Chronological
Imani
11 Imani inaleta uthabiti wa mambo tunayoyatarajia. Ni uthibitisho wa yale tusiyoweza kuyaona. 2 Mungu alifurahishwa na watu walioishi muda mrefu uliopita kwa sababu walikuwa na imani ya namna hii.
3 Imani hutusaidia sisi kufahamu kwamba Mungu aliumba ulimwengu wote kwa amri yake. Hii inamaanisha kwamba vitu tunavyoviona viliumbwa kwa kitu kisichoonekana.
4 Kaini na Habili wote walitoa sadaka kwa Mungu. Lakini Habili alitoa sadaka bora zaidi kwa Mungu kwa sababu alikuwa na imani. Mungu akasema alifurahishwa na kile alichotoa Habili. Na hivyo Mungu akamwita kuwa mtu mwema kwa sababu alikuwa na imani. Habili akafariki, lakini kupitia imani yake bado anazungumza.
5 Henoko alitwaliwa kutoka duniani, hivyo kamwe yeye hajafariki. Maandiko yanatueleza kwamba kabla ya kuchukuliwa, alikuwa mtu aliyempendeza Mungu. Baadaye, hayupo yeyote aliyejua kule alikokuwa, kwa sababu Mungu alimchukua Henoko ili awe pamoja naye. Haya yote yakatokea kwa vile alikuwa na imani. 6 Bila kuwa na imani hakuna anayeweza kumfurahisha Mungu. Yeyote anayemjia Mungu anatakiwa kuamini kwamba yeye ni hakika na kwamba anawalipa wale ambao kwa uaminifu wanajitahidi kumtafuta.
7 Nuhu alionywa na Mungu juu ya mambo ambayo hakuwa ameyaona bado. Lakini alikuwa na imani na heshima kwa Mungu, hivyo akaijenga meli kubwa ili kuiokoa familia yake. Kwa imani yake, Nuhu alionesha kwamba ulimwengu ulikuwa umekosea. Na akawa ni mmoja wa wale waliohesabiwa haki na Mungu kwa njia ya imani.
8 Mungu alimwita Ibrahimu kusafiri kwenda sehemu ingine aliyoahidi kumpa. Ibrahimu hakujua hiyo sehemu ingine ilikuwa wapi. Lakini alimtii Mungu na akaanza kusafiri kwa sababu alikuwa na imani. 9 Ibrahimu akaishi katika nchi ambayo Mungu aliahidi kumpa. Akaishi humo kama mgeni tu asiyekuwa mwenyeji. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. Akaishi katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo, ambao pia walipokea ahadi ile ile kutoka kwa Mungu. 10 Ibrahimu alikuwa anaungoja mji[a] ambao ulikuwa na misingi halisi. Alikuwa anaungoja mji ulibuniwa na kujengwa na Mungu.
11 Sara hakuwa na uwezo wa kupata watoto, na Ibrahimu alikuwa amezeeka sana. Lakini alikuwa anamwamini Mungu, akimwamini kuwa anaweza kutenda yale aliyoahidi. Hivyo Mungu akawawezesha kupata watoto. 12 Ibrahimu alikuwa amezeeka sana karibu ya kufa. Lakini kupitia kwa mtu huyo mmoja vikaja vizazi vingi kama zilivyo nyota za angani. Hivyo watu wengi wakaja kutoka kwake wakiwa kama punje za mchanga katika ufukwe wa bahari.
13 Watu hawa wote mashuhuri wakaendelea kuishi kwa imani hadi walipofariki. Hawakuwa wamepata mambo ambayo Mungu aliwaahidi watu wake. Lakini walikuwa na furaha kuona tu kwamba ahadi hizi zilikuwa zinakuja kwa mbali siku zijazo. Waliukubali ukweli kwamba wao walikuwa kama wageni na wasafiri hapa duniani. 14 Watu wanapolikubali jambo la namna hiyo, wanaonesha kuwa wanaingojea nchi itakayokuwa yao wenyewe. 15 Kama wangekuwa wanaifikiria nchi walikotoka, wangekuwa wamerejea. 16 Lakini walikuwa wanaingoja nchi iliyo bora zaidi, nchi ya mbinguni. Hivyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao. Naye amewaandalia mji.
