Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 12:22-50

Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu

(Mk 3:20-30; Lk 11:14-23; 12:10)

22 Kisha baadhi ya watu wakamleta mtu kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa asiyeona na hakuweza kuzungumza, kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. Yesu akamponya na akaweza kuzungumza na kuona. 23 Watu wote walikishangaa kile Yesu alichotenda. Walisema, “Pengine ni Mwana wa ahadi wa Daudi!”

24 Mafarisayo waliposikia hili, walisema, “Mtu huyu anatumia nguvu za Shetani[a] kufukuza mashetani kutoka kwa watu. Beelzebuli ni mtawala wa mashetani.”

25 Yesu alijua kile Mafarisayo walikuwa wanafikiri. Hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe utateketezwa. Na kila mji au familia iliyogawanyika haiwezi kuishi. 26 Hivyo ikiwa Shetani anayafukuza mashetani[b] yake mwenyewe, anapigana kinyume chake yeye mwenyewe, na ufalme wake hautaishi. 27 Mnasema kuwa ninatumia nguvu za Shetani kuyatoa mashetani. Ikiwa hiyo ni kweli, sasa ni nguvu gani watu wenu hutumia wanapoyafukuza mashetani? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa mmekosea. 28 Lakini ninatumia nguvu ya Roho wa Mungu kuyafukuza mashetani, na hili linaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu. 29 Watu wowote wanaotaka kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuiba vitu vyake lazima wamfunge kwanza. Kisha wanaweza kuiba vitu kutoka katika nyumba yake. 30 Yeyote ambaye hayuko pamoja nami yu kinyume nami. Na yeyote ambaye hakusanyi pamoja nami hutawanya.

31 Hivyo ninawaambia, Mungu atawasamehe watu kila dhambi wanayotenda au kila jambo baya wanalosema kinyume naye. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32 Unaweza kusema kinyume na Mwana wa Adamu na ukasamehewa. Lakini yeyote anayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa; si sasa au baadaye.

Yale Unayofanya Yanaonesha Jinsi Ulivyo

(Lk 6:43-45)

33 Ikiwa unataka matunda mazuri, ni lazima uutunze mti vizuri. Ikiwa mti wako siyo mzuri, utakuwa na matunda mabaya. Mti unajulikana kutokana na aina ya matunda inaozalisha. 34 Ninyi nyoka! Ni waovu sana. Mnawezaje mkasema chochote kilicho chema? Kile ambacho watu husema kwa midomo yao kinatoka katika yale yaliyojaa katika mioyo yao. 35 Walio wema wana vitu vizuri vilivyotunzwa katika mioyo yao. Ndiyo maana husema mambo mazuri. Lakini wale walio waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu husema mambo maovu. 36 Ninawaambia kuwa kila mmoja atajibu kwa ajili ya mambo yasiyo ya maana waliyosema. Hili litatokea siku ya hukumu. 37 Maneno yenu yatatumika kuwahukumu ninyi. Uliyosema yataamua ikiwa una haki mbele za Mungu au unahukumiwa na Mungu.”

Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu

(Mk 8:11-12; Lk 11:29-32)

38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjibu Yesu. Wakasema, “Mwalimu, tunataka kukuona ukifanya miujiza kama ishara kuwa unatoka kwa Mungu.”

39 Yesu akajibu, “Watu wenye dhambi na wasio na imani hutafuta kuona muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika kudhibitisha chochote kwao. Yona[c] ni ishara pekee itakayotolewa kwenu ninyi mlio wa kizazi kiovu cha leo. 40 Yona alikuwa ndani ya tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu, mchana na usiku. Vivyo hivyo, Mwana wa Adamu atakuwa kaburini kwa siku tatu, mchana na usiku. 41 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi leo mtalinganishwa na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha namna mlivyokosea. Kwa nini ninasema hivi? Kwa sababu Yona alipowahubiri watu hao, walibadili maisha yao. Na aliye mkuu kuliko Yona, yupo hapa lakini mnakataa kubadilika!

42 Pia, siku ya hukumu, Malkia wa Kusini[d] atasimama pamoja na wale wanaoishi sasa, atasababisha mhukumiwe kuwa na makosa. Ninasema hivi kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana kuja kusikiliza mafundisho yenye hekima ya Sulemani. Nami Ninawaambia aliye mkuu zaidi ya Sulemani yuko hapa, lakini hamnisikii!

