Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 12:1-21

Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato

(Mk 2:23-28; Lk 6:1-5)

12 Katika wakati huo huo, Yesu alikuwa anasafiri akipita katika mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wafuasi wake walikuwa pamoja naye, na walikuwa na njaa. Hivyo walianza kuchuma nafaka na kula. Mafarisayo walioliona hili, wakamwambia Yesu, “Tazama! Wafuasi wako wanafanya kitu ambacho ni kinyume na sheria yetu kufanya katika siku ya Sabato.”

Yesu akawaambia, “Mmekwisha soma alichofanya Daudi wakati yeye na wale waliokuwa pamoja naye walipokuwa na njaa. Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu. Yeye na wale waliokuwa pamoja naye walikula mkate uliotolewa kwa Mungu. Ilikuwa kinyume cha sheria kwa Daudi au wale waliokuwa pamoja naye kula mkate huo. Makuhani pekee ndio walioruhusiwa kuula. Na mmekwisha soma katika Sheria ya Musa kuwa katika kila Sabato makuhani kwenye Hekalu wanavunja Sheria kwa kufanya kazi Siku ya Sabato. Lakini hawakosei kwa kufanya hivyo. Ninawaambia kuwa kuna kitu hapa ambacho ni kikuu kuliko Hekalu. Maandiko yanasema, ‘Sihitaji dhabihu ya wanyama; Ninataka ninyi muoneshe wema kwa watu.’(A) Hakika hamjui hilo linamaanisha nini. Iwapo mngelielewa, msingewahukumu wale ambao hawajafanya chochote kibaya.

Mwana wa Adamu ni Bwana juu ya siku ya Sabato.”

Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato

(Mk 3:1-6; Lk 6:6-11)

Kutoka hapo Yesu alikwenda katika sinagogi lao. 10 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepooza mkono. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pale walikuwa wanatafuta sababu ya kumshitaki Yesu kwa kutenda kitu kibaya, hivyo walimuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”

11 Yesu akajibu, “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo na akatumbukia shimoni siku ya Sabato, utamsaidia kumtoa yule kondoo katika shimo. 12 Hakika mtu ni bora kuliko kondoo. Hivyo ni sawa kutenda wema siku ya Sabato.”

13 Kisha Yesu akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Unyooshe mkono wako.” Mtu yule akaunyoosha mkono wake, na ukawa mzima tena, kama mkono mwingine. 14 Lakini Mafarisayo waliondoka na wakaweka mipango ya kumuua Yesu.

Yesu ni Mtumishi Aliyechaguliwa na Mungu

15 Yesu alitambua kuwa Mafarisayo walikuwa wanapanga kumuua. Hivyo aliondoka mahali pale na watu wengi walimfuata. Akawaponya wote waliokuwa wagonjwa, 16 lakini aliwaonya wasiwaambie wengine yeye alikuwa nani. 17 Hii ilikuwa ni kuthibitisha kile ambacho nabii Isaya alisema alipozungumza kwa niaba ya Mungu:

18 “Hapa ni mtumishi wangu,
    niliyemchagua.
Ndiye ninayempenda,
    na ninapendezwa naye.
Nitamjaza Roho yangu,
    naye ataleta haki kwa mataifa.
19 Hatabishana au kupiga kelele;
    hakuna atakayesikia sauti yake mitaani.
20 Hatavunja wala kupindisha unyasi.
    Hatazimisha hata mwanga hafifu.
Hatashindwa mpaka ameifanya haki kuwa mshindi.
21     Watu wote watatumaini katika yeye.”(B)

Marko 3

Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato

(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)

Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[a] ili wapate sababu ya kumshitaki. Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”

Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.

Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.

Wengi Wamfuata Yesu

Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake hadi Ziwa Galilaya, na kundi kubwa la watu kutoka Galilaya likawafuata, pamoja na watu kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumea, na katika maeneo yote ng'ambo ya Mto Yordani na yale yanayozunguka Tiro na Sidoni. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. Wote walimjia Yesu kwa sababu walikuwa wamesikia mambo aliyokuwa anafanya.

Kwa sababu ya kundi, aliwaambia wanafunzi wake, kumtayarishia mashua mdogo, ili kwamba wasiweze kumsonga na kumbana. 10 Yesu alikuwa ameponya watu wengi. Hivyo wote wale waliokuwa na magonjwa waliendelea kujisogeza mbele kumwelekea ili wamguse. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona Yesu, walianguka chini mbele yake, na kulia kwa sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” 12 Lakini yeye aliwaamuru kila mara wasimwambie mtu yeyote yeye ni nani.

Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili

(Mt 10:1-4; Lk 6:12-16)

13 Kisha Yesu akapanda juu kwenye vilima na akawaita baadhi ya wanafunzi wake, hasa wale aliowataka wajiunge naye pale. 14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume. Aliwachagua ili waambatane pamoja naye, na kwamba aweze kuwatuma sehemu mbalimbali kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu. 15 Pia aliwapa mamlaka ya kufukuza mashetani toka kwa watu. 16 Yafuatayo ni majina ya mitume kumi na wawili aliowateuwa Yesu:

Simoni ambaye Yesu alimwita Petro,

17 Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake (ambao wote Yesu aliwaita Boanergesi), yaani “wana wa ngurumo yenye radi”,

18 Andrea,

Filipo,

Bartholomayo,

Mathayo,

Thomaso,

Yakobo mwana wa Alfayo,

Thadayo,

Simoni Mzelote

19 na Yuda Iskariote,[b] ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu

(Mt 12:22-32; Lk 11:14-23; 12:10)

20 Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. 21 Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili.

22 Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli[c] ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!”

23 Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? 24 Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. 25 Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. 26 Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake.

27 Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo.

28 Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. 29 Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.”

30 Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.”

Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi

(Mt 12:46-50; Lk 8:19-21)

31 Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. 32 Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako[d] nje wanakusubiri.”

33 Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” 34 Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! 35 Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.”

Luka 6

Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato

(Mt 12:1-8; Mk 2:23-28)

Wakati fulani siku ya Sabato, Yesu alikuwa akitembea kupitia katika baadhi ya mashamba ya nafaka. Wafuasi wake wakachukua masuke, wakayapukusa mikononi mwao na kula nafaka. Baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, “Kwa nini mnafanya hivyo? Ni kinyume na Sheria ya Musa kufanya hivyo siku ya Sabato.”

Yesu akawajibu, “Je, mmesoma kuhusu jambo alilofanya Daudi, wakati yeye na watu wake walipohisi njaa? Daudi alikwenda katika nyumba ya Mungu, akachukua mikate iliyotolewa kwa Mungu na kuila. Na kuwapa wenzake baadhi ya mikate hiyo. Hii ilikuwa kinyume na Sheria ya Musa, inayosema kuwa makuhani pekee ndiyo wanaoruhusiwa kula mikate hiyo.” Kisha Yesu akawaambia Mafarisayo, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato

(Mt 12:9-14; Mk 3:1-6)

Siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na kuwafundisha watu. Katika sinagogi hili alikuwemo mtu aliyepooza mkono wake wa kulia. Walimu wa sheria na Mafarisayo walikuwa wakimvizia Yesu. Walikuwa wanasubiri waone ikiwa ataponya siku hiyo ya Sabato. Walitaka kumwona akifanya jambo lolote lililo kinyume ili wamshitaki. Lakini Yesu alijua walilokuwa wanawaza. Akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyenyuka na simama hapa ambapo kila mtu anaweza kukuona!” Yule mtu akanyenyuka na kusimama pale. Ndipo Yesu akawaambia, “Ninawauliza ninyi, Sheria inaturuhusu tufanye nini siku ya Sabato: kutenda mema au kutenda mabaya? Je, ni halali kuokoa uhai au kuuangamiza?”

10 Yesu akawatazama watu wote kila upande, kisha akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyosha mkono wake, na akaponywa. 11 Mafarisayo na walimu wa sheria wakakasirika sana kiasi cha kutofikiri sawasawa, wakashauriana wao kwa wao wamfanye nini Yesu.

Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili

(Mt 10:1-4; Mk 3:13-19)

12 Siku chache baadaye, Yesu alikwenda mlimani kuomba. Alikaa huko usiku kucha akimwomba Mungu. 13 Asubuhi iliyofuata aliwaita wafuasi wake, akachagua kumi na wawili miongoni mwao na kuwaita Mitume. Nao ni:

14 Simoni (ambaye Yesu alimwita Petro),

Andrea aliyekuwa kaka yake Petro,

Yakobo,

Yohana,

Filipo,

Bartholomayo,

15 Mathayo na

Tomaso,

Yakobo mwana wa Alfayo,

Simoni aliyeitwa Mzelote,

16 Yuda mwana wa Yakobo,

na Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu).

Yesu Afundisha na Kuponya Watu

(Mt 4:23-25; 5:1-12)

17 Yesu na mitume wakatelemka kutoka mlimani. Yesu akasimama mahali tambarare. Kundi kubwa la wafuasi wake lilikuwa pale. Walikuwepo pia watu wengi waliotoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu, na maeneo ya pwani karibu na Tiro na Sidoni. 18 Wote walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya watu waliokuwa wanasumbuliwa na mapepo. 19 Kila mtu alijaribu kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa unamtoka. Yesu aliwaponya wote.

20 Yesu akawatazama wafuasi wake na kusema,

“Heri ninyi mlio maskini.
    Maana Ufalme wa Mungu ni wenu.
21 Heri ninyi mlio na njaa sasa.
    Maana mtashibishwa.
Heri ninyi mnaolia sasa.
    Maana mtafurahi na kucheka.

22 Watu watawachukia kwa sababu ninyi ni wa milki ya Mwana wa Adamu. Watawabagua na watawatukana. Watajisikia vibaya hata kutamka majina yenu. Mambo haya yatakapotukia, mjue kuwa baraka kuu ni zenu. 23 Ndipo mfurahi na kurukaruka kwa furaha, kwa sababu mna thawabu kuu mbinguni. Baba zao waliwafanyia manabii vivyo hivyo.

