Chronological
Joka na Mwanamke Anayezaa
12 Jambo la ajabu lilionekana mbinguni: Mwanamke aliyevalishwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake alionekana. Alikuwa na taji yenye nyota kumi na mbili kichwani pake. 2 Alikuwa na mimba na alilia kwa uchungu kwa sababu alikuwa karibu ya kuzaa.
3 Kisha ajabu nyingine ikaonekana mbinguni: Alikuweko huko joka mkubwa mwekundu. Joka huyo alikuwa na vichwa saba na alikuwa na taji juu ya kila kichwa. Na alikuwa na pembe kumi. 4 Mkia wake ulizoa theluthi ya nyota na kuziangusha duniani. Joka hili lilisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa karibu ya kuzaa mtoto. Lilitaka kumla mtoto mara atakapozaliwa.
5 Mwanamke alimzaa mtoto wa kiume, atakayewatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya chuma. Na mwana wa mwanamke huyu alichukuliwa juu mbinguni kwa Mungu, kwenye kiti chake cha enzii. 6 Mwanamke alikimbilia jangwani mpaka mahali ambako Mungu amemwandalia. Huko angetunzwa kwa siku 1,260.
7 Kisha kulikuwa vita mbinguni. Mikaeli[a] na malaika zake walipigana na joka. Nalo joka na malaika zake wakapigana na Mikaeli pamoja na malaika zake, 8 lakini joka na malaika zake hawakuwa na nguvu za kutosha kushinda, na hivyo wakapoteza nafasi zao mbinguni. 9 Likatupwa chini kutoka mbinguni. (Joka hili kubwa ni nyoka yule wa zamani, aitwaye Ibilisi au Shetani, anayeudanganya ulimwengu wote.) Joka na malaika zake walitupwa duniani.
10 Kisha nilisikia sauti kubwa mbinguni ikisema:
“Ushindi na uweza na ufalme wa Mungu wetu
na mamlaka ya Masihi wake umekuja sasa,
kwa sababu mshitaki wa kaka na dada zetu
ametupwa chini.
Ndiye aliyewashitaki kwa Mungu,
mchana na usiku.
11 Walimshinda kwa sadaka ya damu ya Mwanakondoo
na kwa ujumbe wa Mungu waliowaambia watu.
Hawakuyapenda maisha yao sana.
Hawakuogopa kifo.
12 Hivyo furahi, ewe mbingu
na wote waishio humo!
Lakini ole kwa nchi na bahari,
kwa sababu Ibilisi ameshuka kwako.
Amejaa ghadhabu.
Anajua ana muda mchache.”
13 Joka alipoona amekwisha tupwa chini duniani, alimkimbiza mwanamke aliyemzaa mtoto wa kiume. 14 Lakini mwanamke alipewa mabawa mawili ya tai mkuu. Aliweza kuruka mpaka mahali palipoandaliwa kwa ajili yake jangwani. Huko atatunzwa kwa muda wa miaka mitatu na nusu akiwa mbali na joka. 15 Kisha joka lilitoa maji kama mto kutoka katika kinywa chake kuelekea kwa mwanamke ili mafuriko yamchukue. 16 Lakini nchi ilimsaidia mwanamke. Nchi ilifungua kichwa chake na kumeza mto uliotoka kwenye kinywa cha joka. 17 Kisha joka lilimkasirikia sana mwanamke. Likaenda kufanya vita na watoto wake wengine. Watoto wa mwanamke ni wale wanaozitii amri za Mungu na wanayo kweli ambayo Yesu aliifundisha.
18 Joka lilisimama ufukweni mwa bahari.
Mnyama kutoka Baharini
13 Kisha niliona mnyama mwenye pembe kumi na vichwa saba akipanda kutoka baharini. Kila pembe yake ilikuwa na taji. Alikuwa na kumkufuru Mungu lililoandikwa kwenye kila kichwa. 2 Mnyama huyu alionekana kama chui, miguu yake ilikuwa kama ya dubu. Mdomo wake ulikuwa kama wa simba. Joka akampa huyo mnyama uweza wake wote, kiti chake cha enzi na mamlaka kuu.
3 Kichwa kimoja cha mnyama kilionekana kama kimejeruhiwa na kuuawa, lakini kidonda cha mauti kilipona. Watu wote ulimwenguni walishangaa, na wote walimfuata mnyama. 4 Watu waliliabudu joka kwa sababu limempa nguvu mnyama, na pia walimwabudu mnyama. Waliuliza, “Nani ana nguvu kama mnyama? Nani anaweza kufanya vita dhidi yake?”
