Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Ufunuo 6-11

Mwanakondoo Afungua Kitabu

Kisha nilitazama Mwanakondoo alipokuwa anaufungua muhuri[a] wa kwanza kati ya mihuri saba. Kisha nikasikia sauti ya mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akisema kwa sauti kama ngurumo ya radi ikisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mweupe mbele yangu. Mwendesha farasi aliyekuwa amempanda farasi huyo alikuwa na upinde na alipewa taji. Alimwendesha farasi akatoka kwenda kumshinda adui na ili kupata ushindi.

Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa pili, nilimsikia kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mwekundu akitokea. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alipewa mamlaka ya kuondoa amani duniani ili watu wauane. Alipewa upanga mkubwa.

Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tatu. Nilisikia kiumbe mwenye uhai wa tatu akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mweusi mbele yangu. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alikuwa na mizani mkononi mwake. Kisha nilisikia kitu kilichosikika kama sauti ikitokea pale walipokuwa viumbe wenye uhai wanne. Kikisema, “Kilo moja[b] ya ngano au kilo tatu ya shayiri itagharimu mshahara wote wa siku moja. Lakini usiharibu upatikanaji wa mafuta ya mzeituni na divai!”

Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa nne nilisikia sauti ya kiumbe wa nne mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mwenye rangi ya kijivu. Aliyempanda alikuwa mauti na kuzimu ilikuwa inamfuata nyuma yake kwa karibu. Alipewa mamlaka juu ya robo ya dunia kuwaua watu kwa upanga, njaa, magonjwa na kwa wanyama wa porini waliomo duniani.

Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tano, niliziona baadhi ya roho za wale waliokuwa waaminifu kwa neno la Mungu na kweli waliyopokea zikiwa chini ya madhabahu. 10 Roho hizi zilipiga kelele kwa sauti kuu zikisema, “Mtakatifu na Bwana wa kweli, ni lini utakapowahukumu watu wa dunia na kuwaadhibu kwa kutuua sisi?” 11 Kisha kila mmoja wao alipewa kanzu ndefu nyeupe. Wakaambiwa wasubiri kwa muda mfupi kwani bado walikuwepo ndugu zao katika utumishi wa Kristo ambao ni lazima wauawe kama wao. Roho hizi ziliambiwa zisubiri mpaka mauaji yote yatakapokwisha.

12 Kisha nilitazama wakati Mwanakondoo anaufungua muhuri wa sita. Kulitokea tetemeko kubwa la ardhi na jua likawa jeusi kama gunia jeusi[c] na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zikaanguka chini duniani kama mtini uangushavyo tini zake upepo unapovuma. 14 Anga iligawanyika katikati na pande zote zikajiviringa kama kitabu.[d] Na kila mlima na kisiwa kiliondolewa mahali pake.

15 Kisha watu wote wa ulimwengu, wafalme, watawala, makamanda wa majeshi, matajiri, wenye mamlaka na nguvu, kila mtumwa na asiye mtumwa, walijificha katika mapango na nyuma ya miamba milimani. 16 Waliiambia milima na miamba, “Tuangukieni. Tuficheni mbali na uso wa yule aketiye kwenye kiti cha enzi. Tuficheni dhidi ya hasira ya Mwanakondoo! 17 Siku kubwa ya hasira yao imefika. Hakuna anayeweza kupingana nayo.”

Watu 144,000 wa Israeli

Baada ya hili kutokea, niliwaona malaika wanne wamesimama kwenye pembe nne za dunia wakiwa wamezishikilia pepo nne za dunia. Walikuwa wanazuia upepo kupuliza katika nchi au katika bahari au kwenye mti wowote. Kisha nikaona malaika mwingine akija akitokea upande wa mashariki. Malaika huyu alikuwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Malaika akawaita kwa sauti kuu malaika wale wanne. Malaika hawa wanne walikuwa malaika ambao Mungu amewapa mamlaka ya kuidhuru dunia na bahari. Malaika akawaambia, “Msiidhuru nchi au bahari au miti kabla hatujawawekea alama kwenye vipaji vya nyuso zao wale wanaomtumikia Mungu wetu.”

Kisha nikasikia idadi ya watu wenye alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. Walikuwa watu 144,000. Walitoka katika kila kabila la Israeli:

Kutoka katika kabila la Yuda walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Rubeni walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Gadi walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Asheri walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Naftali walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Manasse walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Simeoni walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Lawi walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Isakari walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Zabuloni walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Yusufu walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Benjamini walikuwa elfu kumi na mbili.

