Chronological
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu Mungu mwenyewe alitaka.
Kwa watakatifu wa Mungu walioko katika mji wa Efeso,[b] waamini walio wa Kristo Yesu.
2 Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.
Baraka za Rohoni katika Kristo
3 Sifa kwake Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Kristo, Mungu ametupa baraka zote za rohoni zilizoko mbinguni. 4 Kwa kuwa anatupenda alituchagua katika Kristo kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu wake, tusio na hatia tunaoweza kusimama mbele zake. 5 Aliamua tangu mwanzo kutufanya kuwa watoto wake kupitia Yesu Kristo. Hivi ndivyo Mungu alivyotaka na ilimpendeza yeye kufanya hivyo. 6 Sifa kwake Mungu kwa sababu ya neema yake ya ajabu aliyotupa bure kupitia Kristo anayempenda.
7 Tumewekwa huru katika Kristo kupitia sadaka ya damu yake. Tumesamehewa dhambi kwa sababu ya wingi na ukuu wa neema ya Mungu. 8 Mungu alitupa bure neema hiyo yote, pamoja na hekima na uelewa wote, 9 na ametuwezesha kuujua mpango wake wa siri. Hivi ndivyo Mungu alitaka, na alipanga kuutekeleza kupitia Kristo. 10 Lengo la Mungu lilikuwa kuukamilisha mpango wake muda sahihi utakapofika. Alipanga kuwa vitu vyote vilivyoko mbinguni na duniani viunganishwe pamoja na Kristo kama kichwa.
11 Tulichaguliwa katika Kristo ili tuwe milki ya Mungu. Mungu alikwisha panga ili tuwe watu wake, kwa sababu ndivyo alivyotaka. Na ndiye ambaye hufanya kila kitu kifanyike kulingana na utashi na maamuzi yake. 12 Sisi Wayahudi ndiyo tuliokuwa wa kwanza kutumaini katika Kristo. Na tulichaguliwa ili tuweze kumletea sifa Mungu katika utukufu wake wote. 13 Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Mliusikia ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema kuhusu namna ambavyo Mungu anavyowaokoa. Mlipoisikia Habari Njema hiyo, mkamwamini Kristo. Na katika Kristo, Mungu aliwatia alama maalum kwa kuwapa Roho Mtakatifu aliyeahidi. 14 Roho ni malipo ya kwanza yanayothibitisha kuwa Mungu atawapa watu wake kila kitu alichonacho kwa ajili yao. Sisi sote tutaufurahia uhuru kamili uliowekwa tayari kwa ajili ya walio wake. Na hili litamletea Mungu sifa katika utukufu wake wote.
Sala ya Paulo
15-16 Ndiyo sababu daima ninawakumbuka katika maombi yangu na ninamshukuru Mungu kwa ajili yenu. Nimekuwa nikifanya hivi tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watu wote wa Mungu. 17 Daima ninamwomba Baba aliye mkuu na mwenye utukufu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ninaomba awape Roho anakayewawezesha kuijua kweli kuhusu Mungu na awasaidie kuzielewa kweli hizo ili mweze kumjua vyema.
18 Ninaomba Mungu afungue mioyo yenu ili mwone kweli yake. Kisha mtalijua tumaini alilochagua kwa ajili yetu. Mtajua kuwa baraka ambazo Mungu amewaahidi watu wake ni nyingi na zimejaa utukufu. 19 Na mtajua kuwa uweza wa Mungu ni mkuu sana kwetu sisi tunaoamini. Ni sawa na nguvu zake kuu 20 alizotumia kumfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumweka akae upande wa kulia wa kiti chake cha enzi huko mbinguni. 21 Amemweka Kristo juu ya watawala wote, mamlaka zote, nguvu zote na wafalme wote. Amempa mamlaka juu ya kila kitu chenye nguvu katika ulimwengu huu na ujao. 22 Mungu alikiweka kila kitu chini ya nguvu za Kristo na kumfanya kuwa kichwa cha kila kitu kwa manufaa ya kanisa. 23 Kanisa ndiyo mwili wa Kristo, yeye ndiye amejaa ndani ya kanisa. Anakikamilisha kila kitu katika kila namna.
