Chronological
Watu Wamsifu Mungu Mbinguni
19 Baada ya hili nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu mbinguni. Walikuwa wakisema:
“Haleluya![a]
Ushindi, utukufu na nguvu ni vyake Mungu wetu.
2 Hukumu zake ni za kweli na za haki.
Mungu wetu amemwadhibu kahaba.
Ndiye aliyeiharibu dunia kwa uzinzi wake.
Mungu amemwadhibu kahaba kulipa kisasi cha vifo vya watumishi wake.”
3 Pia, watu hawa walisema:
“Haleluya!
Anaungua na moshi wake utasimama milele na milele.”
4 Ndipo wazee ishirini na nne na viumbe wenye uhai wanne wakaanguka chini kusujudu wakamwabudu Mungu, akaaye kwenye kiti cha enzi. Wakasema:
“Amina! Haleluya!”
5 Sauti ikatoka kwenye kiti cha enzi na kusema:
“Msifuni Mungu wetu,
ninyi nyote mnaomtumikia!
Msifuni Mungu wetu,
ninyi nyote mlio wadogo na wakubwa mnaomheshimu!”
6 Kisha nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu. Kilikuwa na kelele kama mawimbi ya bahari au radi. Watu walikuwa wakisema:
“Haleluya!
Bwana Mungu wetu anatawala.
Ndiye Mwenye Nguvu, Mungu Mwenyezi.
7 Tushangilie na kufurahi na
kumpa Mungu utukufu!
Mpeni Mungu utukufu, kwa sababu arusi ya Mwanakondoo imewadia.
Na bibi arusi wa Mwanakondoo amekwisha jiandaa.
8 Nguo ya kitani safi ilitolewa kwa bibi arusi ili avae.
Kitani ilikuwa safi na angavu.”
(Kitani safi inamaanisha mambo mazuri ambayo watakatifu wa Mungu waliyatenda.)
9 Kisha malaika akaniambia, “Andika hili: Heri ni kwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!” Kisha malaika akasema, “Haya ni maneno ya Mungu mwenyewe.”
10 Kisha nikaanguka chini mbele miguuni pa malaika ili nimwabudu. Lakini malaika akaniambia, “Usiniabudu! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako na dada zako walio na ushuhuda kuhusu Yesu Kristo. Hivyo mwabudu Mungu! Kwa sababu ushuhuda kuhusu Yesu ndiyo roho ya unabii.”
Mpanda Farasi Juu ya Farasi Mweupe
11 Kisha nikaona mbingu zimefunguka, na nikamwona farasi mweupe. Mpanda farasi aliitwa Mwaminifu na Kweli, kwa sababu ni wa haki katika maamuzi yake na kufanya vita. 12 Macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. Alikuwa na taji nyingi kichwani mwake. Jina lilikuwa limeandikwa juu yake, lakini yeye peke yake ndiye aliyejua maana ya jina hilo. 13 Alivaa vazi lililochovywa katika damu, na aliitwa Neno la Mungu. 14 Majeshi ya mbinguni yalikuwa yanamfuata mpanda farasi mweupe. Walikuwa wanaendesha farasi weupe pia. Walikuwa wamevaa kitani nzuri, nyeupe na safi. 15 Upanga mkali ulikuwa unatoka kwenye kinywa chake, upanga ambao angeutumia kuyashinda mataifa. Na atayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Atazikanyaga zabibu katika shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenye Nguvu. 16 Kwenye vazi lake na kwenye mguu wake alikuwa ameandikwa jina lake:
mfalme wa wafalme na bwana wa mabwana.
