Old/New Testament
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Yh 11:47-53)
22 Ilikuwa karibu ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, inayoitwa Pasaka. 2 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walitaka kumwua Yesu kwa siri kwa sababu waliogopa kile ambacho watu wangefanya.
Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu
(Mt 26:14-16; Mk 14:10-11)
3 Mmoja wa mitume kumi na wawili wa Yesu aliitwa Yuda Iskariote. Shetani alimwingia Yuda, 4 akaondoka, akaenda kuongea na viongozi wa makuhani na baadhi ya wakuu wa askari walinzi wa Hekalu. Aliongea nao kuhusu namna ya kumkabidhi Yesu kwao. 5 Makuhani walifurahia sana hili. Wakaahidi kumlipa Yuda pesa ikiwa angefanya hivi. 6 Akakubali, kisha alianza kusubiri muda mzuri wa kumkabidhi Yesu kwao. Alitaka kumkabidhi Yesu kwao wakati hakuna kundi la watu ambao wangeona.
Karamu ya Pasaka
(Mt 26:17-25; Mk 14:12-21; Yh 13:21-30)
7 Siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu[a] ilifika. Hii ni siku ambayo Wayahudi daima walichinja kondoo kwa ajili ya Pasaka. 8 Yesu aliwaambia Petro na Yohana, “Nendeni mkaandae mlo wa Pasaka ili tule.”
9 Wakamwambia, “Unataka tukauandae wapi?”
Akawaambia, 10 “Mtakapokuwa mnaingia mjini, mtakutana na mtu amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. Ataingia katika nyumba. 11 Mwambieni mmiliki wa nyumba, ‘Mwalimu anakuomba tafadhali utuoneshe chumba ambacho yeye na wafuasi wake wanaweza kulia mlo wa Pasaka.’ 12 Mmiliki atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilicho tayari kwa ajili yetu. Andaeni mlo humo.”
13 Hivyo Petro na Yohana wakaondoka. Kila kitu kilitokea kama Yesu alivyosema. Na hivyo wakauandaa mlo wa Pasaka.
Chakula cha Bwana
(Mt 26:26-30; Mk 14:22-26; 1 Kor 11:23-25)
14 Wakati ulifika kwa wao kula mlo wa Pasaka. Yesu na mitume walikuwa wamekaa pamoja kuzunguka meza ya chakula. 15 Yesu akawaambia, “Nilitaka sana kula mlo huu wa Pasaka pamoja nanyi kabla sijafa. 16 Sitakula mlo mwingine wa Pasaka mpaka itakapopewa maana yake kamili katika ufalme wa Mungu.”
17 Kisha Yesu akachukua kikombe kilichokuwa na divai. Akamshukuru Mungu, na akasema, “Chukueni kikombe hiki na kila mmoja anywe. 18 Sitakunywa divai tena mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19 Kisha akaichukua baadhi ya mkate na akamshukuru Mungu. Akaigawa vipande vipande, akawapa vipande mitume na kusema, “Mkate huu ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili yenu. Kuleni kwa kunikumbuka.” 20 Katika namna ile ile, baada ya kula chakula, Yesu akachukua kikombe chenye divai na akasema, “Divai hii inawakilisha Agano Jipya kutoka kwa Mungu kwa watu wake. Litaanza pale damu yangu itakapomwagika kwa ajili yenu.”[b]
Nani Atamsaliti Yesu?
21 Yesu akasema, “Lakini hapa mezani kuna mkono wa yule atakayenisaliti kwa adui zangu. 22 Mwana wa Adamu atakufa kama Mungu alivyoamua. Lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe.”
23 Ndipo mitume wakaulizana, “Ni nani miongoni mwetu atafanya hivyo?”
Iweni Kama Mtumishi
24 Baadaye, mitume wakaanza kubishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu. 25 Lakini Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa wanawatawala watu kama watumwa wao, na wenye mamlaka juu ya wengine wanataka kuitwa, ‘Wafadhili Wakuu’. 26 Lakini ni lazima msiwe hivyo. Aliye na mamlaka zaidi miongoni mwenu lazima awe kama asiye na mamlaka. Anayeongoza anapaswa kuwa kama anayetumika. 27 Nani ni mkuu zaidi: Yule anayetumika au yule aliyekaa mezani na kuhudumiwa? Kila mtu hudhani ni yule aliyekaa mezani akihudumiwa, sawa? Lakini nimekuwa pamoja nanyi kama ninayetumika.
28 Na ninyi ndiyo mliobaki pamoja nami katika mahangaiko mengi. 29 Hivyo ninawapa mamlaka kutawala pamoja nami katika ufalme ambao Baba yangu amenipa. 30 Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme huo. Mtakaa katika viti vya enzi na kuwahukumu makabila kumi na mbili ya Israeli.
© 2017 Bible League International