5 Mnyama aliruhusiwa kujigamba na kumtukana Mungu na kutumia nguvu zake kwa miezi arobaini na mbili. 6 Mnyama alifungua kinywa chake ili amtukane Mungu, alitukane jina lake, mahali anapoishi, na wale wote wanaoishi mbinguni. 7 Alipewa uwezo wa kufanya vita na watakatifu wa Mungu na kuwashinda. Alipewa uwezo juu ya kila kabila, asili, lugha na taifa. 8 Kila anayeishi duniani angemwabudu mnyama. Hawa ni watu wote ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tangu mwanzo wa ulimwengu. Mwanakondoo ndiye yule aliyeuawa.
9 Kila mtu anayesikia mambo haya azingatie hili:
10 Yeyote ambaye ni lazima awe mfungwa,
atakuwa mfungwa.
Yeyote ambaye ni wa kuuawa kwa upanga,
atauawa kwa upanga.
Hii inamaanisha kwamba watakatifu wa Mungu lazima wawe na subira na imani.
Mnyama Kutoka Nchi Kavu
11 Pia nikaona mnyama mwingine akija kutoka katika nchi. Alikuwa na pembe mbili kama kondoo, lakini anaongea kama joka. 12 Mnyama huyu alisimama mbele ya mnyama wa kwanza na kutumia nguvu ile ile ya mnyama wa kwanza. Alitumia nguvu hii kumfanya kila mtu aishiye duniani amwabudu mnyama wa kwanza. Mnyama wa kwanza ndiye mwenye jeraha la mauti lililopona. 13 Mnyama wa pili alifanya miujiza[b] mikuu. Alitengeneza hata moto ushuke kutoka mbinguni kuja duniani watu wakiangalia.
14 Mnyama huyu wa pili aliwadanganya watu wanaoishi duniani kwa kutumia miujiza ambayo amepewa uwezo wa kuifanya kwa ajili ya mnyama wa kwanza. Aliwaamuru watu kutengeneza sanamu ili kumheshimu mnyama wa kwanza, aliyejeruhiwa kwa upanga lakini hakufa bali akawa hai tena. 15 Mnyama wa pili alipewa uwezo wa kuipa uzima sanamu ya mnyama wa kwanza. Kisha kinyago kiliweza kuongea na kuamuru watu wote ambao hawakukiabudu wauawe. 16 Pia mnyama wa pili aliwaamuru watu wote, wakubwa na wadogo, matajiri na maskini, walio huru au watumwa, wawekewe alama kwenye mikono yao ya kulia au kwenye vipaji vya nyuso zao. 17 Hakuna ambaye angeweza kununua au kuuza bila ya kuwa na alama hii. (Alama hii ni jina la mnyama au namba ya jina lake.)
18 Kila mwenye uelewa anaweza kujua maana ya namba ya mnyama. Hili linahitaji hekima. Namba hii ni namba ya mtu. Nayo ni 666.
Watu wa Mungu Waimba Wimbo Mpya
14 Kisha nikatazama, na mbele yangu alikuwepo Mwanakondoo, amesimama juu ya Mlima Sayuni.[c] Watu 144,000 walikuwa pamoja naye. Jina lake na la Baba yake yalikuwa yameandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.
2 Nikasikia sauti kutoka mbinguni yenye kelele kama mafuriko au ngurumo ya radi. Lakini ilisikika kama sauti ya wapiga vinubi wapigao vinubi vyao. 3 Watu waliimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na viumbe wenye uhai wanne na wazee. Walioujua wimbo mpya ni wale 144,000 tu walionunuliwa kutoka duniani. Hakuna mwingine tena aliyekuwa anaujua.
4 Hawa ni wale ambao hawakuzini na wanawake.[d] Walijiweka safi. Na Sasa wanamfuata Mwanakondoo kila aendako. Walinunuliwa kutoka miongoni mwa watu wa dunia ili kuwa wa kwanza, kuwa sadaka kwa Mungu na Mwanakondoo. 5 Hawana hatia ya kusema uongo; hawana kosa.
Malaika Watatu
6 Kisha nikaona malaika mwingine akipaa juu angani, akitangaza Habari Njema ya milele kwa watu waishio duniani, watu wa kila taifa, kabila, lugha na rangi. 7 Malaika akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na msifuni yeye. Wakati wa Mungu kuwahukumu watu wote umefika. Mwabuduni Mungu. Aliumba mbingu, dunia, bahari na chemichemi za maji.”
