa akitoa pepo aliyemfanya mtu ashindwe kuzungumza. Ikawa, pepo alipotoka, yule mtu akaanza kuongea, umati wa watu walishangaa. 15 Lakini baadhi ya watu walisema, “Anatumia nguvu za Shetani kuwatoa pepo. Shetani[a] ni mtawala wa pepo wachafu.”
16 Baadhi ya watu wengine waliokuwa pale walitaka kumjaribu Yesu, walimwomba afanye muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. 17 Lakini alijua walichokuwa wanafikiria, hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe huteketezwa; na familia yenye magomvi husambaratika. 18 Hivyo, ikiwa Shetani anapigana yeye mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Ninawauliza hivi kwa kuwa mnasema kwamba ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani. 19 Lakini ikiwa ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani, watu wenu wanatumia nguvu gani wanapotoa pepo? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa ninyi ni waovu. 20 Lakini, ninatumia nguvu za Mungu kutoa pepo. Hii inaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu sasa.
21 Mwenye nguvu aliye na silaha nyingi anapoilinda nyumba yake, vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake huwa salama. 22 Lakini chukulia kuwa mwenye nguvu zaidi kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yule mwenye nguvu zaidi humnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea kuilinda nyumba yake. Ndipo mwenye nguvu zaidi atavitumia vitu vya yule mtu wa kwanza kadri anavyotaka.
23 Mtu yeyote asiye pamoja nami, yuko kinyume nami. Na mtu yeyote asiyefanya kazi pamoja nami anafanya kinyume nami.
Hatari ya Kuwa Mtupu
(Mt 12:43-45)
24 Mtu anapotokwa na roho chafu, roho hiyo husafiri sehemu zilizo kavu, ikitafuta mahali ili ipumzike. Lakini hukosa mahali pa kupumzika. Hivyo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba nilikotoka.’ 25 Inaporudi hukuta nyumba imesafishwa na kupangwa vizuri. 26 Ndipo roho hiyo chafu huenda ikachukua roho wengine saba, walio waovu kuliko yenyewe. Na kwa pamoja roho zote hizo huingia na kuishi ndani ya mtu huyo, na mtu huyo hupata matatizo mengi kuliko ya kwanza.”
Watu Wanaobarikiwa na Mungu
27 Yesu alipokuwa akisema mambo haya, mwanamke mmoja katika kundi la watu akapaza sauti akamwambia “Amebarikiwa na Mungu mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!”
28 Lakini Yesu akasema, “Wamebarikiwa zaidi wanaosikia na kuyatii mafundisho ya Mungu.”
© 2017 Bible League International