Kutoka Mauti hadi Uzima
2 Zamani mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi na mambo mliyotenda kinyume na Mungu. 2 Ndiyo, zamani maisha yenu yalijaa dhambi hizo. Mliishi kwa namna ya ulimwengu; mkimfuata mkuu wa nguvu za uovu[c] zilizo katika anga, roho hiyo hiyo inatenda kazi sasa ndani ya watu wasiomtii Mungu. 3 Tuliishi hivyo zamani, tukijaribu kuzifurahisha tamaa zetu za mwili. Tulitenda mambo ambayo miili na akili zetu zilitaka. Kama ilivyo kwa kila mtu ulimwenguni, tulistahili kuteseka kutokana na hasira ya Mungu kwa sababu ya jinsi tulivyokuwa.
4 Lakini Mungu ni mwingi wa rehema na anatupenda sana. 5 Tulikuwa wafu kiroho kwa sababu ya matendo maovu tuliyotenda kinyume naye. Lakini yeye alitupa maisha mapya pamoja na Kristo. (Mmeokolewa na neema ya Mungu.) 6 Ndiyo, ni kwa sababu sisi ni sehemu ya Kristo Yesu, ndiyo maana Mungu alitufufua pamoja naye kutoka kwa wafu na akatuketisha pamoja naye mbinguni. 7 Mungu alifanya hivi ili wema wake kwetu sisi tulio wa Kristo Yesu uweze kuonesha nyakati zote zijazo utajiri wa ajabu wa neema yake.
8 Nina maana ya kuwa mmeokolewa kwa neema kwa sababu mliweka imani yenu kwake.[d] Hamkujiokoa ninyi wenyewe; bali ni zawadi kutoka kwa Mungu. 9 Msijisifu kwa kuwa hamkuokolewa kutokana na matendo yenu. 10 Mungu ndiye aliyetufanya hivi tulivyo. Ametuumba wapya katika Kristo Yesu ili tutende mambo mema katika maisha yetu. Mambo aliyokwisha kutupangia.
Wamoja Katika Kristo
11 Hamkuzaliwa mkiwa Wayahudi. Ninyi ni watu ambao Wayahudi huwaita “Wasiotahiriwa”,[e] na wao wakijiita “Waliotahiriwa” (Tohara yao ni ile inayofanyika kwenye miili yao kwa mikono ya binadamu.) 12 Kumbukeni ya kwamba zamani hamkuwa na Kristo. Hamkuwa raia wa Israeli na hamkujua kuhusu mapatano ya maagano[f] ambayo Mungu aliyaweka kwa watu wake. Hamkuwa na tumaini na hamkumjua Mungu. 13 Lakini sasa mmeungana na Kristo Yesu. Ndiyo, wakati fulani hapo zamani mlikuwa mbali na Mungu, lakini sasa mmeletwa karibu naye kupitia sadaka ya damu ya Kristo.
14 Kristo ndiye sababu ya amani yetu. Yeye ndiye aliyetufanya sisi Wayahudi nanyi msio Wayahudi kuwa wamoja. Tulitenganishwa na ukuta wa chuki uliokuwa kati yetu, lakini Kristo aliubomoa. Kwa kuutoa mwili wake mwenyewe, 15 Kristo aliisitisha sheria pamoja na kanuni na amri zake nyingi. Kusudi lake lilikuwa ni kuyafanya makundi mawili yawe wanadamu wamoja waliounganishwa naye. Kwa kufanya hivi alikuwa analeta amani. 16 Kupitia msalaba Kristo alisitisha uhasama kati ya makundi mawili. Na baada ya makundi haya kuwa mwili mmoja, alitaka kuwapatanisha wote tena kwa Mungu. Alifanya hivi kwa kifo chake msalabani. 17 Kristo alikuja na kuwaletea ujumbe wa amani ninyi msio Wayahudi mliokuwa mbali na Mungu. Na aliwaletea pia ujumbe huo wa amani watu waliokaribu na Mungu. 18 Ndiyo, kupitia Kristo sisi sote tuna haki ya kumjia Baba katika Roho mmoja.
