Old/New Testament
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
27 Sasa ninapata taabu sana rohoni mwangu. Nisemeje? Je, niseme, ‘Baba niokoe katika wakati huu wa mateso’? Hapana, nimeufikia wakati huu ili nipate mateso. 28 Baba yangu, ufanye yale yatakayokuletea wewe utukufu!”
Kisha sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Tayari nimekwisha upata utukufu wangu. Nitaupata tena.”
29 Watu waliokuwa wamesimama hapo wakaisikia sauti hiyo. Wakasema ilikuwa ni ngurumo. Lakini wengine wakasema, “Malaika amesema naye!”
30 Yesu akasema, “Sauti hiyo ilikuwa ni kwa ajili yenu si kwa ajili yangu. 31 Sasa ni wakati wa ulimwengu kuhukumiwa. Sasa mtawala wa ulimwengu[a] huu atatupwa nje. 32 Nami nitainuliwa juu[b] kutoka katika nchi. Mambo hayo yatakapotokea, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33 Yesu alisema hili kuonesha jinsi ambavyo atakufa.
34 Watu wakasema, “Lakini sheria yetu inasema kwamba Masihi ataishi milele. Sasa kwa nini unasema, ‘Ni lazima Mwana wa Adamu ainuliwe juu’? Ni nani huyu ‘Mwana wa Adamu’?”
35 Kisha Yesu akasema, “Nuru[c] itabaki pamoja nanyi kwa muda mfupi tu. Kwa hiyo mtembee mkiwa bado na hiyo nuru. Hapo giza[d] halitaweza kuwakamata. Watu wanaotembea gizani hawajui kule wanakoenda. 36 Hivyo wekeni matumaini yenu katika nuru wakati bado mkiwa nayo. Jinsi hiyo mtakuwa watoto wa nuru.” Yesu alipomaliza kusema mambo hayo, aliondoka na kwenda mahali ambapo watu wasingeweza kumwona.
Baadhi ya Wayahudi Wakataa Kumwamini Yesu
37 Watu wakaona ishara[e] hizi zote alizozifanya Yesu, lakini bado hawakumwamini. 38 Haya yalikuwa hivyo ili kuthibitisha yale aliyoyasema nabii Isaya kuwa:
“Bwana, ni nani aliyeamini yale tuliyowaambia?
Ni nani aliyeziona nguvu za Bwana?”(A)
39 Hii ndiyo sababu watu hawakuweza kuamini. Kwani Isaya alisema pia,
40 “Mungu aliwafanya baadhi ya watu wasione.
Aliufunga ufahamu wao.
Alifanya hivi ili wasiweze kuona kwa macho yao
na kuelewa kwa ufahamu wao.
Alifanya hivyo ili wasiweze kugeuka
na kuponywa.”(B)
41 Isaya alisema hivi kwa sababu aliuona ukuu wa Mungu[f] ndani ya Yesu. Naye alizungumza habari zake Yesu.
42 Lakini watu wengi wakamwamini Yesu. Hata wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi wakamwamini, lakini walikuwa na hofu juu ya Mafarisayo, hivyo hawakusema kwa uwazi kwamba wameamini. Hao walikuwa na hofu kwamba wangeamriwa watoke na kukaa nje ya sinagogi. 43 Wao walipenda kusifiwa na watu zaidi kuliko kupata sifa zinazotoka kwa Mungu.
Mafundisho ya Yesu Yatawahukumu Watu
44 Kisha Yesu akapaza sauti, “Mtu yeyote anayeniamini basi kwa hakika anamwamini yule aliyenituma. 45 Yeyote anayeniona mimi hakika anamwona yeye aliyenituma. 46 Nimekuja katika ulimwengu huu kama mwanga. Nimekuja ili kila mmoja atakayeniamini asiendelee kuishi katika giza.
47 Sikuja ulimwenguni humu kuwahukumu watu. Nimekuja ili kuwaokoa watu wa ulimwengu huu. Hivyo mimi siye ninayewahukumu wale wanaosikia mafundisho yangu bila kuyafuata. 48 Isipokuwa yupo hakimu wa kuwahukumu wote wanaokataa kuniamini na wasiokubaliana na yale ninayoyasema. Ujumbe ninaousema utawahukumu ninyi siku ya mwisho. 49 Hiyo ni kwa sababu yale niliyofundisha hayakutoka kwangu. Baba aliyenituma ndiye aliyeniambia yale nitakayosema na kuyafundisha. 50 Nami najua amri za Mungu kwamba lolote alisemalo na kutenda litawaletea watu uzima wa milele, kama watazifanya. Hivyo mambo ninayosema ni yale ambayo Baba yangu ameniambia niyaseme.”
© 2017 Bible League International