17 Kisha nikaona malaika amesimama katika jua. Kwa sauti kuu malaika akawaambia ndege wote wanaoruka angani, “Kusanyikeni kwa ajili ya karamu kuu ya Mungu. 18 Kusanyikeni mle miili ya watawala, majemadari na watu maarufu. Njooni mle miili ya farasi na wanaowapanda na miili ya watu wote, walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”
19 Kisha nikamwona mnyama na watawala wa dunia. Majeshi yao yalikusanyika pamoja ili kufanya vita kupigana na mpanda farasi mweupe na jeshi lake. 20 Lakini mnyama na nabii wa uongo walikamatwa. Nabii wa uongo ndiye aliyefanya miujiza[b] kwa ajili ya mnyama. Alitumia miujiza hii kuwahadaa wale waliokuwa na alama ya mnyama na walioabudu sanamu yake. Nabii wa uongo na mnyama walitupwa kwenye ziwa la moto linalowaka kwa baruti. 21 Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kwenye kinywa cha mpanda farasi. Ndege wote walikula miili hii mpaka wakashiba.
Miaka Elfu Moja
20 Nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni. Malaika alikuwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. 2 Malaika alimkamata joka, nyoka wa zamani ambaye pia anajulikana kama Ibilisi au Shetani. Malaika akamfunga joka kwa minyororo kwa muda wa miaka elfu moja. 3 Kisha akamtupia kuzimu na akaifunga. Malaika akamfungia joka kuzimu ili asiweze kuwadanganya watu wa dunia mpaka miaka elfu moja iishe. Baada ya miaka elfu moja joka lazima aachiwe huru kwa muda mfupi.
4 Kisha nikaona viti vya enzi na watu wamevikalia. Hawa ni wale waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Na nikaona roho za wale waliouawa kwa sababu walikuwa waaminifu kwa kweli ya Yesu na ujumbe kutoka kwa Mungu. Hawakumwabudu mnyama wala sanamu yake. Hawakuipokea alama ya mnyama kwenye vipaji vya nyuso zao au mkononi mwao. Walifufuka na kutawala na Kristo kwa miaka elfu moja. 5 (Wengine waliokufa hawakufufuka mpaka miaka elfu moja ilipokwisha.)
Huu ni ufufuo wa kwanza. 6 Heri walifufuliwa mara ya kwanza. Ni watakatifu wa Mungu. Mauti ya pili haina nguvu juu yao. Watakuwa makuhani wa Mungu na Kristo. Watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.
Kushindwa kwa Shetani
7 Miaka elfu moja itakapokwisha, Shetani ataachiwa huru kutoka kwenye gereza lake. 8 Atatoka na kwenda kuwadanganya mataifa katika dunia yote, mataifa yajulikanayo kama Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya watu kwa ajili ya vita. Kutakuwa watu wengi wasiohesabika kama mchanga katika ufukwe wa bahari.
9 Nililiona jeshi la Shetani likitembea na kujikusanya ili kuizingira kambi ya watu wa Mungu na mji anaoupenda Mungu. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuliteketeza jeshi la Shetani. 10 Na Shetani, yule aliyewadanganya watu hawa, alitupwa kwenye ziwa la moto pamoja na mnyama na nabii wa uongo. Watateseka kwa maumivu usiku na mchana milele na milele.
Watu wa Dunia Wahukumiwa
11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe. Nikamwona aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha enzi. Dunia na anga vikamkimbia na kutoweka. 12 Na nikaona wale waliokufa, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi na vitabu vilifunguliwa. Na kitabu cha uzima kilifunguliwa pia. Watu walihukumiwa kwa yale waliyotenda, kama yalivyoandikwa katika vitabu.
13 Bahari ikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Mauti na kuzimu zikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Watu wote hawa walihukumiwa kutokana na matendo yao. 14 Mauti na kuzimu vilitupwa kwenye ziwa la moto. Ziwa hili la moto ni mauti ya pili. 15 Na yeyote ambaye jina lake halikuonekana limeandikwa kwenye kitabu cha uzima alitupwa kwenye ziwa la moto.
Yerusalemu Mpya
21 Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu na dunia ya kwanza vilikwisha kutoweka. Na sasa bahari haikuwepo. 2 Nikauona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya,[c] ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyevalishwa kwa ajili ya mumewe.