8 Kisha malaika wa pili akamfuata malaika wa kwanza na kusema, “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Aliwafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.”
9 Malaika wa tatu aliwafuata malaika wawili wa kwanza. Malaika huyu wa tatu alisema kwa sauti kuu, “Mungu atawaadhibu wote wanaomwabudu mnyama na sanamu ya mnyama na kukubali kuwa na alama ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao au kwenye mkono wao. 10 Watakunywa mvinyo wa ghadhabu ya Mungu.[e] Mvinyo huu umeandaliwa kwa nguvu zake zote katika kikombe cha ghadhabu ya Mungu. Watateseka kwa maumivu ya moto uwakao kwa kiberiti mbele ya malaika watakatifu na Mwanakondoo. 11 Na moshi kutokana na kuungua kwao utasimama milele na milele. Hakutakuwa mapumziko, usiku na mchana kwa wale wamwabuduo mnyama au sanamu yake au wale wavaao alama ya jina lake.” 12 Hii inamaanisha kuwa ni lazima watakatifu wa Mungu wawe na subira. Ni lazima wazitii amri za Mungu nakuendelea kumwamini Yesu.
13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Liandike hili: Kuanzia sasa heri wale wanaokufa wakiwa wa Bwana.”
Roho Mtakatifu anasema, “Ndiyo, hilo ni kweli. Watapumzika kutokana na kazi yao ngumu. Yale waliyotenda yatakaa pamoja nao.”
Dunia Yavunwa
14 Nikatazama, na mbele yangu, katika wingu jeupe, alikuwepo mmoja aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa na taji ya dhahabu kwenye kichwa chake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, akamwambia aliyekaa kwenye wingu, “Chukua mundu wako na ukusanye kutoka duniani. Wakati wa kuvuna umefika, na tunda limeiva duniani.” 16 Hivyo aliyekaa kwenye wingu akaupitisha mundu wake juu ya dunia. Na dunia ikavunwa.
17 Ndipo malaika mwingine akatoka hekaluni mbinguni. Malaika huyu naye alikuwa na mundu mkali. 18 Na malaika mwingine, aliyekuwa msimamizi wa moto wa madhabahu akatoka madhabahuni. Akamwita malaika mwenye mundu mkali na kusema, “Chukua mundu wako wenye makali na ukusanye mafungu ya zabibu kutoka shamba la mizabibu duniani. Zabibu zimeiva duniani.” 19 Malaika akaupitisha mundu juu ya dunia. Akakusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 Zabibu zikaminywa kwenye shinikizo nje ya mji. Damu ikatiririka kutoka kwenye shinikizo, ikanyanyuka juu kama vichwa vya farasi kwa urefu wa kilomita mia tatu.[f]
Malaika Wenye Mapigo ya Mwisho
15 Ndipo nikaona ajabu nyingine mbinguni, ilikuwa kubwa na ya kushangaza. Walikuwepo malaika saba wenye mapigo saba. Haya ni mapigo ya mwisho kwa sababu baada ya haya, ghadhabu ya Mungu itakuwa imekwisha.
2 Niliona kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Wale wote waliomshinda mnyama na sanamu yake na namba ya jina lake walikuwa wamesimama kando ya bahari. Watu hawa walikuwa na vinubi walivyopewa na Mungu. 3 Waliuimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwanakondoo:
“Mambo unayotenda ni makuu na ya kushangaza,
Bwana Mungu Mwenye Nguvu.
Njia zako ni sahihi na za kweli,
mtawala wa mataifa.
4 Watu wote watakucha wewe, Ee Bwana.
Watu wote watalisifu jina lako.
Mtakatifu ni wewe peke yako.
Watu wote watakuja na kusujudu mbele yako,
kwa sababu ni dhahiri kuwa wewe hutenda yaliyo haki.”
5 Baada ya hili nikaona hekalu, mahali patakatifu pa Mungu[g] mbinguni. Likiwa wazi; 6 kisha malaika saba wenye mapigo saba wakatoka nje ya hekalu. Walikuwa wamevaa kitani safi inayong'aa. Wamevaa mikanda mipana ya dhahabu vifuani mwao. 7 Kisha mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akawapa malaika bakuli saba za dhahabu. Bakuli zilikuwa zimejaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. 8 Hekalu lilikuwa limejaa moshi uliotoka katika utukufu na nguvu ya Mungu. Hakuna ambaye angeweza kuingia hekaluni mpaka mapigo saba ya malaika saba yamemalizika.