19 Hivyo ninyi msio Wayahudi si wageni wala wahamiaji, lakini ninyi ni raia pamoja na watakatifu wa Mungu. Ninyi ni wa familia ya Mungu. 20 Ninyi mnaoamini ni kama jengo linalomilikiwa na Mungu. Jengo hilo limejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii. Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la muhimu sana[g] katika jengo hilo. 21 Jengo lote limeunganishwa katika Kristo, naye hulikuza na kuwa hekalu[h] takatifu katika Bwana. 22 Na katika Kristo mnajengwa pamoja na watu wake wengine. Mnafanywa kuwa makazi ambapo Mungu anaishi katika Roho.
Huduma ya Paulo kwa Wasio Wayahudi
3 Hivyo, mimi Paulo ni mfungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi msio Wayahudi. 2 Mnajua hakika ya kuwa Mungu alinipa kazi hii kupitia neema yake ili niwasaidie. 3 Mungu alinionyesha na nikaweza kuujua mpango wake wa siri. Nimekwisha kuandika kiasi fulani juu ya hili. 4 Na ikiwa mtasoma nilichowaandikia, mtajua kuwa ninaielewa siri ya kweli kuhusu Kristo. 5 Watu walioishi zamani hawakuambiwa siri hiyo. Lakini sasa, kupitia Roho, Mungu amewawezesha mitume na manabii wake watakatifu kuijua siri hiyo. 6 Na siri hiyo ni hii: Kwa kuikubali Habari Njema, wale wasio Wayahudi watashiriki pamoja na Wayahudi katika baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake. Wao ni sehemu ya mwili mmoja, na wanashiriki manufaa ya ahadi ambayo Mungu aliitimiza kupitia Kristo Yesu.
7 Kwa kipawa cha neema ya Mungu, nilifanywa mtumishi wa kuihubiri Habari Njema. Alinipa neema hiyo kwa nguvu zake. 8 Mimi nisiye na umuhimu zaidi miongoni mwa watu wa Mungu. Lakini alinipa kipawa hiki cha kuwahubiri wasio Wayahudi Habari Njema kuhusu utajiri alionao Kristo. Utajiri huu ni mkuu na si rahisi kuuelewa kikamilifu. 9 Pia Mungu alinipa kazi ya kuwaambia watu kuhusu mpango wa siri yake ya kweli. Aliificha siri hii ya kweli ndani yake tangu mwanzo wa nyakati. Ndiye aliyeumba kila kitu. 10 Lengo lake lilikuwa kwamba watawala wote na mamlaka zote zilizo mbinguni zijue njia nyingi anazotumia kuionesha hekima yake. Watalijua hili kwa sababu ya kanisa. 11 Hii inaendana na mpango aliokuwa nao Mungu tangu mwanzo wa nyakati. Alitekeleza mpango wake kupitia Kristo Yesu Bwana wetu. 12 Kwa kuwa tu wake Kristo tunakuja mbele za Mungu tukiwa huru bila woga. Tunaweza kufanya hivi kwa sababu ya uaminifu wake Kristo.[i] 13 Hivyo ninawaomba msikate tamaa kutokana na yale yanayonipata. Mateso yangu ni faida kwenu, na pia ni kwa ajili ya heshima na utukufu wenu.