Umati Mkubwa

Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu. Walikuwa wengi hakuna mtu angeweza kuwahesabu wote. Walikuwa wametoka katika kila taifa, kabila, rangi za watu na lugha za dunia. Walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo. Wote walikuwa wamevaa majoho meupe na wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Walipaza sauti kwa nguvu, wakasema “Ushindi ni wa Mungu wetu, anayeketi kwenye kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo.”

11 Wazee na wenye uhai wanne walikuwa pale. Malaika wote walikuwa wamesimama kuwazunguka na kukizunguka kiti cha enzi. Malaika wakainamisha nyuso zao, wakasujudu mpaka chini mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu. 12 Walisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, nguvu na uweza ni vyake Mungu wetu milele na milele. Amina!”

13 Kisha mmoja wa wazee akaniuliza, “Watu hawa waliovaa kanzu nyeupe ni akina nani? Wametoka wapi?”

14 Nikajibu, “Wewe unajua ni akina nani, bwana.”

Mzee akasema, “Hawa ni wale waliokuja kutokana na mateso makuu. Wamefua kanzu zao[e] kwa kutumia damu ya Mwanakondoo, wako safi na ni weupe. 15 Hivyo sasa watu hawa wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Wanamwabudu Mungu mchana na usiku hekaluni mwake. Naye aketiye kwenye kiti cha enzi atawalinda. 16 Hawatasikia njaa tena. Hawatasikia kiu tena. Jua halitawadhuru. Hakuna joto litakalowachoma. 17 Mwanakondoo mbele ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao. Atawaongoza kwenda kwenye chemichemi za maji ya uzima. Na Mungu atafuta kila chozi kutoka kwenye macho yao.”

Muhuri wa Saba

Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa saba, kulikuwa ukimya mbinguni kama nusu saa hivi. Niliwaona malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu. Walipewa tarumbeta saba.

Malaika mwingine akaja na kusimama kwenye madhabahu. Malaika huyu alikuwa na chetezo ya dhahabu. Malaika alipewa ubani mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote wa Mungu. Malaika akaweka sadaka hii juu ya madhabahu ya dhahabu mbele ya kiti cha enzi. Moshi kutoka kwenye ubani ukatoka kwenye mikono ya malaika kwenda kwa Mungu. Moshi ukaenda kwa Mungu ukiwa na Maombi ya watakatifu. Kisha malaika akaijaza chetezo moto kutoka madhabahuni na kuitupa chini duniani, kukatokea miali, radi na ngurumo zingine na tetemeko la ardhi.

Sauti ya Tarumbeta ya Kwanza

Kisha malaika saba wenye tarumbeta walijiandaa kupuliza tarumbeta zao.

Malaika wa kwanza alipuliza tarumbeta yake. Mvua ya mawe na moto uliochanyanyikana na damu vilimwagwa chini duniani. Theluthi moja ya dunia na nyasi zote za kijani na theluthi ya miti vikaungua.

Malaika wa pili alipopuliza tarumbeta yake. Kitu fulani kilichoonekana kama mlima mkubwa unaowaka moto kilitupwa baharini. Na theluthi moja ya bahari ikawa damu. Na theluthi moja ya viumbe walioumbwa wanaokaa baharini wakafa na ya meli theluthi moja zikaharibika.

10 Malaika wa tatu alipopuliza tarumbeta yake. Nyota kubwa, inayowaka kama tochi ikaanguka kutoka mbinguni. Ilianguka kwenye theluthi moja ya mito na chemichemi za maji. 11 Jina la nyota hiyo lilikuwa Uchungu.[f] Na theluthi moja ya maji yote yakawa machungu. Watu wengi wakafa kutokana na kunywa maji haya machungu.

12 Malaika wa nne alipopuliza tarumbeta yake. Theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota vikapigwa. Hivyo theluthi moja yao vikawa giza. Theluthi moja ya mchana na usiku ikakosa mwanga.

13 Nilipokuwa ninatazama, nilimsikia tai aliyekuwa anaruka juu sana angani akisema kwa sauti kuu, “Ole! Ole! Ole kwa wale wanaoishi duniani! Shida kuu zitaanza baada ya sauti za tarumbeta ambazo malaika wengine watatu watapuliza.”

Tarumbeta ya Tano Yaanzisha Kitisho cha Kwanza

Malaika wa tano alipopuliza tarumbeta yake, niliiona nyota ikianguka kutoka angani mpaka duniani. Nyota ilipewa ufunguo wa kufungulia shimo refu sana liendalo kuzimu. Kisha nyota ikafungua shimo refu sana liendalo kuzimu. Moshi ukatoka kwenye shimo kama moto utokao kwenye tanuru kubwa. Jua na anga vikawa giza kwa sababu ya moshi uliotoka kwenye shimo.