17-18 Mungu aliijaribu imani ya Ibrahimu. Mungu alimtaka amtoe Isaka kama sadaka. Ibrahimu akatii kwa sababu alikuwa na imani. Tayari alikuwa na ahadi kutoka kwa Mungu. Na Mungu tayari alikuwa amekwishamwambia, “Ni kupitia kwa Isaka kwamba vizazi vyako watakuja.”(A) Lakini Ibrahimu alikuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 19 Aliamini kwamba Mungu angeweza kuwafufua watu kutoka kifoni. Na hakika, Mungu alipomzuia Ibrahimu katika kumuua Isaka, ilikuwa ni kama vile alimpata tena kutoka kifoni.
20 Isaka akayabariki maisha ya mbeleni ya Yakobo na Esau. Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na imani. 21 Na Yakobo, pia kwa vile alikuwa na imani, alimbariki kila mmoja wa wana wa Yusufu. Alifanya haya wakati alipokuwa akifa, akaiegemea fimbo yake akimwabudu Mungu.
22 Na Yusufu alipokuwa karibu amefariki, alizungumza kuhusu watu wa Israeli kuondoka Misri. Na aliwaambia yale waliyotakiwa kuufanyia mwili wake. Alifanya haya kwa sababu alikuwa na imani.
23 Na mama na baba wa Musa wakaona kwamba alikuwa ni mtoto mzuri hivyo wakamficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Hili lilikuwa kinyume na agizo la mfalme. Lakini hawakuogopa kwa sababu walikuwa na imani.
24-25 Musa akakua na akawa mwanaume. Akakataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kutokujifurahisha katika raha na dhambi zinazodumu kwa muda mfupi tu. Badala yake, akachagua kuteseka pamoja na watu wa Mungu. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 26 Alifikiri kuwa ni bora kuteseka kwa ajili ya Masihi kuliko kuwa na hazina zote za Misri. Alikuwa anaisubiri malipo ambayo Mungu angempa.
27 Musa akaondoka Misri kwa sababu alikuwa na imani. Hakuiogopa hasira ya mfalme. Aliendelea kuwa jasiri kama vile angemwona Mungu ambaye hakuna mtu mwingine angeweza kumwona. 28 Na kwa sababu alikuwa na imani, Musa akaandaa mlo wa Pasaka. Na akanyunyiza damu ya mwanakondoo katika miimo ya milango ya watu wake, ili kwamba malaika wa kifo[b] asiwaue wazaliwa wao wa kwanza wa kiume.
29 Na watu wa Mungu wote wakatembea kuvuka Bahari ya Shamu kama vile ilikuwa ni ardhi kavu. Waliweza kufanya hivi kwa sababu walikuwa na imani. Lakini wakati Wamisri walipojaribu kuwafuata, wote wakazama majini.
30 Na kuta za Yeriko zilianguka kwa ajili ya imani ya watu wa Mungu. Walitembea kuuzunguka ukuta kwa siku saba, na kisha kuta zikaanguka.
31 Na Rahabu, yule kahaba, aliwakaribisha wapelelezi wa Kiisraeli kama marafiki. Na kwa sababu ya imani yake, hakuuawa pamoja na wale waliokataa kutii.
32 Je, nahitaji niwape mifano zaidi? Sina muda wa kutosha kuwaeleza kuhusu Gidioni, Baraki, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii. 33 Wote walikuwa na imani kuu. Na kwa njia ya imani hiyo wakaziangusha falme. Wakafanya kilichokuwa sahihi, na Mungu akawasaidia katika njia alizoahidi. Kwa imani zao watu wengine waliifunga midomo ya simba. 34 Na wengine waliweza kuizuia miali ya moto. Wengine wakaepuka katika kuuawa kwa upanga. Wengine waliokuwa dhaifu wakafanywa wenye nguvu. Wakawa na nguvu katika vita na kuyaangusha majeshi mengine. 35 Walikuwepo wanawake waliowapoteza wapendwa wao lakini wakawapata tena walipofufuliwa kutoka wafu. Wengine waliteswa lakini wakakataa kuukubali uhuru wao. Walifanya hivi ili waweze kufufuliwa kutoka kifoni kuingia katika maisha bora zaidi. 36 Wengine walichekwa na kupigwa. Wengine walifungwa na kutiwa magerezani. 37 Waliuawa kwa mawe. Walikatwa vipande viwili. Waliuawa kwa panga. Mavazi pekee wengine wao waliyokuwa nayo yalikuwa ni ngozi za kondoo au za mbuzi. Walikuwa maskini, waliteswa, na kutendewa mabaya na wengine. 38 Ulimwengu haukustahili kuwa na watu wakuu na waaminifu kama hawa. Hawa waliweza kuzunguka jangwani na milimani, wakiishi katika mapango na mashimo ardhini.