Upendo wa Kristo
14 Hivyo ninapiga magoti nikimwomba Baba. 15 Ambaye katika yeye kila familia iliyoko mbinguni na duniani inapewa jina. 16 Ninamwomba Baba kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake awajaze nguvu za ndani kwa nguvu za Roho wake. 17 Ninaomba kwamba Kristo aishi katika mioyo yenu kwa sababu ya imani yenu. Ninaomba maisha yenu yawe na mizizi mirefu na misingi imara katika upendo. 18 Na ninaomba ili ninyi na watakatifu wote wa Mungu muwe na uwezo wa kuuelewa upana, urefu, kimo na kina cha ukuu wa upendo wa Kristo. 19 Upendo wa Kristo ni mkuu kuliko namna ambavyo mtu yeyote anaweza kujua, lakini ninawaombea ili mweze kuujua. Ndipo mtajazwa kwa kila kitu alichonacho Mungu kwa ajili yenu.
20 Tukiwa na nguvu za Mungu zinazotenda kazi ndani yetu, anaweza kufanya zaidi, zaidi ya kila kitu tunachoweza kuomba au kufikiri. 21 Atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kila wakati, milele na milele. Amina.
Umoja wa Mwili wa Kristo
4 Hivyo, mimi niliye mfungwa kwa ajili ya Bwana nawasihi mwishi kwa jinsi inavyowapasa watu wa Mungu, kwa sababu aliwachagua muwe wake. 2 Iweni wanyenyekevu na wapole siku zote. Mvumiliane na kuchukuliana ninyi kwa ninyi katika upendo. 3 Mmeunganishwa pamoja kwa amani na Roho. Jitahidini mwezavyo kudumu kuutunza umoja huo, mkiunganishwa pamoja kwa amani. 4 Kuna mwili mmoja na Roho moja, na Mungu aliwachagua ili muwe na tumaini moja. 5 Kuna Bwana mmoja, imani moja, na ubatizo mmoja. 6 Mungu ni mmoja na ni Baba wetu sote, anayetawala juu ya kila mtu. Hutenda kazi kupitia kwetu sote na ndani yetu sote.
7 Kristo alimpa kila mmoja wetu karama. Kila mmoja alipokea kwa jinsi alivyopenda yeye kuwapa. 8 Ndiyo maana Maandiko yanasema,
“Alipaa kwenda mahali pa juu sana;
aliwachukua wafungwa pamoja naye,
na akawapa watu vipawa.”(A)
9 Inaposema, “Alipaa juu,” inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa kwanza alikuja chini duniani. 10 Hivyo Kristo alishuka chini, na ndiye aliyekwenda juu. Alikwenda juu ya mbingu za juu zaidi ili avijaze vitu vyote pamoja naye. 11 Na Kristo huyo huyo aliwapa watu hawa vipawa: aliwafanya wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kwenda na kuhubiri Habari Njema, na wengine kuwa wachungaji[j] ili wawafundishe watu wa Mungu. 12 Mungu aliwapa hao ili kuwaandaa watakatifu wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma, kuufanya imara mwili wa Kristo. 13 Kazi hii inabidi iendelee hadi wote tutakapounganishwa pamoja katika lile tunaloliamini na tunalolijua kuhusu Mwana wa Mungu. Lengo letu ni kufanana na mtu mzima aliyekomaa na kuwa kama Kristo tukiufikia ukamilifu wake wote.
14 Ndipo tutakapokuwa si kama watoto wachanga. Hatutakuwa watu ambao nyakati zote hubadilika kama meli inayochukuliwa na mawimbi huku na kule. Hatutaweza kuathiriwa na fundisho lolote jipya tutakalosikia kutoka kwa watu wanaojaribu kutudanganya. Hao ni wale wanaoweka mipango ya ujanja na kutumia kila aina ya mbinu kuwadanganya wengine waifuate njia iliyopotoka. 15 Hapana, tunapaswa kusema ukweli kwa upendo. Tutakua na kuwa kama Kristo katika kila njia. Yeye ni kichwa, 16 na mwili wote unamtegemea yeye. Viungo vyote vya mwili vimeunganishwa na kushikanishwa pamoja, huku kila kiungo kikitenda kazi yake. Hili huufanya mwili wote ukue na kujengeka katika upendo.