Nzige wakatoka kwenye moshi na wakateremka kwenda duniani. Walipewa nguvu ya kuuma kama nge. Waliamriwa kutoharibu nyasi au mimea ya mashambani na mti. Walitakiwa kuwadhuru watu wasio na alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao tu. Hawakupewa mamlaka ya kuwaua lakini kuwatia maumivu kwa muda wa miezi mitano, maumivu kama ambayo mtu huyasikia anapoumwa na nge. Siku hizo watu watatafuta kifo, lakini hawatakiona. Watataka kufa, lakini kifo kitajificha.

Nzige hao walionekana kama farasi walioandaliwa kwa ajili ya mapigano. Vichwani mwao walivaa kitu kilichoonekana kama taji ya dhahabu. Nyuso zao zilionekana kama nyuso za wanadamu. Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake. Meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Vifua vyao vilionekana kama ngao za chuma. Sauti zilizotoka katika mbawa zao zilikuwa kama za farasi wengi na magari ya farasi yaendayo vitani. 10 Walikuwa na mikia kama ya nge. Nguvu ya kuwasababishia wanadamu maumivu kwa miezi mitano ilikuwa kwenye mikia yao. 11 Walikuwa na mtawala, aliyekuwa malaika wa kuzimu. Jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni.[g] Na kwa Kiyunani ni Apolioni.[h]

12 Kitisho cha kwanza kimepita sasa. Bado vinakuja vitisho vingine viwili.

Mlio wa Tarumbeta ya Sita

13 Malaika wa sita alipopuliza tarumbeta yake, nilisikia sauti ikitoka katika pembe[i] zilizo katika pembe[j] nne za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu. 14 Ikamwambia malaika wa sita aliyekuwa na tarumbeta, “Wafungue huru malaika wanne waliofungwa pembezoni mwa mto mkuu Frati.” 15 Malaika hawa wanne walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hii, siku hii, mwezi na mwaka huu. Malaika waliachwa huru ili waue theluthi moja ya watu duniani. 16 Nikasikia kuwa idadi ya askari waliowaendesha farasi walikuwa milioni mia mbili.

17 Katika maono yangu, niliona farasi na waendesha farasi wakiwa juu ya farasi. Walionekana hivi: Walivaa dirii za chuma vifuani mwao zilizokuwa za rangi nyekundu, rangi ya bahari iliyoiva na za rangi ya njano kama baruti. Vichwa vya farasi vilionekana kama vichwa vya simba. Farasi walikuwa wanatoa moto, moshi na baruti katika vinywa vyao. 18 Theluthi ya watu wote duniani walikufa kutokana na mapigo haya matatu yaliyokuwa yanatoka vinywani mwa farasi: moto, moshi na baruti. 19 Nguvu ya farasi ilikuwa kwenye midomo na mikia yao. Mikia yao ilikuwa kama nyoka walio na vichwa vya kuwauma na kuwadhuru watu.

20 Watu wengine duniani hawakufa kwa mapigo haya. Lakini watu hawa bado hawakubadili mioyo yao na kuacha kuabudu vitu walivyovitengeneza kwa mikono yao wenyewe. Hawakuacha kuabudu mapepo na sanamu zilizotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, au kusikia au kutembea. 21 Hawakubadili mioyo yao na kuacha kuua watu wengine au kuacha uchawi, dhambi ya uzinzi na wizi.

Malaika Na Kitabu kidogo

10 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni akiwa amevikwa wingu na upinde wa mvua ulizunguka kichwa chake. Uso wake ulikuwa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Malaika alikuwa ameshika kitabu kidogo kilichofunguliwa. Akaweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na mguu wa kushoto nchi kavu. Alipaza sauti yake kama simba anavyounguruma na sauti za radi saba zikasikika.

Radi saba ziliongea, na nikaanza kuandika. Lakini nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Usiandike ambacho radi saba zinasema. Yaache mambo hayo yawe siri.”

Kisha nikamwona malaika aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu akinyoosha mkono wake kuelekea mbinguni. Malaika akaapa kwa nguvu ya yule aishiye milele na milele. Ndiye aliyeziumba mbingu na vyote vilivyomo ndani yake. Aliumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, na aliumba bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Malaika alisema, “Hakutakuwa kusubiri tena! Katika siku ambazo malaika wa saba atakuwa tayari kupuliza tarumbeta yake, mpango wa siri wa Mungu utakamilika, nao ni Habari Njema ambayo Mungu aliwaambia watumishi wake, manabii.”

Kisha nikasikia tena sauti ile ile kutoka mbinguni. Ikaniambia, “Nenda ukachukue kitabu kilicho wazi mkononi mwa malaika, aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu.”

