Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Chronological

Read the Bible in the chronological order in which its stories and events occurred.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 15

Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu

(Mk 7:1-23)

15 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria kutoka Yerusalemu walimjia Yesu na kumwuliza, “Kwa nini wafuasi wako hawatii desturi tulizorithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu walioishi hapo zamani? Wafuasi wako hawanawi mikono kabla ya kula!”

Yesu akajibu, “Na kwa nini mnakataa kutii amri ya Mungu ili muweze kuzifuata desturi zenu? Mungu alisema, ‘Ni lazima umtii baba na mama yako.’(A) Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe.’(B) Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu.’ Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo. Enyi wanafiki! Isaya alikuwa sahihi alipozungumza kwa niaba ya Mungu kuhusu ninyi aliposema:

‘Watu hawa wananiheshimu kwa maneno tu,
    lakini mimi si wa muhimu kwao.
Ibada zao kwangu hazina maana.
    Wanafundisha kanuni za kibinadamu tu.’”(C)

10 Yesu akawaita watu. Akasema, “Sikieni na mwelewe nitakachosema. 11 Si chakula kinachoingia mdomoni kinachomtia mtu unajisi,[a] bali kile kinachomtoka mdomoni mwake.” 12 Kisha wafuasi wakamjia na kumwuliza, “Unajua kuwa Mafarisayo wamekasirika kutokana na yale uliyosema?”

13 Yesu akajibu, “Kila mti ambao haukupandwa na Baba yangu wa mbinguni utang'olewa. 14 Kaeni mbali na Mafarisayo. Wanawaongoza watu, lakini ni sawa na wasiyeona wanaowaongoza wasiyeona wengine. Na kama asiyeona akimwongoza asiyeona mwingine, wote wawili wataangukia shimoni.”

15 Petro akasema, “Tufafanulie yale uliyosema awali kuhusu kile kinachowatia watu najisi.”

16 Yesu akasema, “Bado mna matatizo ya kuelewa? 17 Hakika mnajua kuwa vyakula vyote vinavyoingia kinywani huenda tumboni. Kutoka huko hutoka nje ya mwili. 18 Lakini mambo mabaya ambayo watu wanasema kwa vinywa vyao hutokana na mawazo yao. Na hayo ndiyo yanayoweza kumtia mtu unajisi. 19 Mambo mabaya haya yote huanzia akilini: mawazo maovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, uongo, na matukano. 20 Haya ndiyo mambo yanayowatia watu unajisi. Kula bila kunawa mikono hakuwezi kuwafanya watu wasikubaliwe na Mungu.”

Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi

(Mk 7:24-30)

21 Kutoka pale, Yesu alikwenda maeneo ya Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke Mkanaani kutoka eneo hilo akatokea na kuanza kupaza sauti, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie! Binti yangu ana pepo ndani yake, na anateseka sana.”

23 Lakini Yesu hakumjibu. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea Yesu na kumwambia, “Mwambie aondoke, anaendelea kupaza sauti na hatatuacha.”

24 Yesu akajibu, “Mungu alinituma niwasaidie kondoo wa Mungu waliopotea, watu wa Israeli.”[b]

25 Ndipo mwanamke alikuja mahali alipokuwa Yesu na kuinama mbele yake. Akasema, “Bwana, nisaidie!”

26 Akamjibu kwa kumwambia, “Si sahihi kuwapa mbwa mkate wa watoto.”

27 Mwanamke akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula vipande vya chakula vinavyoanguka kutoka kwenye meza za mabwana zao.”

28 Kisha Yesu akamjibu, “Mwanamke, una imani kuu! Utapata ulichoomba.” Wakati huo huo binti wa yule mwanamke akaponywa.

Yesu Awaponya Watu Wengi

29 Kisha Yesu akatoka pale na kwenda pwani ya Ziwa Galilaya. Alipanda vilima na akaketi chini.

30 Kundi kubwa la watu likamwendea. Walileta watu wengine wengi waliokuwa wagonjwa na kuwaweka mbele yake. Walikuwepo watu wasioweza kutembea, wasiyeona, walemavu wa miguu, wasiyesikia na wengine wengi. 31 Watu walishangaa walipoona kuwa waliokuwa wasiyesema walianza kusema, walemavu wa miguu waliponywa, waliokuwa hawawezi kutembea waliweza kutembea, wasiyeona waliweza kuona. Kila mtu alimshukuru Mungu wa Israeli kwa hili.

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000

(Mk 8:1-10)

32 Kisha Yesu akawaita wafuasi wake na kuwaambia, “Ninawaonea huruma watu hawa. Wamekuwa pamoja nami kwa siku tatu, na sasa hawana chakula. Sitaki niwaache waende wakiwa na njaa. Wanaweza kuzimia njiani wanaporudi nyumbani.”

