Revised Common Lectionary (Complementary)
Karama Kutoka kwa Roho Mtakatifu
12 Na sasa ninataka mwelewe kuhusu karama za Roho Mtakatifu. 2 Mnayakumbuka maisha mliyoishi kabla hamjawa waamini. Mlipotoshwa na kuongozwa kuziabudu sanamu, ambazo hata kuzungumza haziwezi. 3 Hivyo ninawaambia ya kwamba hakuna mtu anayezungumza kwa Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu alaaniwe.” Na hakuna anayeweza kusema “Yesu ni Bwana,” bila msaada wa Roho Mtakatifu.
4 Kuna karama mbalimbali za Roho, lakini zote zinatoka kwa Roho yule yule. 5 Kuna namna mbalimbali za kutumika, lakini sote tunatumika kwa niaba ya Bwana yule yule. 6 Na kuna namna ambazo Mungu hufanya kazi ndani yetu sote, lakini ni Mungu yule yule anayetenda kazi ndani yetu ili tutende kila kitu.
7 Kitu fulani kutoka kwa Roho kinaweza kuonekana ndani ya kila mtu. Roho humpa kila mtu hili ili awasaidie wengine. 8 Roho humpa mtu fulani uwezo wa kuzungumza kwa hekima. Na Roho huyo huyo humpa mwingine uwezo wa kuzungumza kwa maarifa. 9 Roho huyo huyo humpa mtu karama ya imani na humpa mwingine karama ya kuponya. 10 Roho humpa mtu nguvu ya kutenda miujiza, na humpa mwingine uwezo wa kutabiri, na mwingine uwezo wa kupambanua kujua kilichotoka kwa Roho na ambacho hakikutoka kwa Roho. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kusema kwa lugha zingine tofauti, na humpa mwingine uwezo wa kufasiri lugha hizo. 11 Roho mmoja, Roho yule yule hufanya mambo yote haya. Roho ndiye huamua ampe nini kila mtu.
Arusi Katika Mji wa Kana
2 Siku tatu baadaye kulikuwa na arusi katika mji wa Kana huko Galilaya, mama yake Yesu naye pia alikuwapo. 2 Yesu na wafuasi wake nao walialikwa. 3 Hapo arusini divai ilipungua, mama yake Yesu akamwambia mwanaye, “Hawana divai ya kutosha.”
4 Yesu akajibu, “Mama, kwa nini unaniambia mambo hayo? Wakati sahihi kwangu kufanya kazi haujafika bado.”
5 Mama yake akawaambia wahudumu wa arusi, “Fanyeni lo lote lile atakalowaambia.”
6 Mahali hapo ilikuwepo mitungi mikubwa sita iliyotengenezwa kwa mawe iliyotumiwa na Wayahudi katika desturi yao maalumu ya kunawa.[a] Kila mtungi mmoja ulikuwa na ujazo wa lita 80 au 120.[b]
7 Yesu akawaambia wale wahudumu, “Ijazeni maji hiyo mitungi.” Nao wakaijaza maji mpaka juu.
8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kiasi na mumpelekee mkuu wa sherehe.” Nao wakafanya kama walivyoambiwa. 9 Mkuu wa sherehe akayaonja yale maji, ambayo tayari yamegeuka na kuwa divai. Naye hakujua wapi ilikotoka hiyo divai, bali wahudumu walioleta yale maji wao walijua. Akamwita bwana arusi 10 na kumwambia, “Watu wanapoandaa huleta kwanza divai iliyo bora zaidi. Baadaye, wageni wanapokuwa wametosheka, huleta divai iliyo na ubora pungufu. Lakini wewe umeandaa divai bora zaidi hadi sasa.”
11 Ishara hii ilikuwa ya kwanza aliyoifanya Yesu katika mji wa Kana ya Galilaya. Kwa hili Yesu alionesha ukuu wake wa kimungu, na wafuasi wake wakamwamini.
© 2017 Bible League International