Mnavyopaswa Kuishi
17 Nina kitu cha kuwaambia kutoka kwa Bwana. Ninawaonya: Msiendelee kuishi kama wale wasiomwamini Mungu wetu. Mawazo yao hayafai kitu. 18 Hawana ufahamu, na hawajui lolote kwa sababu wamekataa kusikiliza. Hivyo hawawezi kupata maisha mapya Mungu anayowapa watu. 19 Wamepoteza hisia zao za aibu na wanayatumia maisha yao kutenda yale yaliyo mabaya kimaadili. Zaidi ya hapo wanataka kutenda kila aina ya uovu. 20 Lakini aina hiyo ya maisha haiko kama ile mliyojifunza mlipomjua Kristo. 21 Najua kwamba mlisikia juu yake, na ndani yake mlifundishwa ukweli. Ndiyo, ukweli umo ndani ya Yesu. 22 Mlifundishwa kuacha utu wenu wa kale. Hii inamaanisha kwamba mnapaswa kuacha kuishi katika njia za uovu mlivyoishi zamani. Utu wenu wa kale huharibika zaidi na zaidi, kwa sababu watu hudanganywa na uovu wanaotaka kuutenda. 23 Mnapaswa kufanywa upya katika mioyo yenu na katika fikra zenu. 24 Kila mmoja wenu auvae utu ule mpya ulioumbwa kwa kufananishwa na Mungu, ambao kwa hakika una wema na ni wenye kumpendeza Mungu.
25 Hivyo mnapaswa kuacha kusema uongo, “Nyakati zote mseme ukweli tu,”(B) kwa sababu wote sisi tunahusiana na ni wa mwili mmoja. 26 “Unapokasirika, usiruhusu hasira hiyo ikusababishe wewe kutenda dhambi,”(C) na usiendelee na hasira kwa siku nzima. 27 Usimwachie Ibilisi nafasi ya kukushinda. 28 Yeyote ambaye amekuwa akiiba anapaswa kuacha kuiba na afanye kazi. Unapaswa kutumia mikono yako kufanya kitu chenye kufaa. Hapo utakuwa na kitu cha kuwashirikisha walio maskini.
29 Unapozungumza, usiseme chochote kilicho kibaya. Bali useme mambo mazuri ambayo watu wanayahitaji ili waimarike. Ndipo kile unachosema kitakuwa ni baraka kwa wale wanaokusikia. 30 Tena usimhuzunishe Roho Mtakatifu. Mungu alikupa Roho Mtakatifu kama uthibitisho kwamba wewe ni wake na kwamba atakulinda hadi siku atakapokufanya uwe huru kabisa. 31 Usiwe na uchungu, wala kukasirika. Kamwe usiongee kwa hasira au kusema chochote ili uwaumize wengine. Usifanye chochote kilicho kiovu. 32 Mwe mwema na mpendane ninyi kwa ninyi. Msameheane ninyi kwa ninyi kama Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo.
5 Ninyi ni watoto wa Mungu wapendwao, hivyo jitahidini kuwa kama yeye. 2 Ishini maisha ya upendo. Wapendeni wengine kama Kristo alivyotupenda sisi. Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu na kuwa sadaka ya harufu ya manukato mazuri na dhabihu kwa Mungu.
3 Lakini hakupaswi kuwepo dhambi ya zinaa kati yenu. Hakupaswi kuwepo aina yoyote ya uasherati au matamanio ya zinaa, kwa sababu mambo kama hayo hayastahili kwa watakatifu wa Mungu. 4 Vivyo hivyo, pasiwepo na mazungumzo maovu miongoni mwenu. Msizungumze mambo ya kipuuzi au ya uchafu. Hayo siyo kwa ajili yenu. Bali mnatakiwa kutoa shukrani kwa Mungu. 5 Mnaweza kuwa na uhakika wa hili: Hakuna atakayepata sehemu katika ufalme wa Kristo na wa Mungu kama mtu huyo atakuwa anafanya dhambi ya uzinzi, au akitenda mambo maovu, au kama atakuwa mtu wa kutamani vitu zaidi na zaidi. Mtu mwenye choyo kama huyo atakuwa anamtumikia mungu wa uongo.
