Revised Common Lectionary (Complementary)
Yesu, Mwana wa Adamu Atawahukumu Watu Wote
31 Mwana wa Adamu atakuja akiwa katika utukufu wake, pamoja na malaika wote. Ataketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa mfalme. 32 Watu wote wa ulimwenguni watakusanywa mbele zake, kisha atawagawa katika makundi mawili. Itakuwa kama mchungaji anavyowatenga kondoo kutoka katika kundi la mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wa kushoto.
34 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kuume, ‘Njooni, baba yangu ana baraka kuu kwa ajili yenu. Ufalme alioahidi ni wenu sasa. Uliandaliwa kwa ajili yenu tangu dunia ilipoumbwa. 35 Ni wenu kwa sababu nilipokuwa na njaa, mlinipa chakula. Nilipokuwa na kiu, mlinipa maji ya kunywa. Nilipokosa mahali pa kukaa, mlinikaribisha katika nyumba zenu. 36 Nilipokosa nguo, mlinipa mavazi ya kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa, mlinijali. Nilipofungwa gerezani, mlikuja kunitembelea.’
37 Kisha wenye haki watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakupa chakula? Lini tulikuona una kiu tukakupa maji ya kunywa? 38 Lini tulikuona huna mahali pa kukaa tukakukaribisha katika nyumba zetu? Lini tulikuona huna nguo za kuvaa na tukakuvisha? 39 Lini tulikuona unaumwa au uko gerezani tukaja kukuona?’
40 Kisha mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, kila mlichowafanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si watu wa thamani, mlinifanyia mimi pia.’
41 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu. Mungu amekwisha amua kuwa mtaadhibiwa. Nendeni katika moto uwakao milele, moto ulioandaliwa kwa ajili ya yule Mwovu na malaika zake. 42 Ondokeni kwa sababu nilipokuwa na njaa, hamkunipa chakula nile. Nilipokuwa na kiu, hamkunipa maji ya kunywa. 43 Nilipokosa mahali pa kukaa, hamkunikaribisha katika nyumba zenu. Nilipokosa nguo za kuvaa, hamkunipa nguo za kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa au mfungwa gerezani hamkunijali.’
44 Ndipo watu hao watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu? Lini tulikuona huna mahali pa kukaa? Au ni lini tulikuona huna nguo au mgonjwa au ukiwa gerezani? Tuliona haya yote lini na hatukukusaidia?’
45 Mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, chochote mlichokataa kumfanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si wa muhimu, mlikataa kunifanyia mimi.’
46 Ndipo watu hawa watakapondolewa ili kuadhibiwa milele. Lakini wenye haki watakwenda kuyafurahia maisha ya milele.”
© 2017 Bible League International