24 Lakini ole wenu ninyi matajiri,
    kwa kuwa mmekwishapata maisha yenye raha.
25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,
    kwa kuwa mtasikia njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
    kwa kuwa mtalia na kuhuzunika.

26 Ole wenu watu wote wanapowasifu ninyi. Maana mababu zao waliwasifu manabii wa uongo vivyo hivyo daima.

Wapende Adui Zako

(Mt 5:38-48; 7:12a)

27 Lakini ninawaambia ninyi mnaonisikiliza, wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wale wanaowachukia. 28 Mwombeni Mungu awabariki wale wanaowalaani ninyi, waombeeni wale wanaowaonea. 29 Mtu akikupiga shavu moja, mwache akupige na la pili pia. Mtu akichukua koti lako, usimkataze kuchukua shati pia. 30 Mpe kila akuombaye kitu. Mtu yeyote akichukua kitu chako, usitake akurudishie. 31 Watendeeni wengine kama mnavyotaka wao wawatendee ninyi.

32 Je, msifiwe kwa sababu ya kuwapenda wale wanaowapenda ninyi tu? Hapana, hata wenye dhambi, wanawapenda wale wanaowapenda. 33 Je, msifiwe kwa kuwa mnawatendea mema wale wanaowatendea mema ninyi? Hapana, hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo! 34 Je, msifiwe kwa kuwa mnawakopesha watu kwa kutarajia kupata vitu kutoka kwao? Hapana, hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wengine, ili warudishiwe kiasi kile kile!

35 Ninawaambia kuwa wapendeni adui zenu na kuwatendea mema. Wakopesheni watu bila kutarajia kitu kutoka kwao. Mkifanya hivyo, mtapata thawabu kuu. Mtakuwa wana wa Mungu Mkuu Aliye Juu. Ndiyo kwa sababu Mungu ni mwema hata kwa wenye dhambi na wasiomshukuru. 36 Iweni na upendo na huruma, kama Baba yenu alivyo.

Iweni Waangalifu Mnapokosoa Wengine

(Mt 7:1-5)

37 Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa na Mungu. Msiwalaani wengine nanyi hamtalaaniwa. Wasameheni wengine nanyi mtasamehewa. 38 Wapeni wengine vitu, nanyi mtapokea. Mtapewa vingi; kipimo chenye ujazo wa kusukwasukwa na kumwagika. Mungu atawapa ninyi kwa kadri mnavyotoa.”

39 Yesu akawaambia mfano huu, “Je, asiyeona anaweza kumwongoza asiyeona mwenzake? Hapana. Wote wawili watatumbukia shimoni. 40 Wanafunzi si bora kuliko mwalimu wao. Lakini wakiisha kufundishwa na kuhitimu, wanakuwa kama mwalimu wao.

41 Kwa nini unaona kipande kidogo cha vumbi kilicho katika jicho la rafiki yako, lakini hujali kipande cha ubao kilicho ndani ya jicho lako mwenyewe? 42 Unawezaje kumwambia rafiki yako, ‘Hebu nikitoe kipande cha vumbi kilicho katika jicho lako’? Je, huwezi kukiona kipande cha ubao kilicho katika jicho lako mwenyewe? Wewe ni mnafiki. Kwanza kitoe kipande cha ubao katika jicho lako, ndipo utaona vyema na utaweza kukitoa kipande cha vumbi kilicho katika jicho la rafiki yako.

Yale Unayofanya Yanaonesha Jinsi Ulivyo

(Mt 7:17-20; 12:34b-35)

43 Mti mzuri hauzai matunda mabaya. Na mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44 Kila mti unatambuliwa kutokana na aina ya matunda unayozaa. Huwezi kupata tini kwenye vichaka vya miiba. Na huwezi kuchuma zabibu kwenye michongoma! 45 Watu wema wana mambo mazuri katika mioyo yao. Ndiyo sababu hutamka mambo mema. Lakini waovu wana mioyo iliyojaa uovu, na ndiyo sababu hutamka mambo maovu. Mambo wanayotamka watu katika midomo yao, ndiyo yaliyojaa katika mioyo yao.

Aina Mbili za Watu

(Mt 7:24-27)

46 Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana’ lakini hamtendi kama ninavyosema? 47 Nitawaonesha namna walivyo watu wanaokuja kwangu, wale wanaoyasikia na kuyatii mafundisho yangu. 48 Ni kama mtu anayejenga nyumba, huchimba chini sana, na kujenga nyumba yake kwenye mwamba. Mafuriko yanapokuja, huigonga nyumba kwa nguvu, nyumba hiyo haiwezi kuanguka kwa kuwa imejengwa vizuri.

49 Lakini watu wanaoyasikia maneno yangu na hawayatii ni kama mtu anayejenga nyumba bila kutayarisha msingi. Mafuriko yanapokuja, nyumba huanguka chini kwa urahisi na kubomoka kabisa.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International