Old/New Testament
22 Watu wale walipokwenda gerezani, hawakuwaona mitume. Hivyo walirudi na kuwaambia viongozi wa Kiyahudi kuhusu hili. 23 Walisema, “Gereza lilikuwa limefungwa na milango ilikuwa imefungwa. Walinzi walikuwa wamesimama milangoni. Lakini tulipofungua milango, gereza lilikuwa tupu!” 24 Mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani walipolisikia hili, walichanganyikiwa na kujiuliza maana yake ni nini.
25 Ndipo mtu mwingine akaja na kuwaambia, “Sikilizeni! Watu mliowafunga gerezani wamesimama katika eneo la Hekalu wanawafundisha watu!” 26 Mkuu wa walinzi na askari walinzi wa Hekalu walikwenda na kuwarudisha mitume. Lakini askari hawakutumia nguvu, kwa sababu waliwaogopa watu. Waliogopa watu wangewapiga kwa mawe mpaka wafe.
27 Askari waliwaleta mitume na kuwasimamisha mbele ya baraza. Kuhani mkuu akawauliza. 28 Akisema, “Tuliwaambia msifundishe tena kwa kutumia jina lile. Lakini tazameni mlichofanya! Mmeujaza mji wa Yerusalemu kwa mafundisho yenu. Na mnajaribu kutulaumu sisi kwa sababu ya kifo chake.”
29 Petro na mitume wengine wakajibu, “Ni lazima tumtii Mungu, siyo wanadamu! 30 Mlimwua Yesu kwa kumpigilia msalabani. Lakini Mungu, Mungu yule yule wa Baba zetu, alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. 31 Yesu ndiye ambaye Mungu amemtukuza kwa kumpa nafasi upande wake wa kuume. Amemfanya kuwa Kiongozi na Mwokozi wetu. Mungu alifanya hivi ili kuwapa watu wote wa Israeli fursa ya kubadilika na kumgeukia Mungu ili dhambi zao zisamehewe. 32 Tuliona mambo haya yote yakitokea, na tunathibitisha kuwa ni ya kweli. Pia, Roho Mtakatifu anaonesha kuwa mambo haya ni ya kweli. Mungu amemtoa Roho huyu kwa ajili ya wote wanaomtii Yeye.”
33 Wajumbe wa Baraza waliposikia haya, walikasirika sana. Walianza kupanga namna ya kuwaua mitume. 34 Lakini mjumbe mmoja wa Baraza, Farisayo aliyeitwa Gamalieli, akasimama, alikuwa mwalimu wa sheria na watu wote walimheshimu. Aliwaambia wajumbe wawatoe nje mitume kwa dakika chache. 35 Kisha akawaambia, “Wanaume wa Israeli, iweni waangalifu kwa kile mnachopanga kuwatendea watu hawa. 36 Mnakumbuka Theuda alipotokea? Alijidai kuwa alikuwa mtu mkuu, na wanaume kama mia nne waliungana naye. Lakini aliuawa na wote waliomfuata walitawanyika. 37 Baadaye, wakati wa sensa, mtu mmoja aitwaye Yuda alikuja kutoka Galilaya. Watu wengi walijiunga kwenye kundi lake, lakini yeye pia aliuawa na wafuasi wake wote walitawanyika. 38 Na sasa ninawaambia, kaeni mbali na watu hawa. Waacheni. Ikiwa mpango wao ni kitu walichopanga wao wenyewe, utashindwa. 39 Lakini ikiwa ni mpango wa Mungu, hamtaweza kuwazuia. Mnaweza kuwa mnapigana kinyume na Mungu mwenyewe!”
Viongozi wa Kiyahudi wakakubaliana na kile alichosema Gamalieli. 40 Wakawaita mitume ndani tena. Wakawachapa viboko na kuwakanya waache kusema na watu kwa kutumia jina la Yesu. Kisha wakawaachia huru. 41 Mitume waliondoka kwenye mkutano wa Baraza, wakifurahi kwamba wamepewa heshima ya kudharauliwa kwa ajili ya Yesu. 42 Mitume hawakuacha kuwafundisha watu. Waliendelea kuzisema Habari Njema, kwamba Yesu ni Masihi. Walifanya hivi kila siku katika eneo la Hekalu na katika nyumba za watu.
© 2017 Bible League International