Revised Common Lectionary (Complementary)
Tunao uzima wa Milele Sasa
13 Ninawaandikia barua hii ninyi mnaomwamini Mwana wa Mungu ili mjue ya kwamba sasa mnao uzima wa milele. 14 Tunaweza kwenda kwa Mungu tukiwa na ujasiri huo. Hii ina maana kuwa tunapomwomba Mungu mambo (na mambo hayo yakakubaliana na matakwa yake kwetu), Mungu huyajali yale tunayosema. 15 Hutusikiliza kila wakati tunapomwomba. Hivyo tunatambua kuwa yeye hutupa kila tunachomwomba.
16 Utakapomwona muumini mwenzio akitenda dhambi (Dhambi isiyomwongoza kwenye mauti), unapaswa kumwombea. Kisha Mungu atampa uzima. Ipo aina ya dhambi inayomwongoza mtu hadi mauti ya milele. Sina maana ya kusema unapaswa kuombea aina hiyo ya dhambi. 17 Daima kutenda yasiyo haki ni dhambi. Lakini ipo dhambi isiyomwongoza mtu katika mauti ya milele.
18 Tunajua kwamba wale waliofanyika watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi. Mwana wa Mungu anawahifadhi salama.[a] Yule Mwovu hawezi kuwagusa. 19 Tunajua kwamba sisi ni wa Mungu, Lakini yule Mwovu anautawala ulimwengu wote. 20 Nasi tunajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja na ametupa uelewa. Hivyo sasa tunaweza kumjua yeye aliye kweli, na tunaishi katika Mungu huyo wa kweli. Nasi tumo ndani ya mwanaye, Yesu Kristo. Yeye ndiye Mungu wa kweli, naye ndiye uzima wa milele. 21 Kwa hiyo, watoto wapendwa, mjiepushe na miungu wa uongo.
© 2017 Bible League International