Hivyo nilimwendea malaika nikamwomba anipe kitabu kidogo. Naye aliniambia, “Chukua kitabu na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako lakini kitakuwa kitamu kama asali mdomoni mwako.” 10 Hivyo nilichukua kitabu kidogo kutoka mkononi mwa malaika na kukila. Mdomoni mwangu kilikuwa na ladha tamu kama asali, lakini baada ya kukila, kilikuwa kichungu tumboni mwangu. 11 Kisha nikaambiwa, “Ni lazima uwatabirie tena watu wa asili tofauti, mataifa, lugha na watawala.”

Mashahidi Wawili

11 Kisha nilipewa fimbo ya kupimia, ndefu kama fimbo ya kutembelea. Nikaambiwa, “Nenda ukalipime hekalu[k] la Mungu na madhabahu na uwahesabu watu wanaoabudu humo. Lakini usipime eneo lililo nje ya hekalu. Liache. Eneo hilo wamepewa watu wasio wa Mungu. Wataonesha nguvu zao juu ya mji mtakatifu kwa miezi 42. Nami nitawapa nguvu mashahidi wangu wawili, watatabiri kwa siku 1,260. Nao watakuwa wamevaa magunia.”

Mashahidi hawa wawili ni mizeituni miwili na vinara viwili vya taa vinavyosimama mbele za Bwana wa dunia. Ikiwa mtu yeyote atajaribu kuwadhuru mashahidi hawa, moto utatoka katika vinywa vyao na kuwaua adui zao. Yeyote atakaye jaribu kuwadhuru atakufa. Mashahidi hawa wana nguvu ya kuzuia mvua isinyeshe katika wakati ambao watakuwa wanatabiri. Pia wana uwezo wa kugeuza maji kuwa damu. Wana uwezo wa kutuma kila aina ya pigo duniani. Wanaweza kufanya hivi kadri wanavyotaka.

Mashahidi wawili watakapomaliza kuutangaza ujumbe wao, mnyama atokaye kuzimu atapigana nao. Atawashinda na kuwaua. Miili ya mashahidi hawa wawili italala kwenye mtaa wa mji mkuu. Mji huu unaitwa Sodoma na Misri. Majina ya mji huu yana maana maalumu. Huu ni mji ambako Bwana aliuawa. Watu kutoka kila asili, kabila, lugha na taifa wataiangalia miili ya mashahidi hawa wawili kwa siku tatu na nusu. Watu watakataa kuwazika. 10 Na Kila aishiye duniani atafurahi kwa sababu mashahidi hawa wawili wamekufa. Watu watafanya sherehe na kupeana zawadi kwa sababu manabii hawa wawili walileta mateso mengi kwa watu waishio duniani.

11 Lakini baada ya siku tatu na nusu, Mungu akawarudishia uhai mashahidi hawa wawili. Wakasimama kwa miguu yao. Na wale waliowaona wakajaa hofu. 12 Kisha mashahidi wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikisema, “Njooni huku juu!” Na wote wawili wakaenda juu mbinguni katika wingu, adui zao wakiangalia wanavyokwenda.

13 Katika wakati huo huo kulitokea tetemeko kuu la ardhi. Sehemu ya kumi ya mji ikateketea, na watu elfu saba wakafa. Wale ambao hawakufa waliogopa sana. Wakampa utukufu Mungu wa mbinguni.

14 Kitisho cha pili kimepita. Kitisho cha tatu kinakuja haraka.

Mlio wa tarumbeta ya Saba

15 Malaika wa saba alipopuliza tarumbeta yake, zikatokea sauti kuu mbinguni, zikasema:

“Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Masihi wake sasa.
    Na atatawala milele na milele.”

16 Kisha wazee 24 wakaanguka chini nyuso zao zikiwa chini wakamwabudu Mungu. Hawa ni wazee ambao wanakaa kwenye viti vyao vya heshima mbele za Mungu. 17 Wazee wakasema:

“Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi.
    Wewe ndiye uliyepo na ambaye daima umekuwepo.
Tunakushukuru kwa sababu umetumia uweza wako mkuu
    na umeanza kutawala.
18 Mataifa walikasirika,
    lakini sasa ni wakati kwa ajili ya hasira yako.
    Sasa ni wakati wa waliokufa kuhukumiwa.
Ni wakati wa kuwapa thawabu watumishi wako, manabii,
    na kuwapa thawabu watu wako watakatifu,
    wakubwa na wadogo, wanaokuheshimu wewe.
Ni wakati wa kuwaangamiza watu wanaoiangamiza dunia!”

19 Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa. Sanduku la Agano likaonekana ndani ya hekalu lake. Kisha kukatokea miali ya radi na miungurumo ya radi, kelele, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International