Revised Common Lectionary (Complementary)
Yesu Aonya Kuhusu Matatizo
(Mk 13:9-13; Lk 21:12-17)
16 Sikilizeni! Ninawatuma, nanyi mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Hivyo muwe na akili kama nyoka. Lakini pia muwe kama njiwa na msimdhuru yeyote. 17 Muwe waangalifu! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka ili kuwashitaki mbele ya mabaraza ya mijini. Watawachapa ndani ya masinagogi yao. 18 Mtasimamishwa mbele ya magavana na wafalme. Watu watawafanyia ninyi hivi kwa sababu mnanifuata. Mtakuwa mashahidi wangu mbele za wafalme na magavana hao na kwa watu wa mataifa mengine. 19 Mtakapokamatwa, msisumbuke kuhusu nini mtakachosema au namna gani mtakavyosema. Katika wakati huo mtapewa maneno ya kusema. 20 Si ninyi mtakaoongea; Roho wa Baba Mungu wenu atakuwa anaongea kupitia ninyi.
21 Ndugu watakuwa kinyume cha ndugu zao wenyewe na kuwapeleka kwenda kuuawa. Baba watawapeleka watoto wao wenyewe kuuawa. Watoto watapigana kinyume na wazazi wao na watawapeleka kuuawa. 22 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 23 Mnapotendewa vibaya katika mji mmoja, nendeni katika mji mwingine. Ninawaahidi kuwa hamtamaliza kwenda katika miji ya Israeli kabla Mwana wa Adamu hajarudi.
24 Wanafunzi si wazuri kuliko mwalimu wao. Watumwa si wazuri kuliko bwana wao. 25 Inatosha kwa wanafunzi kuwa kama walimu wao na watumwa kuwa kama bwana wao. Iwapo watu hao wananiita ‘mtawala wa pepo’, na mimi ni kiongozi wa familia, basi ni dhahiri kwa kiasi gani watawatukana ninyi, mlio familia yangu!
© 2017 Bible League International