33 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha watu wote hawa? Tuko nyikani mbali ni miji.”

34 Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”

Wakamjibu, “Tuna mikate saba na samaki wadogo wachache.”

35 Yesu akawaambia watu waketi chini. 36 Akaichukua mikate saba na samaki. Akamshukuru Mungu kwa sababu ya chakula. Akaigawa vipande vipande, akawapa wafuasi wake na wafuasi wakawapa watu chakula. 37 Watu wote walikula mpaka wakashiba. Baada ya hili, wafuasi walijaza vikapu saba kwa vipande vya chakula vilivyosalia ambavyo havikuliwa. 38 Walikuwepo wanaume 4,000 pale waliokula. Walikuwepo pia wanawake na watoto. 39 Baada ya wote kula, Yesu akawaambia watu wanaweza kwenda nyumbani. Alipanda mashua na kwenda eneo la Magadani.

Marko 7

Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu

(Mt 15:1-20)

Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Sheria waliokuja kutoka Yerusalemu walikusanyika mbele zake. Hao wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula chao kwa mikono michafu (yaani bila kuosha mikono yao). Kwani Mafarisayo na Wayahudi wengineo wote hawawezi kula isipokuwa wameosha mikono yao kwa njia maalumu, kulingana na desturi ya wazee. Na wanaporudi kutoka sokoni, hawali chakula kwanza mpaka wamenawa. Na zipo desturi nyingi wanazozishika, kama vile kuosha vikombe, magudulia na mitungi ya shaba.[a]

Kwa hiyo Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, badala yake wanakula chakula chao kwa mikono isiyo safi?”

Yesu akawaambia, “Isaya alikuwa sahihi alipotoa unabii juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa:

‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
    lakini mioyo yao iko mbali nami.
Ibada wanayonitolea haifai,
    kwa sababu wanawafundisha watu amri
    zilizotungwa na wanadamu kana kwamba ndizo itikadi zao.’(A)

Mmezipuuza amri za Mungu, na mnashikilia desturi za binadamu.”

Yesu akawaambia, “Ninyi ni wazuri katika kuzikataa amri za Mungu ili kuanzisha desturi yenu. 10 Kwa mfano Musa alisema, ‘Mheshimu baba yako na mama yako,’(B) na yule mtu atakayesema maneno mabaya juu ya ‘mama au baba yake itampasa auwawe.’(C) 11 Lakini ikiwa mtu atamwambia baba au mama yake, ‘Nilikuwa na kitu ambacho ningekupa kikusaidie, lakini nimeahidi kukitoa wakfu kwa Mungu, nacho sasa ni kurbani.[b] 12 Kisha, anasema, hivyo hawezi kufanya kitu chochote kwa ajili ya kumsaidia baba au mama yake. 13 Kwa hiyo unalifanya neno la Mungu kuwa batili kwa desturi mlizozirithishana. Na mnafanya mambo mengi mengine yanayofanana na hayo.”

14 Yesu akaliita lile kundi kwake na kuwaambia, “Kila mmoja anisikilize na kunielewa. 15 Hakuna kitu kilicho nje ya mtu kinachoweza kumchafua kwa kumwingia. Lakini vitu vinavyotoka ndani ya mtu ndivyo vinavyomchafua.” 16 [c]

17 Na alipoliacha lile kundi na kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza juu ya fumbo lile. 18 Na akawaambia, “Hata nanyi hamuelewi pia? Je, hamuelewi ya kuwa hakuna kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumchafua mtu? 19 Kwa sababu hakiingii ndani ya moyo wake bali kinaenda tumboni mwake na kasha kinatoka na kwenda chooni.” Kwa kuyasema hayo alivifanya vyakula vyote kuwa safi.

20 Na Yesu akasema, “Ni kile kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomchafua. 21 Kwani mambo hayo yote mabaya hutoka ndani ya moyo wa mwanadamu; yaani mawazo mabaya na uasherati, wizi, mauaji, 22 zinaa, ulafi, kufanya mabaya kwa watu, udanganyifu, kufanya uhuni, wivu, kutukana, kujivuna, na ujinga. 23 Mambo haya yote yanatoka ndani ya mtu nayo ndiyo yanayomfanya asikubalike kwa Mungu.”

Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi

(Mt 15:21-28)

24 Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. 26 Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake.

27 Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.”

28 Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.”

29 Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.”

30 Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka.

Yesu Amponya Asiyesikia

31 Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. 32 Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya.

33 Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “Efatha” yaani, “Funguka!” 35 Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri.

36 Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. 37 Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International