3 Nikasikia sauti kuu kutoka kwenye kiti cha enzi. Ikisema, “Makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Yeye ataishi pamoja nao. Na wao watakuwa watu wake. Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao naye atakuwa Mungu wao. 4 Atafuta kila chozi kutoka machoni mwaona. Hakutakuwa na kifo tena, huzuni, kilio wala maumivu. Namna zote za zamani zimepita.”
5 Aliyekaa kwenye kiti cha enzi akasema, “Tazama, sasa ninakiumba kila kitu upya!” Kisha akasema, “Andika hili, kwa sababu maneno haya ni kweli na ya kuaminiwa.”
6 Akaniambia, “Imekwisha! Mimi ni Alfa na Omega,[d] Mwanzo na Mwisho. Kila mwenye kiu nitampa bure maji kutoka kwenye chemichemi ya maji ya uzima. 7 Wale wote watakaoshinda watapokea yote haya. Na nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watoto wangu. 8 Lakini waoga, wanaokataa kuniamini, wafanyao mambo ya kuchukiza, wauaji, wazinzi, wachawi, waabuduo sanamu na waongo, nitawatupa katika ziwa linalowaka moto. Hii ni mauti ya pili.”
9 Mmoja wa malaika saba akaja kwangu. Huyu alikuwa mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli saba zilizojaa mapigo saba ya mwisho. Malaika akasema, “Njoo huku. Nitakuonesha bibi arusi, mke wa Mwanakondoo.” 10 Malaika akanichukua kwa Roho Mtakatifu mpaka kwenye mlima mkubwa na mrefu. Akanionyesha mji mtakatifu wa Yerusalemu. Mji ulikuwa ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu.
11 Mji ulikuwa unang'aa kwa utukufu wa Mungu. Ulikuwa unang'aa kwa uangavu kama yaspi, kito cha thamani sana. Ulionekana kwa uwazi kama kioo. 12 Mji ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mbili. Kulikuwa malaika kumi na mbili kwenye milango. Kwenye kila mlango kuliandikwa jina la kabila moja la Israeli. 13 Yalikuwepo malango matatu upande wa mashariki, malango matatu kaskazini, malango matatu kusini, na malango matatu magharibi. 14 Kuta za mji zilijengwa kwenye mawe kumi na mbili ya msingi. Kwenye mawe kulikuwa kumeandikwa majina ya mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.
15 Malaika aliyezungumza na mimi alikuwa na fimbo ya kupimia iliyotengenezwa kwa dhahabu. Alikuwa na fimbo hii ili kuupima mji, malango na ukuta wake. 16 Mji ulijengwa kimraba. Urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Malaika aliupima mji kwa fimbo. Mji ulikuwa na urefu wa kilomita 2,400,[e] upana wake ulikuwa kilomita 2,400, na kimo chake kwenda juu kilikuwa kilomita 2,400. 17 Malaika akaupima ukuta pia. Kimo cha ukuta kilikuwa ni mita 60[f] kwenda juu. (Malaika alikuwa anatumia vipimo ambavyo watu hutumia.) 18 Ukuta ulijengwa kwa yaspi. Mji ulijengwa kwa dhahabu safi, iliyo safi kama kioo.
19 Mawe ya msingi wa ukuta wa mji yalikuwa na kila aina ya vito vya thamani ndani yake. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedoni, la nne lilikuwa zumaridi, 20 la tano lilikuwa sardoniki, la sita lilikuwa akiki, la saba lilikuwa krisolitho, la nane lilikuwa zabarajadi, la tisa lilikuwa yakuti ya manjano, la kumi lilikuwa krisopraso, la kumi na moja lilikuwa hiakintho na la kumi na mbili lilikuwa amethisto. 21 Malango kumi na mbili yalikuwa lulu kumi na mbili. Kila lango lilitengenezwa kwa lulu moja. Mitaa ya mji ilitengenezwa kwa dhahabu safi, inayong'aa kama kioo.
