Revised Common Lectionary (Complementary)
Zitumieni Karama za Roho Kulisaidia Kanisa
14 Upendo uwe lengo la maisha yenu, lakini mnapaswa pia kuzitaka karama za Roho. Na itakeni sana karama ya unabii. 2 Nitafafanua ni kwa nini. Wenye karama ya kusema kwa lugha zingine hawazungumzi na watu. Huzungumza na Mungu. Hakuna anayewaelewa kwa sababu huzungumza mambo ya siri kupitia Roho. 3 Lakini wanaotabiri huzungumza na watu. Huwasaidia watu kuwa imara katika imani, na huwatia moyo na kuwafariji. 4 Wanaosema kwa lugha hujiimarisha wao wenyewe. Lakini wanaotabiri huliimarisha kanisa lote.
5 Ningependa ninyi nyote muwe na karama ya kusema kwa lugha zingine. Lakini ninachotaka zaidi ni ninyi kutabiri. Yeyote anayetabiri ni wa muhimu zaidi kuliko wale wanaosema kwa lugha zingine. Hata hivyo, ikiwa wanaweza kufasiri lugha hizo, basi kanisa linasaidiwa kutokana na kile wanachosema.
6 Ndugu zangu, je, itawasaidia nikija kwenu na kusema kwa lugha zingine? Hapana, itawasaidia pale tu nitakapowaletea ufunuo mpya au maarifa fulani, unabii au mafundisho. 7 Hii ni kweli hata kwa vitu visivyo na uhai vinavyotoa sauti kama filimbi na kinubi. Ikiwa muziki hauchezwi kwa ufasaha, hutaweza kujua ni wimbo gani unaopigwa. 8 Na katika vita, ikiwa tarumbeta haitatoa ishara vizuri, askari hawawezi kujua kuwa ni wakati wa kujiandaa kwa mapigano.
9 Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Watu hawataweza kuelewa unachosema, ikiwa utazungumza katika lugha tofauti wasiyoitambua. Utakuwa unazungumza hewani tu! 10 Ni dhahiri kuwa kuna lugha nyingi ulimwenguni, na zote zina maana. 11 Lakini ikiwa sielewi maana ya maneno wanayosema wengine, kwangu itakuwa sauti ya ajabu tu, na nitasikika kama ninayetoa sauti za ajabu. 12 Kwa kuwa mna nia kuhusu karama za Kiroho, muwe na hamu ya kulisaidia kanisa kuwa imara.
© 2017 Bible League International