Bakuli Zilizojazwa Ghadhabu ya Mungu
16 Kisha nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni. Ikiwaambia malaika saba, “Nendeni mkazimimine bakuli saba zenye ghadhabu ya Mungu juu ya dunia.”
2 Malaika wa kwanza akaondoka. Akaimimina bakuli yake duniani. Ndipo wale wote waliokuwa na alama ya mnyama na walioiabudu sanamu yake wakapata majipu mabaya yenye maumivu makali.
3 Malaika wa pili akaimimina bakuli yake baharini. Bahari ikawa kama damu ya mtu aliyekufa. Kila kitu kinachoishi baharini kikafa.
4 Malaika wa tatu akaimimina bakuli yake juu ya mito na chemichemi za maji. Mito na chemichemi za maji zikawa damu. 5 Ndipo nikasikia malaika wa maji akimwambia Mungu:
“Wewe ni yule uliyepo na uliyekuwepo daima.
Wewe ni Mtakatifu.
Uko sahihi kwa hukumu hizi ulizofanya.
6 Watu walimwaga damu za
watakatifu na manabii wako.
Sasa umewapa watu hao damu ili wanywe.
Hiki ndicho wanachostahili.”
7 Pia nikasikia madhabahu ikisema:
“Ndiyo, Bwana Mungu Mwenye Nguvu,
hukumu zako ni za kweli na za haki.”
8 Malaika wa nne akaimimina bakuli yake juu ya jua. Jua lilipewa nguvu kuwachoma watu kwa moto. 9 Watu wakaungua kwa joto kali. Wakalilaani jina la Mungu, mwenye mamlaka juu ya mapigo haya. Lakini walikataa kubadili mioyo na maisha yao, na kumpa Mungu utukufu.
10 Malaika wa tano akaimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha mnyama. Giza likaufunika ufalme wa mnyama. Watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu. 11 Wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majipu waliyokuwa nayo. Lakini walikataa kubadili mioyo yao na kuyaacha maovu wanayotenda.
12 Malaika wa sita akaimimina bakuli yake juu ya mto mkuu Frati. Maji yaliyokuwa mtoni yakakauka. Hili likaandaa njia kwa ajili ya watawala kutoka mashariki kuweza kupita. 13 Kisha nikaona roho chafu tatu zilizoonekana kama vyura. Walitoka katika kinywa cha joka, kinywa cha mnyama, na kinywa cha nabii wa uongo. 14 Roho hizi chafu ni roho za mapepo. Zina nguvu za kutenda miujiza.[h] Nazo huenda kwa watawala wa ulimwengu wote na kuwakusanya kwa ajili ya mapigano siku ile Mungu Mkuu Mwenye Nguvu.
15 “Sikilizeni! Nitakuja kama mwizi wakati msioutarajia. Heri watakaokuwa macho na waliovaa nguo zao. Hawatakwenda wakiwa uchi na kuona aibu watakapoonwa na watu.”
16 Ndipo roho chafu zikawakusanya pamoja watawala pamoja mahali ambapo kwa Kiebrania panaitwa “Armagedoni”.
17 Malaika wa saba akaimimina bakuli yake angani. Sauti kuu ikatoka hekaluni katika kiti cha enzi. Ikasema, “Imekwisha!” 18 Kisha kukawa na mwako wa radi, kelele, ngurumo za radi na tetemeko kuu la nchi. Hili lilikuwa tetemeko kuu kuwahi kutokea tangu watu walipokuwepo duniani. 19 Mji mkuu ukagawanyika vipande vitatu. Miji ya mataifa ikaharibiwa. Na Mungu hakusahau kuuadhibu Babeli Mkuu. Aliupa mji ule kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu yake kuu. 20 Kila kisiwa kikatoweka na milima ikasawazika, hakukuwa milima yoyote tena. 21 Mvua yenye mawe makubwa kutoka mbinguni ikawanyeshea watu. Mawe haya yalikuwa na uzito wa kilo 40[i] kila jiwe. Watu wakamlaani Mungu kwa sababu ya mvua hii ya mawe. Hali hiyo Ilitisha sana.
Mwanamke Juu ya Mnyama Mwekundu
17 Mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli sa akaja kuzungumza nami. Akasema, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu itakayotolewa kwa kahaba maarufu. Ndiye yule aketiye juu ya maji mengi. 2 Watawala wa dunia walizini pamoja naye. Watu wa dunia walilewa kutokana na mvinyo wa dhambi yake ya uzinzi.”