6 Msimruhusu mtu yeyote awadanganye kwa maneno yasiyo ya kweli. Mungu huwakasirikia sana watu wasipomtii kama hivyo. 7 Hivyo msiwe na jambo lolote pamoja nao. 8 Hapo zamani mlijaa giza, lakini sasa mmejaa nuru katika Bwana. Hivyo ishini kama watoto wa nuru. 9 Nuru hii huleta kila aina ya wema, maisha ya haki, na kweli. 10 Jaribuni kutafuta yale yanayompendeza Bwana. 11 Msishiriki katika mambo yanayotendwa na watu wa giza, yasiyosababisha jambo lolote zuri. Badala yake, mwambieni kila mtu jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 12 Hakika, ni aibu hata kuyazungumzia mambo haya wanayoyatenda sirini. 13 Lakini nuru inaonesha wazi jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 14 Ndiyo, kila kitu kinawekwa wazi na nuru. Ndiyo maana tunasema,
“Amka, wewe unayelala!
Fufuka kutoka kwa wafu,
na Kristo atakuangazia nuru yake.”
15 Hivyo, muwe makini sana jinsi mnavyoishi. Ishini kwa busara, si kama wajinga. 16 Nasema kwamba jitahidini kutumia kila fursa mliyo nayo katika kutenda mema, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Hivyo msiwe kama wajinga katika maisha yenu, bali mfahamu yale ambayo Bwana anapenda ninyi mfanye. 18 Msilewe kwa mvinyo, ambao utaharibu maisha yenu, bali mjazwe Roho. 19 Mhimizane ninyi kwa ninyi katika zaburi, nyimbo za sifa, na nyimbo zinazoongozwa na Roho. Imbeni na msifuni Bwana katika mioyo yenu. 20 Siku zote mshukuruni Mungu Baba kwa mambo yote katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Ushauiri Kwa Mke na Mume
21 Mwe radhi kuhudumiana ninyi kwa ninyi kwa kuwa mnamheshimu Kristo.
22 Wake, muwe radhi kuwahudumia waume zenu kama mlivyo radhi kumtumikia Bwana. 23 Mume ni kichwa cha mke wake, kama Kristo alivyo kichwa cha kanisa. Kristo ni Mwokozi wa kanisa, ambalo ni mwili wake. 24 Kanisa hutumika chini ya Kristo, hivyo ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi wake. Mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu katika kila jambo.
25 Waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa na kuyatoa maisha yake kwa ajili yake. 26 Alikufa ili alitakase kanisa lake. Alitumia ujumbe wa Habari Njema kulisafisha kanisa kwa kuliosha katika maji. 27 Kristo alikufa ili aweze kujiletea mwenyewe kanisa lililo kama bibi harusi katika uzuri wake wote. Alikufa ili kanisa liweze kuwa takatifu na lisilo na dosari, lisilokuwa na uovu au dhambi au chochote kilicho kibaya ndani yake.
28 Na waume wawapende hivyo wake zao. Wawapende wake zao kama vile ni miili yao wenyewe. Mtu anayempenda mkewe anajipenda mwenyewe, 29 kwa sababu kamwe hakuna anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza. Na hivyo ndivyo Kristo anavyolifanyia kanisa 30 kwa sababu sisi sote ni viungo vya mwili wake. 31 Maandiko yanasema, “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake na kuungana na mkewe, nao hao wawili watafanyika mwili mmoja.”(D) 32 Siri hiyo ya kweli ni ya muhimu sana, ninazungumza juu ya Kristo na kanisa. 33 Lakini kila mmoja wenu anapaswa kumpenda mkewe kama anavyojipenda mwenyewe. Na mke anapaswa kumheshimu mume wake.
