Old/New Testament
23 Hivyo baada ya askari kumpigilia Yesu kwa misumari msalabani, walizichukua nguo zake na kuzigawa katika mafungu manne. Kila askari alipata fungu moja. Pia wakalichukua vazi lake lililokuwa limefumwa kwa kipande kimoja tu cha kitambaa kutoka juu hadi chini. 24 Hivyo askari wakasemezana wao kwa wao, “Hatutalichana vazi hili vipande vipande. Hebu tulipigie kura kuona nani atakayelipata.” Hili lilitokea ili kuweka wazi maana kamili ya yale yanayosemwa katika Maandiko:
“Waligawana miongoni mwao mavazi yangu,
na wakakipigia kura kile nilichokuwa nimevaa.”(A)
Hivyo ndivyo maaskari walivyofanya.
25 Mama yake Yesu alisimama karibu na msalaba wa mwanawe, Dada yake mamaye Yesu pia alikuwa amesimama pale pamoja na Mariamu mke wake Kleopa, na Mariamu Magdalena. 26 Yesu akamwona mama yake na akamwona pia mfuasi aliyempenda sana akisimama pale. Akamwambia mama yake, “Mama mpendwa, mwangalie huyo, naye ni mwanao sasa.” 27 Kisha akamwambia yule mfuasi, “Huyu hapa ni mama yako sasa.” Kisha baada ya hayo, mfuasi huyo akamchukua mama yake Yesu na kuishi naye nyumbani kwake.
Yesu Afariki
(Mt 27:45-56; Mk 15:33-41; Lk 23:44-49)
28 Baadaye, Yesu akajua kuwa kila kitu kimekwisha kamilika. Ili kuyafanya Maandiko yatimie akasema, “Nina kiu.”[a] 29 Palikuwapo na bakuli lililojaa siki[b] mahali pale, wale askari wakachovya sponji ndani yake. Wakaiweka ile sponji kwenye tawi la mwanzi na kuliinua hadi kinywani kwa Yesu. 30 Alipoionja ile siki, akasema, “Imekwisha.” Baada ya hapo akainamisha kichwa chake na kufa.
31 Hii ilikuwa Ijumaa, Siku ya Matayarisho. Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya Sabato maalumu. Viongozi wa Kiyahudi hawakuitaka ile miili ya waliosulubiwa ikae juu misalabani katika siku ya Sabato. Hivyo wakamwomba Pilato atoe amri kuwa miguu ya wale watu misalabani ivunjwe. Pia wakaomba ile miili ishushwe kutoka kwenye misalaba. 32 Kwa hiyo askari wakaja na kuivunja miguu[c] ya watu wale wawili kwenye misalaba kando ya Yesu. 33 Lakini askari walipomkaribia Yesu, wakaona kuwa tayari alikuwa amekwisha kufa. Hivyo hawakuivunja miguu yake.
34 Lakini mmoja wa askari akauchoma ubavu wa Yesu kwa mkuki wake. Mara hiyo hiyo damu na maji vikamtoka mwilini mwake. 35 (Yeye aliyeona haya yakitokea ametueleza. Aliyaeleza haya ili ninyi pia muweze kuamini. Mambo anayosema ni ya kweli. Yeye anajua kuwa anasema kweli.) 36 Mambo haya yalitokea ili kutimiza Maandiko yaliyosema, “Hakuna mfupa wake utakaovunjwa”[d] 37 na “Watu watamwangalia yeye waliyemchoma.”(B)
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Lk 23:50-56)
38 Baadaye, mtu mmoja aliyeitwa Yusufu wa kutoka Arimathaya akamwomba Pilato mwili wa Yesu. (Yusufu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini hakumweleza mtu yeyote, kwa sababu aliwaogopa viongozi wa Kiyahudi.) Pilato akasema Yusufu anaweza kuuchukua mwili wa Yesu, hivyo naye akaja na kuuchukua.
39 Nikodemu akaenda pamoja na Yusufu. Nikodemu, alikuwa ni yule mtu aliyekuja kwa Yesu hapo kabla na kuzungumza naye usiku. Huyu alileta kadiri ya lita[e] mia moja ya marashi yenye mchanganyiko wa manemane na uvumba. 40 Watu hawa wawili wakauchukua mwili wa Yesu na wakauzungushia vipande vya sanda ya kitani pamoja na marashi yale. (Hivi ndivyo Wayahudi walivyowazika watu.) 41 Pale msalabani sehemu alipouawa Yesu, palikuwepo na bustani. Katika bustani ile palikuwemo na kaburi[f] jipya la kuzikia. Hakuna mtu aliyewahi kuzikwa ndani ya kaburi lile. 42 Wanaume wakauweka mwili wa Yesu katika kaburi lile kwa kuwa lilikuwa karibu, na Wayahudi walikuwa wakijiandaa kuianza siku yao ya Sabato.
© 2017 Bible League International