Revised Common Lectionary (Complementary)
22 Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23 Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24 Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. 25 Daudi alilisema hili kuhusu Yesu:
‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami.
Yupo hapa pembeni yangu,
hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru.
26 Ndiyo sababu ninafurahi sana,
na ninaimba kwa furaha!
Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu,
27 kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini.[a]
Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu[b] kuozea huko.
28 Umenionyesha njia iendayo uzimani.
Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’(A)
29 Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. 30 Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme.[c] 31 Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme ajaye:
‘Hakuachwa kaburini.
Mwili wake haukuozea humo.’[d]
Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu. 32 Yesu ndiye ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi sote ni mashahidi wa jambo hili. Tulimwona. 33 Yesu alichukuliwa juu mbinguni. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu. Baba amempa Roho Mtakatifu, kama alivyoahidi. Hivyo Yesu amemimina huyo Roho Mtakatifu na hiki ndicho mnachoona na kusikia 34 Daudi hakuchukuliwa mpaka mbinguni. Daudi mwenyewe alisema,
‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kuume
35 hadi nitakapowaweka maadui zako chini ya udhibiti wako.’[e](B)
36 Hivyo, watu wote wa Israeli wanapaswa kulijua hili bila kuwa na mashaka: Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na Masihi. Ndiye yule mliyempigilia msalabani!”
© 2017 Bible League International