Old/New Testament
Petro na Yohana Warudi kwa Waamini
23 Petro na Yohana waliondoka kwenye mkutano wa viongozi wa Kiyahudi na kurudi kwa waamini wenzao. Wakalieleza kundi la waamini kila kitu walichoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 24 Waamini waliposikia hili, wote kwa pamoja wakamwomba Mungu wakiwa na nia moja. Wakasema, “Bwana wa wote, wewe ndiye uliyeumba mbingu, dunia, bahari na kila kitu ulimwenguni. 25 Baba yetu Daudi alikuwa mtumishi wako. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliandika maneno haya:
‘Kwa nini mataifa yanatenda kwa kiburi?
Kwa nini watu wanapanga mipango isiyofaa kama hii?
26 Wafalme wa dunia hujiandaa kwa mapigano,
na watawala hukusanyika pamoja kinyume na Bwana
na kinyume na Masihi wake.’(A)
27 Ndicho hasa kilichotokea wakati Herode, Pontio Pilato, mataifa mengine na watu wa Israeli walipokusanyika pamoja hapa Yerusalemu wakawa kinyume na Yesu; Masihi, Mtumishi wako mtakatifu. 28 Watu hawa waliokusanyika pamoja kinyume na Yesu waliwezesha mpango wako kukamilika. Ilifanyika kwa sababu ya nguvu zako na matakwa yako. 29 Na sasa, Bwana, sikiliza wanayosema. Wanajaribu kututisha. Sisi ni watumishi wako. Tusaidie ili tuseme yale unayotaka tuseme bila kuogopa. 30 Tusaidie, ili tuwe jasiri kwa kutuonesha nguvu zako. Ponya Wagonjwa. Fanya ishara na maajabu kutokea kwa mamlaka[a] ya Yesu mtumishi wako mtakatifu.”
31 Baada ya waamini kuomba, mahali walipokuwa palitikisika. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, na wakaendelea kuhubiri Habari Njema bila woga.
Ushirika wa Waamini
32 Kundi lote la waamini waliungana katika kuwaza na katika mahitaji yao. Hakuna aliyesema vitu alivyokuwa navyo ni vyake peke yake. Badala yake walishirikiana kila kitu. 33 Kwa nguvu kuu mitume walifanya ijulikane kwa kila mmoja kwamba Bwana Yesu alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na Mungu aliwabariki sana waamini wote. 34 Hakuna aliyepungukiwa kitu. Kila aliyemiliki shamba au nyumba aliuza na kuleta pesa alizopata, 35 na kuzikabidhi kwa mitume. Kisha kila mtu akapewa kiasi alichohitaji.
36 Mmoja wa waamini aliitwa Yusufu. Mitume walimwita Barnaba, jina linalomaanisha “Mtu anayewatia moyo wengine.” Alikuwa Mlawi mzaliwa wa Kipro. 37 Yusufu aliuza shamba alilomiliki. Akaleta pesa na kuwapa mitume.
© 2017 Bible League International