39 Mungu alifurahishwa nao wote kwa sababu ya imani zao. Lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea ahadi ya Mungu. 40 Mungu alikusudia kitu bora zaidi kwa ajili yetu. Alitaka kutukamilisha sisi. Hakika, pia alitaka watu hawa wakuu wakamilishwe, lakini siyo kabla ya sisi wote kuzifurahia baraka pamoja.
Sisi Pia Tuufuate Mfano wa Yesu
12 Tunao hawa watu mashuhuri wakituzunguka kama mifano kwetu. Maisha yao yanatueleza imani ni nini. Hivyo, nasi pia, tunapaswa kufanya mashindano yaliyo mbele yetu na kamwe tusikate tamaa. Tunapaswa kuondoa katika maisha yetu kitu chochote kitakachotupunguzia mwendo pamoja na dhambi zinazotufanya tutoke kwenye mstari mara kwa mara. 2 Hatupaswi kuacha kumwangalia Yesu. Yeye ndiye kiongozi wa imani yetu, na ndiye anayeikamilisha imani yetu. Aliteseka hadi kufa msalabani. Lakini aliikubali aibu ya msalaba kama kitu kisicho na maana kwa sababu ya furaha ambayo angeiona ikimngojea. Na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mfikirie Yesu. Kwa uvumilivu alistahimili matusi ya hasira ya watenda dhambi waliokuwa wakiwapigia kelele. Mfikirie yeye ili usikate tamaa na kuacha kujaribu.
Mungu ni Kama Baba
4 Mnashindana na dhambi, lakini bado hamjamwaga damu hata kuutoa uhai wenu katika mashindano hayo. 5 Ninyi ni watoto wa Mungu, naye huzungumza maneno ya faraja kwenu. Labda mmeyasahau maneno haya:
“Mwanangu, wakati Mungu anapokurekebisha,
zingatia na usiache kujaribu.
6 Bwana humrekebisha kila anayempenda;
humpa adhabu kila anayemkubali kama mwana wake.”(B)
7 Hivyo muyapokee mateso kama adhabu ya baba. Mungu hufanya mambo haya kwenu kama baba anavyowarekebisha watoto wake. Mnajua kuwa watoto wote hurekebishwa na baba zao. 8 Hivyo, kama hukupata marekebisho ambayo kila mtoto anapaswa kuyapata, wewe siyo mtoto wa kweli na hakika wewe siyo wa Mungu. 9 Sisi wote tulikuwa na baba wa hapa duniani walioturekebisha, na tuliwaheshimu. Ni muhimu zaidi basi kwamba tunapaswa kuyapokea marekebisho kutoka kwa Baba wa roho zetu. Tukifanya hivyo, tutakuwa na uzima. 10 Baba zetu wa duniani waliturekebisha kwa muda mfupi katika njia waliyofikiri ilikuwa bora zaidi. Lakini Mungu huturekebisha sisi ili atusaidie tuweze kuwa watakatifu kama yeye. 11 Hatufurahii marekebisho tunapokuwa tunayapata. Yanauma. Lakini baadaye, baada ya kujifunza somo kutokana na hayo, tutaifurahia amani itakayokuja kwa njia ya kufanya yaliyo sahihi.
Muwe Makini Jinsi Mnavyoishi
12 Mmekuwa dhaifu, hebu mjitie nguvu tena. 13 Muishi katika njia iliyo sahihi ili muweze kuokolewa na udhaifu wenu hautawasababisha ninyi kupotea.