Watoto na Wazazi Wao
6 Watoto, watiini wazazi wenu katika namna ambayo Bwana anataka, kwa sababu hili ni jambo sahihi kutenda. 2 Amri husema, “Waheshimu baba yako na mama yako.”(E) Hii ndiyo amri ya kwanza iliyo na ahadi pamoja nayo. 3 Na hii ndiyo ahadi: “Ndipo utakapofanikiwa, na utakuwa na maisha marefu duniani.”(F)
4 Wababa, msiwakasirishe watoto wenu, lakini waleeni kwa mafunzo na mausia mliyopokea kutoka kwa Bwana.
Watumwa na Bwana
5 Watumwa, watiini bwana zenu hapa duniani kwa hofu na heshima. Na fanyeni hivi kwa moyo ulio wa kweli, kama mnavyomtii Kristo. 6 Mfanye hivi siyo tu kwa kuwafurahisha bwana zenu wakati wanapowaona, bali wakati wote. Kwa vile ninyi hakika ni watumwa wa Kristo, mfanye kwa mioyo yenu yale Mungu anayotaka. 7 Fanyeni kazi zenu, na mfurahie kuzifanya. Fanyeni kana kwamba mnamtumikia Bwana, siyo tu bwana wa duniani. 8 Kumbukeni kwamba Bwana atampa kila mmoja zawadi kwa kufanya vema. Kila mmoja, mtumwa au aliye huru, atapata zawadi kwa mambo mema aliyotenda.
9 Mabwana, kwa jinsi hiyo hiyo, muwe wema kwa watumwa wenu. Msiseme mambo ya kuwatisha. Mnajua kuwa yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, na humchukulia kila mmoja sawa.
Vaeni Silaha Zote za Mungu
10 Hapa lipo neno moja la mwisho la ushauri: Mtegemeeni Bwana kwa ajili ya nguvu zenu. Wekeni matumaini yenu katika nguvu zake kuu. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kupigana dhidi ya hila za Shetani. 12 Mapigano yetu si juu ya watu duniani. Tunapigana dhidi ya watawala, mamlaka na nguvu za giza za ulimwengu huu. Tunapigana dhidi ya nguvu za uovu katika ulimwengu wa roho. 13 Ndiyo sababu mnahitaji silaha zote za Mungu. Ili siku ya uovu, mweze kusimama imara. Na mtakapomaliza mapigano yote, mtaendelea kusimama.
14 Hivyo simameni imara mkiwa mmefungwa mkanda wa kweli viunoni mwenu, na katika vifua vyenu mkiwa mmevaa kinga ya maisha ya haki. 15 Miguuni mwenu vaeni Habari Njema za amani ili ziwasaidie msimame imara. 16 Pia itumieni ngao ya imani ambayo itatumika kuizuia mishale inayowaka moto inayotoka kwa yule Mwovu. 17 Upokeeni wokovu wa Mungu kama chapeo yenu. Na chukueni upanga wa Roho, yaani mafundisho ya Mungu. 18 Ombeni katika Roho kila wakati. Ombeni maombi ya aina zote, na ombeni kila mnachohitaji. Ili mfanye hivi ni lazima muwe tayari. Msikate tamaa. Waombeeni watu wa Mungu daima.
19 Pia ombeni kwa ajili yangu ili ninapoongea, Mungu anipe maneno ili niweze kusema siri ya kweli juu ya Habari Njema bila woga. 20 Ninayo kazi ya kuhubiri Habari Njema, na hicho ndicho ninachofanya sasa humu gerezani. Niombeeni ili ninapowahubiri watu Habari Njema, nihubiri kwa ujasiri kama inavyonipasa kuhubiri.
Salamu za Mwisho
21 Namtuma kwenu Tikiko, ndugu yetu mpendwa na msaidizi mwaminifu katika kazi ya Bwana. Atawaeleza kila kitu kinachonipata. Kisha mtaelewa jinsi nilivyo na ninachofanya. 22 Ndiyo sababu namtuma yeye ili awajulishe hali zetu na tuwatie moyo.
23 Namwomba Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo awape amani, upendo na imani ndugu zangu wote mlio huko. 24 Naomba neema ya Mungu iwe pamoja nanyi nyote mnaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa pendo lisilo na mwisho.
© 2017 Bible League International