Old/New Testament
Petro na Kornelio
10 Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. 2 Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. 3 Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!”
4 Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?”
Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. 5 Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 6 Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” 7 Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. 8 Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa.
9 Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa[a] kuomba. 10 Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. 11 Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. 12 Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. 13 Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.”
14 Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.”
15 Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” 16 Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. 17 Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani.
Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. 18 Waliuliza, “Je, Simoni Petro yuko hapa?”
19 Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. 20 Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” 21 Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?”
22 Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” 23 Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo.
Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye.
© 2017 Bible League International