Revised Common Lectionary (Complementary)
Kielelezo Kutoka Katika Ndoa
7 Ndugu zangu, ninyi nyote mnailewa sheria ya Musa. Hivyo kwa hakika mnafahamu kuwa sheria huwatawala watu wanapokuwa hai tu. 2 Ni kama ambavyo sheria kuhusu ndoa inavyosema: ni lazima mwanamke abaki katika ndoa mume wake akiwa hai. Lakini mume wake akifa, atakuwa amewekwa huru kutoka katika sheria ya ndoa. 3 Iwapo ataolewa na mwanaume mwingine, mume wake akiwa angali hai, sheria inasema kuwa ana hatia ya uzinzi. Lakini mumewe akifa, atakuwa amewekwa huru kutoka katika sheria ya ndoa. Hivyo akiolewa na mwanaume mwingine baada ya mumewe kufa, hatakuwa na hatia ya uzinzi.
4 Kwa njia hiyo hiyo, kaka na dada zangu, mliwekwa huru kutoka katika sheria utu wenu wa zamani ulipokufa pamoja na Kristo. Sasa ninyi ni mali yake yeye yule aliyefufuliwa kutoka kwa wafu. Sote ni mali ya Kristo ili tutumike kwa ajili ya huduma kwa Mungu. 5 Hapo zamani tulitawaliwa na udhaifu wetu wa kibinadamu. Sheria ilitufanya tutake kutenda dhambi. Na tamaa hizo za dhambi ziliitawala miili yetu, na yale tuliyofanya yalituletea mauti ya rohoni. 6 Sasa, kama watu waliokufa, tuko huru kutoka katika sheria iliyotushikilia kama wafungwa. Hivyo hatumtumikii Mungu tena kwa jinsi ya zamani, kwa sheria zilizoandikwa. Sasa tunamtumikia Mungu kwa namna mpya, kwa Roho.
© 2017 Bible League International