14 Jitahidini kuishi kwa amani na kila mtu. Na mjitahidi kuyaweka mbali na dhambi maisha yenu. Yeyote ambaye maisha yake siyo matakatifu hawezi kumwona Bwana. 15 Muwe makini ili mtu asije akakosa kuipata neema ya Mungu. Muwe makini ili asiwepo atakayepoteza imani yake na kuwa kama gugu chungu linalomea miongoni mwenu. Mtu wa jinsi hiyo anaweza kuharibu kundi lenu lote. 16 Muwe makini ili asiwepo yeyote atakayefanya dhambi ya uzinzi au kushindwa kumheshimu Mungu moyoni kama alivyofanya Esau. Kama kijana mkubwa katika nyumba ya babaye, Esau angerithi sehemu kubwa ya vitu kutoka kwa baba yake. Lakini akauza kila kitu kwa mlo mmoja tu. 17 Mnakumbuka kwamba baada ya Esau kufanya hivi, akataka kupata baraka za baba yake. Akaitamani sana baraka ile kiasi kwamba akalia. Lakini baba yake akakataa kumpa baraka hiyo, kwa sababu Esau hakupata njia ya kubadili yale aliyotenda.
18 Ninyi ni watu wa Mungu, kama watu wa Israeli walipofika katika Mlima Sinai. Lakini hamjaufikia mlima halisi wa kuweza kushikwa. Mlima huo haupo kama ule waliouona, uliokuwa ukiwaka moto na kufunikwa na giza, utusitusi na dhoruba. 19 Haipo sauti ya tarumbeta au sauti iliyoyasema maneno kama hayo waliyoyasikia. Walipoisikia sauti, wakasihi kamwe wasisikie neno lingine. 20 Hawakutaka kusikia amri: “Kama chochote, hata mnyama, akigusa mlima, lazima kiuawe kwa kupigwa mawe.”(C) 21 Kile walichoona kilikuwa cha kutisha kiasi kwamba Musa akasema, “Natetemeka kwa hofu.”(D)[c]
22 Lakini mmeufikia Mlima Sayuni, kwenye mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni.[d] Mmefika mahali ambapo maelfu wa malaika wamekusanyika kusherehekea. 23 Mmefika katika kusanyiko la watoto wazaliwa wa kwanza wa Mungu. Majina yao yameandikwa mbinguni. Mmemfikia Mungu, hakimu wa watu wote. Na mmefika kwenye roho za watu wema ambao wamekamilishwa. 24 Mmemfikia Yesu; yeye aliyelileta kutoka kwa Mungu agano jipya kwenda kwa watu wake. Mmefika kwenye damu iliyonyunyizwa[e] ambayo inasema habari za mema zaidi kuliko damu ya Habili.
25 Muwe makini na msijaribu kupuuza kusikiliza Mungu anaposema. Watu wale walipuuza kumsikiliza yeye alipowaonya hapa duniani. Nao hawakuponyoka. Sasa Mungu anasema kutoka mbinguni. Hivyo sasa itakuwa vibaya zaidi kwa wale watakaopuuza kumsikiliza yeye. 26 Alipozungumza pale mwanzoni, sauti yake iliitetemesha dunia. Lakini sasa ameahidi, “Kwa mara nyingine tena nitaitetemesha dunia, lakini pia nitazitetemesha mbingu.”(E) 27 Maneno “Kwa mara nyingine” yanatuonyesha kwa uwazi kwamba kila kitu kilichoumbwa kitaangamizwa; yaani, vitu vinavyoweza kutetemeshwa. Na ni kile tu kisichoweza kutetemeshwa kitakachobaki.
28 Hivyo tunahitajika kuwa na shukrani kwa sababu tunao ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa. Na kwa sababu sisi ni watu wa shukrani, tunahitajika kumwabudu Mungu kwa njia itakayompendeza yeye. Tunahitajika kufanya hivi kwa heshima na hofu, 29 kwa sababu “Mungu wetu yuko kama moto unaoweza kutuangamiza sisi.”(F)
Ibada Inayompendeza Mungu
13 Endeleeni kupendana ninyi kwa ninyi kama kaka na dada katika Kristo. 2 Mkikumbuka kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha majumbani mwenu. Watu wengine wamefanya hivyo na wakawa wamewasaidia malaika pasipo wao kujua. 3 Msiwasahau wale walioko magerezani. Wakumbukeni kama vile mko magerezani pamoja nao. Na msiwasahau wale wanaoteseka. Wakumbukeni kama vile mnateseka pamoja nao.
