Old/New Testament
Petro Atajaribiwa na Kushindwa
(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Yh 13:36-38)
31 Shetani ameomba ili awapepete kwa nguvu kama mkulima anavyopepeta ngano kwenye ungo ili mwanguke. Simoni, Simoni,[a] 32 nimekuombea ili usipoteze imani yako! Wasaidie ndugu zako kuwa imara utakaponirudia.”
33 Lakini Petro akamwambia Yesu, “Bwana, niko tayari kufungwa gerezani pamoja nawe. Hata kufa pamoja nawe!”
34 Lakini Yesu akasema, “Petro, asubuhi kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.”
Iweni Tayari kwa Matatizo
35 Kisha Yesu akawaambia mitume, “Kumbukeni nilipowatuma bila pesa, mkoba, wala viatu. Je, mlipungukiwa chochote?”
Mitume wakajibu, “Hapana.”
36 Yesu akawaambia, “Lakini sasa kama una pesa au mkoba, uchukue pamoja nawe. Kama huna upanga, uza koti lako ukanunue. 37 Maandiko yanasema, ‘Alidhaniwa kuwa mhalifu.’(A) Maandiko haya lazima yatimizwe. Yaliyoandikwa kuhusu mimi yanatimilika sasa.”
38 Wafuasi wakasema, “Tazama Bwana, hapa kuna panga mbili.”
Yesu akawaambia, “Nyamazeni, acheni mazungumzo ya namna hiyo!”
Yesu Aomba Akiwa Peke Yake
(Mt 26:36-46; Mk 14:32-42)
39-40 Yesu akaondoka mjini akaenda Mlima wa Mizeituni. Wafuasi wake wakaenda pamoja naye. (Alikuwa akienda huko mara kwa mara.) Akawaambia wafuasi wake, “Ombeni ili mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
41 Kisha Yesu akaenda kama hatua hamsini mbali nao. Akapiga magoti na akaomba akisema, 42 “Baba, ukiwa radhi, tafadhali usinifanye ninywe katika kikombe[b] hiki. Lakini fanya unalotaka wewe, siyo ninalotaka mimi.” 43 Kisha malaika kutoka mbinguni akaja akamtia nguvu. 44 Yesu aliomba kwa nguvu zaidi na kustahimili zaidi kama mpiganaji wa mieleka akiwa katika mapambano makali. Jasho kama matone ya damu likadondoka kutoka kwenye uso wake.[c] 45 Alipomaliza kuomba, alikwenda kwa wafuasi wake. Akawakuta wamelala, wamechoka kwa sababu ya huzuni. 46 Yesu akawaambia, “Kwa nini mnalala? Amkeni, ombeni mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
© 2017 Bible League International