Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Revised Common Lectionary (Complementary)

Daily Bible readings that follow the church liturgical year, with thematically matched Old and New Testament readings.
Duration: 1245 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Gen for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Error: Book name not found: Ps for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Wakolosai 1:15-28

Mwana wa Mungu yu sawa na Mungu

15 Hakuna anayeweza kumwona Mungu,
    lakini Mwana anafanana kabisa na Mungu.
    Anatawala juu ya kila kitu kilichoumbwa.
16 Kwa uweza wake, vitu vyote viliumbwa:
    vitu vya angani na ardhini, vinavyoonekana na visivyoonekana,
watawala wote wa kiroho, wakuu, enzi, na mamlaka.
    Kila kitu kiliumbwa kupitia Yeye na kwa ajili yake.

17 Mwana alikuwapo kabla ya kuumbwa kitu chochote,
    na vyote vinaendelea kuwepo kwa sababu yake.
18 Yeye ni kichwa cha mwili,
    yaani kanisa.
Yeye ni mwanzo wa maisha yajayo,
    ni wa kwanza miongoni mwa wote watakaofufuliwa kutoka kwa wafu.[a]
    Hivyo katika mambo yote yeye ni mkuu zaidi.

19 Mungu alipendezwa kwamba ukamilifu wa uungu wake
    uishi ndani ya Mwana.
20 Na kupitia Yeye, Mungu alifurahi
    kuvipatanisha tena vitu vyote kwake Yeye mwenyewe;
    vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani.
Mungu alileta amani kupitia sadaka ya damu ya Mwanaye msalabani.

21 Hapo mwanzo mlitengwa na Mungu, na mlikuwa adui zake katika fikra zenu, kwa sababu ya maovu mliyotenda kinyume naye. 22 Lakini sasa amewafanya kuwa marafiki zake tena, kupitia kifo cha Kristo katika mwili wake. Ili kwa njia hiyo awalete kwake mkiwa watakatifu, msio na lawama na msiohukumiwa jambo lolote mbele zake; 23 na hiki ndicho kitatokea mkiendelea kuiamini Habari Njema mliyoisikia. Mwendelee kuwa imara na kudumu katika imani. Jambo lolote lisiwafanye mkaliacha tumaini lenu mlilopokea mlipoisikia Habari Njema. Habari Njema ile ile ambayo imehubiriwa kwa kila mtu duniani, ndiyo kazi ambayo mimi, Paulo, nilipewa kufanya.

Kazi ya Paulo kwa Ajili ya Kanisa

24 Nina furaha kwa sababu ya mateso ninayopata kwa manufaa yenu. Yapo mambo mengi ambayo kupitia hayo Kristo bado anateseka. Nami ninayapokea mateso haya kwa furaha katika mwili wangu kwa ajili ya mwili wake, yaani Kanisa. 25 Nilifanyika kuwa mtumishi wa kanisa kwa sababu Mungu alinipa kazi maalum ya kufanya. Kazi hii inawasaidia ninyi, nayo ni kuuhubiri ujumbe kamili wa Mungu. 26 Ujumbe huu ni ukweli wenye siri uliofichwa tangu mwanzo wa nyakati. Nao ulifichwa kutoka kwa kila mtu kwa muda mrefu, lakini sasa umedhihirishwa kwa watakatifu wa Mungu. 27 Mungu aliamua kuwajulisha watu wake namna Kweli hii ilivyo na utajiri na utukufu. Siri hii ya kweli hii, ambayo ni kwa ajili ya watu wote, ni kwamba Kristo anaishi ndani yenu. Yeye ndiye tumaini la kushiriki katika utukufu wake. 28 Hivyo tunaendelea kuwaambia watu juu ya Kristo. Tunatumia hekima yote kumshauri na kumfundisha kila mtu. Tunajaribu kumleta kila mtu mbele za Mungu kama watu waliokomaa kiroho katika uhusiano wao na Kristo.

Luka 10:38-42

Maria na Martha

38 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanasafiri, walifika katika kijiji kimoja. Mwanamke aitwaye Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Mariamu. Mariamu alikuwa amekaa karibu na Yesu akimsikiliza anavyofundisha. 40 Lakini Martha dada yake Mariamu alikuwa anashughulisha na shughuli mbalimbali zilizotakiwa kufanywa. Martha aliingia ndani na akasema, “Bwana, hujali kuona mdogo wangu ameniacha nifanye kazi zote peke yangu? Mwambie aje kunisaidia.”

41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unasumbuka na kuhangaika kwa shughuli nyingi. 42 Lakini kitu kimoja tu ndicho cha lazima. Mariamu amefanya uchaguzi sahihi na kamwe hautachukuliwa kutoka kwake.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International