22 Sikuona hekalu ndani ya mji. Bwana Mungu Mwenye Nguvu na Mwanakondoo ndiyo waliokuwa hekalu la mji. 23 Mji haukuhitaji jua wala mwezi kuung'arizia. Utukufu wa Mungu uliupa mji mwanga. Mwanakondoo ndiye alikuwa taa ya mji.
24 Mataifa watatembea katika mwanga unaotoka katika mji ule.[g] Watawala wa dunia wataleta utukufu wao katika mji. 25 Milango ya mji haitafungwa hata siku moja, kwa sababu hakutakuwa usiku huko. 26 Ukuu na heshima ya mataifa vitaletwa katika mji. 27 Kilicho najisi hakitaingia katika mji. Atendaye mambo ya kuchukiza na mwongo hawataingia katika mji huo. Walioandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tu, ndiyo watakaoingia katika mji huo.
22 Malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, ulikuwa anga'avu kama kioo. Mto hutiririka kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. 2 Hutiririka kupitia katika mtaa mkuu wa mji. Mti wa uzima[h] uko kila upande wa mto, na huzaa tunda kila mwezi, mara kumi na mbili kwa mwaka. Majani ya mti ni kwa ajili ya kutibu mataifa.
3 Katika mji ule hakuna mtu au kitu kitakachokuwa chini ya laana ya Mungu tena. Kiti cha ufalme cha Mungu na Mwanakondoo vitakuwa ndani ya mji. Watumishi wa Mungu watamwabudu yeye. 4 Watauona uso wake. Jina la Mungu litaandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Hakutakuwa usiku tena. Watu hawatahitaji mwanga wa taa au mwanga wa jua. Bwana Mungu atawapa mwanga. Watatawala kama wafalme milele na milele.
6 Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminiwa. Bwana, Mungu awavuviaye manabii, amemtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake mambo ambayo lazima yatokee hivi karibuni: 7 ‘Sikiliza, Naja upesi! Heri anayetii maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.’”
8 Mimi ni Yohana. Mimi ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Baada ya kuyasikia na kuyaona, niliinama chini kusujudu miguuni pa malaika aliyeyaonesha kwangu. 9 Lakini malaika aliniambia, “Usinisujudie mimi! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako manabii, ni mtumishi kama wale wote wanaoyatii maneno yaliyo katika kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
10 Kisha malaika akaniambia, “Usiyafanye siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, wakati umekaribia kwa mambo haya kutokea. 11 Kila atendaye mabaya aendelee kutenda mabaya. Yeyote aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Atendaye mema aendelee kutenda mema. Aliye mtakatifu aendelee kuwa mtakatifu.”
12 “Sikiliza, nakuja upesi! Nakuja na ujira ili kumlipa kila mtu sawa sawa na matendo yake. 13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 Heri walioosha kanzu zao.[i] Watakuwa na haki ya kula chakula kutoka kwenye mti wa uzima. Wanaweza kuingia katika mji kwa kupitia katika malango yake. 15 Nje ya mji ni kwa ajili wale waishio kama mbwa; wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wapendao kudanganya na kujifanya wema.
16 Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kukuambia mambo hayo kwa ajili ya makanisa. Mimi ni mzao wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi.”
17 Roho Mtakatifu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Kila asikiaye hili aseme pia, “Njoo!” Wote wenye kiu waje wanywe maji ya uzima bure ikiwa wanataka.
18 Ninamwonya kila mtu anayesikia maneno ya unabii wa kitabu hiki: Ikiwa mtu yeyote ataongeza chochote kwa haya, Mungu atampa mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 Na ikiwa mtu yeyote akitoa sehemu yoyote ya maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu ya urithi wa mtu huyo katika mti wa uzima na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yesu ndiye anayesema kwamba haya yote ni kweli. Sasa anasema, “Ndiyo, naja upesi.”
Amina! Njoo, Bwana Yesu!
21 Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja na watu wote.
© 2017 Bible League International