Hatari ya Kuwa Mtupu

(Lk 11:24-26)

43 Roho chafu inapotoka kwa mtu, husafiri katika sehemu kavu ikitafuta mahali pa kupumzika, lakini haipati mahali pa kupumzika. 44 Inapokosa mahali pa kupumzika, husema, ‘Nitarudi katika nyumba niliyotoka.’ Inaporudi, ikakuta nyumba hiyo bado ni tupu, ikiwa safi na nadhifu, 45 hutoka nje na kuleta roho zingine saba zilizo chafu zaidi yake. Huingia na kuishi humo, na mtu huyo anakuwa na matatizo mengi kuliko mwanzo wakati roho chafu moja iliishi ndani yake. Ndivyo ilivyo kwa kizazi hiki cha watu wanaoishi leo.”

Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi

(Mk 3:31-35; Lk 8:19-21)

46 Yesu alipokuwa akiongea na watu, mama yake na ndugu zake walikuwa nje. Walitaka kuongea naye. 47 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na wadogo zako wanakusubiri nje. Wanataka kuongea nawe.”

48 Yesu akajibu, “Mama yangu ni nani? Ndugu zangu ni nani?” 49 Kisha akanyoosha kidole kwa wafuasi wake na akasema, “Unaona! Watu hawa ni mama yangu na ndugu zangu. 50 Kaka yangu, dada yangu na mama yangu halisi ni yule afanyaye yale Baba yangu wa mbinguni anataka.”

Luka 11

Yesu Afundisha Kuhusu Maombi

(Mt 6:9-15)

11 Siku moja Yesu alitoka akaenda mahali fulani kuomba. Alipomaliza, mmoja wa wafuasi wake akamwambia, “Yohana aliwafundisha wafuasi wake namna ya kuomba. Bwana, tufundishe nasi pia.”

Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivi ndivyo mnapaswa kuomba:

‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe daima.
    Tunaomba Ufalme wako uje.
Utupe chakula tunachohitaji kila siku.
Utusamehe dhambi zetu,
    kama tunavyomsamehe kila mtu anayetukosea.
Na usiruhusu tukajaribiwa.’”

Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji

(Mt 7:7-11)

5-6 Kisha Yesu akawaambia, “Chukulia mmoja wenu angekwenda kwa rafiki yake usiku na kumwambia, ‘Rafiki yangu aliyekuja mjini amekuja kunitembelea. Lakini sina chakula cha kumpa ili ale. Tafadhali nipe mikate mitatu.’ Rafiki yako ndani ya nyumba akajibu, ‘Nenda zako! Usinisumbue! Mlango umefungwa. Mimi na watoto wangu tumeshapanda kitandani kulala. Siwezi kuamka ili nikupe kitu chochote kwa sasa.’ Ninawaambia, urafiki unaweza usimfanye aamke akupe kitu chochote. Lakini hakika ataamka ili akupe unachohitaji ikiwa utaendelea kumwomba. Hivyo ninawaambia, Endeleeni kuomba na Mungu atawapa. Endeleeni kutafuta na mtapata. Endeleeni kubisha milangoni, na milango itafunguliwa kwa ajili yenu. 10 Ndiyo, kila atakayeendelea kuomba atapokea. Kila atakayeendelea kutafuta atapata. Na kila atakayeendelea kubisha mlangoni, mlango utafunguliwa kwa ajili yake. 11 Je, kuna mmoja wenu aliye na mwana? Utafanya nini ikiwa mwanao atakuomba samaki? Je, kuna baba yeyote anayeweza kumpa nyoka? 12 Au akiomba yai, utampa nge? Hakika hakuna baba wa namna hivyo. 13 Ikiwa ninyi waovu mnajua namna ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Vivyo hivo, hakika Baba yenu aliye mbinguni anajua namna ya kuwapa Roho Mtakatifu wale wanao mwomba?”

Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu

(Mt 12:22-30; Mk 3:20-27)

14 Wakati mmoja Yesu alikuwa akitoa pepo aliyemfanya mtu ashindwe kuzungumza. Ikawa, pepo alipotoka, yule mtu akaanza kuongea, umati wa watu walishangaa. 15 Lakini baadhi ya watu walisema, “Anatumia nguvu za Shetani kuwatoa pepo. Shetani[a] ni mtawala wa pepo wachafu.”