3 Kisha malaika akanichukua mbali kwa Roho Mtakatifu mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke amekaa juu ya mnyama mwekundu. Mnyama alikuwa ameandikwa majina ya kumkufuru Mungu katika mwili wake wote. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. 4 Mwanamke aliyekuwa juu yake alikuwa amevaa nguo za zambarau na nyekundu. Alikuwa anang'aa kutokana na dhahabu, vito na lulu alizokuwa amevaa. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu. Kikombe hiki kilijaa maovu na machukizo ya dhambi yake ya uzinzi. 5 Alikuwa na jina kwenye kipaji cha uso wake. Jina hili lina maana iliyofichwa. Hiki ndicho kilichoandikwa:
babeli mkuu
mama wa makahaba
na machukizo ya dunia.
6 Nikatambua kuwa mwanamke alikuwa amelewa. Alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu wa Mungu. Alikuwa amelewa kwa damu ya wale walioshuhudia imani yao katika Yesu Kristo.
Nilipomwona mwanamke, nilishangaa sana. 7 Kisha malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Nitakuambia maana iliyofichwa kuhusu mwanamke huyu na mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumi anayeendeshwa na mwanamke huyu. 8 Mnyama unayemwona alikuwa hai kwanza, lakini sasa si hai. Hata hivyo, atapanda kutoka kuzimu na kwenda kuangamizwa. Watu wanaoishi duniani watashangaa watakapomwona mnyama, kwa sababu aliwahi kuwa hai, hayuko hai, lakini atakuwa hai tena. Hawa ni watu ambao majina yao hayajawahi kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu.
9 Unahitaji hekima kulielewa hili. Vichwa saba juu ya mnyama ni milima saba ambako mwanamke amekaa. Pia ni watawala saba. 10 Watawala watano wamekwisha kufa tayari. Mmoja wa watawala anaishi sasa, na mtawala wa mwisho anakuja. Atakapokuja, atakaa kwa muda mfupi tu. 11 Mnyama ambaye hapo kwanza alikuwa hai, lakini haishi tena ni mtawala wa nane. Naye ni mmoja wa watawala saba wa kwanza. Naye ataangamizwa.
12 Pembe kumi ulizoziona ni watawala kumi. Watawala hawa kumi hawajapata falme zao, lakini watapata nguvu ya kutawala pamoja na mnyama kwa saa moja. 13 Lengo la watawala hawa wote kumi linafanana. Nao watampa mnyama nguvu na mamlaka yao. 14 Watafanya vita kinyume na Mwanakondoo. Lakini Mwanakondoo atawashinda, kwa sababu ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Pamoja naye watakuwepo wateule wake na wafuasi waaminifu, watu aliowaita kuwa wake.”
15 Kisha malaika akaniambia, “Uliyaona maji ambako kahaba amekaa. Maji haya ni watu wengi, wa asili, mataifa, na lugha tofauti ulimwenguni. 16 Mnyama na pembe kumi ulizoziona watamchukia kahaba. Watachukua kila kitu alichonacho na kumwacha akiwa uchi. Watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. 17 Mungu aliweka wazo katika akili zao kutenda yale yatakayotimiza kusudi lake. Walikubaliana kumpa mnyama nguvu zao kutawala mpaka yale aliyosema Mungu yamekamilika. 18 Mwanamke uliyemwona ni mji mkuu ambao unatawala juu ya wafalme wa dunia.”
Babeli Inaangamizwa
18 Kisha nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Malaika huyu alikuwa na nguvu kuu. Utukufu wa malaika ukaing'arisha dunia. 2 Malaika akapaza sauti akasema:
“Ameteketezwa!
Mji mkuu Babeli umeteketezwa!
Umekuwa nyumba ya mapepo.
Mji ule umekuwa najisi.
Mji uliojaa kila aina ya ndege najisi.
Ni mahali ambapo kila mnyama najisi
na anayechukiwa anaishi.
3 Watu wote wa dunia wamekunywa mvinyo
wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.
Watawala wa dunia walizini pamoja naye,
na wafanya biashara wa ulimwengu walitajirika
kutokana na utajiri wa anasa zake.”
4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:
“Enyi watu wangu, tokeni katika mji huo,
ili msishiriki katika dhambi zake.
Ili msiteseke kwa adhabu yoyote kuu atakayoipata.
5 Dhambi za mji huo zimerundikana na kufika mbinguni.
Mungu hajasahau makosa aliyotenda.
6 Upeni mji huo sawasawa na ulivyowapa wengine.
Mlipeni mara mbili kadiri ya alivyotenda.
