Revised Common Lectionary (Complementary)
Paulo Apanga Safari
21 Baada ya hili, Paulo alipanga kwenda Yerusalemu. Alipanga kupitia katika majimbo ya Makedonia na Akaya kisha kwenda Yerusalemu. Alisema, “Baada ya kwenda Yerusalemu, ni lazima niende Rumi pia.” 22 Timotheo na Erasto walikuwa wasaidizi wake wawili. Paulo aliwatuma watangulie Makedonia. Lakini yeye alikaa Asia kwa muda.
Tatizo Katika Mji wa Efeso
23 Lakini katika wakati huo huo kulikuwepo tatizo kuhusiana na Njia. Hivi ndivyo ilivyotokea: 24 Alikuwepo mtu aliyeitwa Demetrio aliyekuwa mfua fedha. Alikuwa akitengeneza sanamu ndogo za fedha zilizofanana na hekalu la Artemi, mungu mke. Wanaume waliokuwa wakifanya kazi hii walijipatia pesa nyingi sana.
25 Demetrio alifanya mkutano na watu hawa pamoja na wengine waliokuwa wanafanya kazi ya aina hiyo. Akawaambia, “Ndugu, mnafahamu kuwa tunapata pesa nyingi kutokana na kazi yetu. 26 Lakini angalieni kitu ambacho mtu huyu Paulo anafanya. Sikilizeni anachosema. Amewashawishi watu wengi katika Efeso na karibu Asia yote kubadili dini zao. Anasema miungu ambayo watu wanatengeneza kwa mikono si miungu wa kweli. 27 Ninaogopa hili litawafanya watu kuwa kinyume na biashara yetu. Lakini kuna tatizo jingine pia. Watu wataanza kufikiri kuwa hekalu la Artemi, mungu wetu mkuu halina maana. Ukuu wake utaharibiwa. Na Artemi ni mungu mke anayeabudiwa na kila mtu katika Asia na ulimwengu wote.”
© 2017 Bible League International