16 Baadhi ya watu wengine waliokuwa pale walitaka kumjaribu Yesu, walimwomba afanye muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. 17 Lakini alijua walichokuwa wanafikiria, hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe huteketezwa; na familia yenye magomvi husambaratika. 18 Hivyo, ikiwa Shetani anapigana yeye mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Ninawauliza hivi kwa kuwa mnasema kwamba ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani. 19 Lakini ikiwa ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani, watu wenu wanatumia nguvu gani wanapotoa pepo? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa ninyi ni waovu. 20 Lakini, ninatumia nguvu za Mungu kutoa pepo. Hii inaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu sasa.

21 Mwenye nguvu aliye na silaha nyingi anapoilinda nyumba yake, vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake huwa salama. 22 Lakini chukulia kuwa mwenye nguvu zaidi kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yule mwenye nguvu zaidi humnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea kuilinda nyumba yake. Ndipo mwenye nguvu zaidi atavitumia vitu vya yule mtu wa kwanza kadri anavyotaka.

23 Mtu yeyote asiye pamoja nami, yuko kinyume nami. Na mtu yeyote asiyefanya kazi pamoja nami anafanya kinyume nami.

Hatari ya Kuwa Mtupu

(Mt 12:43-45)

24 Mtu anapotokwa na roho chafu, roho hiyo husafiri sehemu zilizo kavu, ikitafuta mahali ili ipumzike. Lakini hukosa mahali pa kupumzika. Hivyo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba nilikotoka.’ 25 Inaporudi hukuta nyumba imesafishwa na kupangwa vizuri. 26 Ndipo roho hiyo chafu huenda ikachukua roho wengine saba, walio waovu kuliko yenyewe. Na kwa pamoja roho zote hizo huingia na kuishi ndani ya mtu huyo, na mtu huyo hupata matatizo mengi kuliko ya kwanza.”

Watu Wanaobarikiwa na Mungu

27 Yesu alipokuwa akisema mambo haya, mwanamke mmoja katika kundi la watu akapaza sauti akamwambia “Amebarikiwa na Mungu mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!”

28 Lakini Yesu akasema, “Wamebarikiwa zaidi wanaosikia na kuyatii mafundisho ya Mungu.”

Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu

(Mt 12:38-42; Mk 8:12)

29 Baada ya kundi la watu kuongezeka na kumzunguka, Yesu alisema, “Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu. Mnaomba muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia jambo lolote. Ishara pekee mtakayopata ni kile kilichompata Yona.[b] 30 Yona alikuwa ishara kwa watu walioishi katika mji wa Ninawi. Ni sawasawa na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa watu wa wakati huu.

31 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa, mtalinganishwa na Malkia wa Kusini,[c] naye pia, atakuwa shahidi atakayeonyesha namna mlivyo waovu. Kwa nini ninasema haya? Kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana ili ayasikilize mafundisho yenye hekima ya Suleimani. Na ninawaambia mkuu[d] kuliko Suleimani yupo hapa, lakini hamnisikilizi!

32 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa mtafananishwa pia na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha makosa yenu. Ninasema hivi kwa sababu Yona alipowahubiri, walibadili mioyo na maisha yao. Na sasa mnamsikia mtu aliye mkuu kuliko Yona, Lakini hamtaki kubadilika!

Iweni Mwanga kwa Ajili ya Ulimwengu

(Mt 5:15; 6:22-23)

33 Hakuna mtu anayechukua taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunika. Badala yake huiweka mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani waweze kuiona nuru yake. 34 Namna unavyowatazama watu inaonesha kwa hakika jinsi ulivyo. Unapowatazama watu katika hali isiyo ya ubinafsi, inaonesha wazi kuwa umejaa nuru. Lakini unapowatazama watu katika namna ya uchoyo, ni wazi kuwa umejaa giza.[e] 35 Hivyo iweni waangalifu ili nuru iliyo ndani yenu usiwe giza! 36 Ikiwa umejaa nuru na hakuna sehemu yenye giza ndani yako, basi utang'aa, kama nuru ya kwenye taa.”

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 20:45-47)

37 Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. 38 Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa[f] mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. 39 Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. 40 Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. 41 Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu.

42 Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani[g] zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine.

43 Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. 44 Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.”

45 Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.”

46 Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii.[h] Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. 47 Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. 48 Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! 49 Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume[i] kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’

50 Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. 51 Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria,[j] aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote.

52 Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.”

53 Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, 54 ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International