Mwandalieni mvinyo ulio na nguvu mara mbili
ya mvinyo aliowaandalia wengine.
7 Alijipa utukufu mwingi na kuishi kitajiri.
Mpeni mateso mengi na huzuni nyingi.
Kama vile utukufu na starehe aliyoifurahia.
Hujisemea mwenyewe, ‘Mimi ni malkia nikaaye kwenye kiti changu cha enzi.
Mimi si mjane;
Sitakuwa na huzuni.’
8 Hivyo katika siku moja atateseka
kwa njaa kuu, maombolezo na kifo.
Atateketezwa kwa moto,
kwa sababu Bwana Mungu anayemhukumu ni mwenye nguvu.”
9 Watawala wa dunia waliozini pamoja naye na kushiriki utajiri wake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watalia na kuhuzunika kwa sababu ya kifo chake. 10 Wataogopa mateso yake na kukaa mbali sana. Watasema:
“Inatisha! Inatisha sana, Ee mji mkuu,
ee Babeli, mji wenye nguvu!
Adhabu yako imekuja katika saa moja!”
11 Na wafanya biashara wa dunia watalia na kuhuzunika kwa ajili yake. Watahuzunika kwa sababu hakutakuwa hata mmoja wa kununua vitu wanavyouza; 12 dhahabu, fedha, vito, lulu, nguo za kitani safi, nguo za zambarau, hariri na nguo nyekundu, aina zote za mti wa udi, na aina zote za vitu vilivyotengenezwa kutokana na pembe za wanyama, miti ya thamani, shaba, chuma, na marimari. 13 Na mdalasini, viungo, uvumba, marhamu, ubani, mvinyo, mafuta ya mzeituni, unga safi, ngano, ng'ombe, kondoo, farasi, magari na watumwa, ndiyo hata maisha ya watu. Wafanya biashara watalia na kusema:
14 “Ee Babeli, mambo mazuri uliyoyataka yamekuacha.
Utajiri wako wote na vitu vya fahari vimetoweka.
Hautakuwa navyo tena.”
15 Wafanya biashara wataogopa mateso yake na watakaa mbali naye. Hawa ni wale waliotajirika kwa kumwuzia vitu hivyo. Watalia na kuhuzunika. 16 Watasema:
“Inatisha! Inatisha kwa mji mkuu!
Alivalishwa kitani safi;
alivaa zambarau na nguo nyekundu.
Alikuwa anang'aa kwa sababu ya dhahabu, vito na lulu!
17 Utajiri wote huu umeteketezwa kwa saa moja!”
Kila nahodha, wote ambao husafiri katika meli, mabaharia na wote ambao hupata pesa kutokana na bahari walisimama mbali na Babeli. 18 Waliuona moshi wa kuungua kwake. Walilia kwa sauti, “Hakukuwa na mji kama mji huu mkuu!” 19 Walirusha mavumbi juu ya vichwa vyao na kulia kwa sauti kuu kuonesha huzuni kuu waliyokuwa nayo. Walisema:
“Inatisha! Inatisha sana kwa mji mkuu!
Wote waliokuwa na meli baharini walitajirika kwa sababu ya utajiri wake!
Lakini umeteketezwa katika saa moja!
20 Ufurahi kwa sababu ya hili, Ee mbingu!
Furahini, watakatifu wa Mungu, mitume na manabii!
Mungu amemhukumu kwa sababu ya kile alichowatendea ninyi.”
21 Kisha malaika mwenye nguvu akainua jiwe kubwa. Jiwe hili lilikuwa kubwa kama jiwe kubwa la kusagia. Malaika akalitupia jiwe baharini na kusema:
“Hivyo ndivyo mji mkuu Babeli utakavyotupwa chini.
Hautaonekana tena.
22 Ee Babeli, muziki wa wapigao vinanda na ala zingine waimbaji na tarumbeta,
hautasikika tena ndani yako.
Hakuna mfanyakazi afanyaye kazi atakayeonekana ndani yako tena.
Sauti ya jiwe la kusagia haitasikika ndani yako tena.
23 Mwanga wa taa hautang'aa ndani yako tena.
Sauti za maarusi hazitasikika ndani yako tena.
Wafanyabiashara wako walikuwa watu wakuu wa ulimwengu.
Mataifa yote yalidanganyika kwa uchawi wako.
24 Una hatia ya vifo vya manabii, na watakatifu wa Mungu,
na vya wote waliouawa duniani.”
© 2017 Bible League International