4 Ndoa iheshimiwe na kila mmoja. Na kila ndoa itunzwe kwa usafi kati ya mume na mke. Mungu atawahukumu kuwa na hatia wale wanaofanya uzinzi na uasherati. 5 Yatunzeni maisha yenu yawe huru kutokana na kupenda fedha. Na mridhike na kile mlichonacho. Mungu amesema: “Sitakuacha kamwe; Sitakukimbia kamwe.”(G) 6 Hivyo tunaweza kuwa na uhakika na kusema:
“Bwana ndiye msaidizi wangu;
Sitaogopa.
Watu hawawezi kunifanya chochote.”(H)
7 Wakumbukeni viongozi wenu. Waliwafundisha ujumbe wa Mungu. Kumbukeni jinsi walivyoishi na walivyokufa, na muiige imani yao. 8 Yesu Kristo ni yule yule jana, leo na hata milele. 9 Msiruhusu aina yoyote ya mafundisho mageni yawaongoze hadi katika njia isiyo sahihi. Itegemeeni neema ya Mungu pekee kwa ajili ya nguvu za kiroho, siyo katika sheria kuhusu vyakula. Kuzitii sheria hizi hakumsaidii yeyote.
10 Tunayo sadaka. Na wale makuhani waliotumika ndani ya Hema Takatifu hawawezi kula sadaka tuliyo nayo. 11 Kuhani mkuu hubeba damu za wanyama hadi Patakatifu pa Patakatifu na hutoa damu hiyo kwa ajili ya dhambi. Lakini miili ya wanyama hao huchomwa nje ya kambi. 12 Hivyo Yesu naye alitesekea nje ya mji. Alikufa ili awatakase watu wake kwa damu yake mwenyewe. 13 Hivyo tumwendee Yesu nje ya kambi na kuikubali aibu hiyo hiyo aliyoipata yeye. 14 Hatuna mji unaodumu milele hapa duniani. Lakini tunaungoja mji tutakaoupata hapo baadaye. 15 Hivyo kwa njia ya Yesu hatupaswi kuacha kumtolea Mungu sadaka zetu. Dhabihu hizo ni sifa zetu, zinazotoka katika vinywa vyetu vinavyolisema jina lake. 16 Na msisahau kutenda mema na kushirikishana na wengine mlivyo navyo, kwa sababu sadaka kama hizi zinamfurahisha sana Mungu.
17 Muwatii viongozi wenu. Muwe tayari kufanya yale wanayowaambia. Wanawajibika katika maisha yenu ya kiroho, hivyo nyakati zote wanaangalia jinsi ya kuwalinda ninyi. Muwatii ili kazi yao iwafurahishe wao, siyo kupata majonzi. Haitawasaidia ninyi mnapowasababishia matatizo.
18 Endeleeni kutuombea. Tunajisikia tuko sahihi katika tunayoyafanya, kwa sababu nyakati zote tunajitahidi kadri tuwezavyo. 19 Na nawasihi muombe ili Mungu anirudishe tena kwenu mapema. Nalitamani sana hili kuliko kitu chochote.
20-21 Ninawaombea Mungu wa amani awape ninyi mambo mazuri mnayohitaji ili muweze kufanya anayoyapenda. Mungu ndiye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka katika kifo, Mchungaji Mkuu wa kondoo wake. Alimfufua kwa sababu Yesu aliitoa sadaka ya damu yake ili kulianza agano jipya lisilo na mwisho. Namwomba Mungu atuwezeshe kwa njia ya Yesu Kristo kufanya mambo yanayompendeza yeye. Utukufu ni wake milele. Amina.
22 Ndugu na dada zangu, nawasihi msikilize kwa uvumilivu katika yale niliyoyasema. Niliandika barua hii ili kuwatia moyo. Na siyo ndefu sana. 23 Nawataka mjue kwamba ndugu yetu Timotheo ametoka gerezani. Akija kwangu mapema, sote tutakuja kuwaona ninyi.
24 Fikisheni salama zangu kwa viongozi wote na kwa watu wote wa Mungu. Wote walioko Italia wanawasalimuni.
25 Naomba neema ya Mungu iwe nanyi nyote.
© 2017 Bible League International