Book of Common Prayer
Kuhesabiwa Haki na Mungu
5 Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya imani.[a] Hivyo sote[b] tuna amani pamoja na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 2 Kupitia imani yetu, Kristo ametufungulia mlango kuingia katika neema ya Mungu, tunayoifurahia sasa. Na tunashangilia sana kwa sababu ya tumaini tulilonalo la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Na tunafurahia matatizo tunayoyapitia. Kwa nini? Kwa sababu tunajua kuwa mateso hutufundisha kuwa jasiri kipindi kigumu. 4 Na ujasiri huu ni uthibitisho kuwa tuko imara. Na uthibitisho huu unatupa tumaini. 5 Na tukiwa na tumaini hili, hatutakata tamaa kamwe. Tunajua hili kwa sababu Mungu ameumimina upendo wake na kuijaza mioyo yetu kupitia Roho Mtakatifu aliyetupa.
6 Yote haya ni kweli kutokana na aliyoyafanya Kristo. Wakati sahihi ulipotimia, tukiwa hatuwezi kujisaidia wenyewe na tusioonyesha heshima yoyote kwa Mungu, yeye Kristo, alikufa kwa ajili yetu. 7 Ni watu wachache walio tayari kufa ili kuokoa maisha ya mtu mwingine, hata kama mtu huyo ni mwema. Mtu anaweza kuwa radhi kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema sana. 8 Lakini Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa bado ni wenye dhambi, na kwa hili Mungu akatuonyesha jinsi anavyotupenda sana.
9 Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Kristo. Hivyo kwa njia ya Kristo hakika tutaokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. 10 Nina maana kuwa tulipokuwa bado adui wa Mungu, Yeye alifanya urafiki nasi kwa njia ya kifo cha Mwanaye. Kutokana na ukweli kwamba sasa tumekuwa marafiki wa Mungu, basi tunaweza kupata uhakika zaidi kwamba Baba atatuokoa kupitia uhai wa Mwanaye. 11 Na si kuokolewa tu, bali pia, hata sasa tunafurahi kwa yale ambayo Mungu ametutendea kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa sababu ya Yesu sisi ni marafiki wa Mungu sasa.
Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake
(Mk 10:32-34; Lk 18:31-34)
17 Yesu alikuwa anakwenda Yerusalemu akiwa na wafuasi wake kumi na wawili. Walipokuwa wakitembea, aliwakusanya pamoja wafuasi hao na kuzungumza nao kwa faragha. Akawaambia, 18 “Tunakwenda Yerusalemu. Mwana wa Adamu atatolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, nao watasema ni lazima auawe. 19 Watamkabidhi wa wageni, watakaomcheka na kumpiga kwa mijeledi, kisha watamwua kwenye msalaba. Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuliwa kutoka kwa wafu.”
Mama Ataka Upendeleo Maalum kwa Wanaye
(Mk 10:35-45)
20 Ndipo mke wa Zebedayo akamjia Yesu akiwa na wanaye. Akainama mbele ya Yesu na akamwomba amtendee kitu.
21 Yesu akasema, “Unataka nini?”
Akasema, “Niahidi kuwa mmoja wa wanangu atakaa upande wa kuume na mwingine wa kushoto katika ufalme wako.”
22 Hivyo Yesu akawaambia wana wa Zebedayo, “Hamwelewi mnachokiomba. Mnaweza kukinywea kikombe[a] ambacho ni lazima nikinywee?”
Wana wa Zebedayo wakajibu, “Ndiyo tunaweza!”
23 Yesu akawaambia, “Ni kweli kuwa mtakinywea kikombe nitakachokinywea. Lakini si mimi wa kuwaambia ni nani ataketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto. Baba yangu amekwisha amua ni nani ataketi kuume au kushoto kwangu. Amekwisha andaa nafasi hizo kwa ajili yao.”
24 Wafuasi wengine kumi waliposikia hili walikasirika kwa ajili ya wale ndugu wawili. 25 Hivyo Yesu akawaita pamoja, akawaambia, “Mnajua kuwa watawala wa watu wasio Wayahudi[b] wanapenda kuonesha nguvu yao kwa watu. Na viongozi wao muhimu wanapenda kutumia mamlaka yao yote juu ya watu. 26 Lakini isiwe hivyo miongoni mwenu. Kila anayetaka kuwa kiongozi wenu lazima awe mtumishi wenu. 27 Kila anayetaka kuwa wa kwanza ni lazima awatumikie ninyi nyote kama mtumwa. 28 Fanyeni kama nilivyofanya: Mwana wa Adamu hakuja ili atumikiwe na watu. Alikuja ili awatumikie wengine na kutoa maisha yake ili kuwaokoa watu wengi.”
© 2017 Bible League International