Book of Common Prayer
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu.[a]
Mungu alinichagua niwe mtume na akanipa kazi ya kuhubiri Habari Njema yake. 2 Tangu zamani, kwa vinywa vya manabii katika Maandiko Matakatifu, Mungu aliahidi kwamba angewaletea Habari Njema watu wake. 3 Habari Njema hii inahusu Mwana wa Mungu, ambaye kama mwanadamu, alizaliwa katika ukoo wa Mfalme Daudi. 4 Na alipofufuliwa na Roho Matakatifu[b] kutoka kwa wafu, alipewa mamlaka kamili ya kutawala kama Mwana wa Mungu. Ni Yesu Kristo, Bwana wetu.
5 Kupitia kwa Yesu, Mungu amenionyesha wema wake. Na amenipa mamlaka ya kuwaendea watu wa mataifa yote na kuwaongoza kumwamini na kumtii yeye. Kazi yote hii ni kwa ajili yake. 6 Nanyi pia ni miongoni mwa waliochaguliwa na Mungu ili mmilikiwe na Yesu Kristo.
7 Waraka huu ni kwa ajili yenu ninyi nyote mlio huko Rumi. Kwani Mungu anawapenda na amewachagua kuwa watu wake watakatifu.
Ninamwomba Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo, wawape ninyi neema na amani.
Maombi ya Shukrani
8 Kwanza, ninamshukuru Mungu wangu kupitia Yesu Kristo kwa ajili yenu ninyi nyote. Ninamshukuru yeye kwa sababu kila mahali ulimwenguni watu wanazungumza kuhusu imani yenu kuu. 9-10 Kila wakati ninapoomba, ninawakumbuka ninyi daima. Mungu anajua kuwa hii ni kweli. Yeye ndiye ninayemtumikia kwa moyo wangu wote nikiwaambia watu Habari Njema kuhusu Mwanaye. Hivyo ninaendelea kuomba kwamba mwishowe Mungu atanifungulia njia ili niweze kuja kwenu. 11 Ninataka sana niwaone na niwape zawadi ya kiroho ili kuimarisha imani yenu. 12 Ninamaanisha kuwa ninataka tusaidiane sisi kwa sisi katika imani tuliyo nayo. Imani yenu itanisaidia mimi, na imani yangu itawasaidia ninyi.
13 Kaka zangu na dada zangu, ninataka mjue kwamba nimepanga mara nyingi kuja kwenu, lakini jambo fulani hutokea na kubadili mipango yangu kila ninapopanga kuja. Juu ya kazi yangu miongoni mwenu, ningependa kuona matokeo yale yale mazuri yakitokea ya kazi yangu miongoni mwa watu wengine wasio Wayahudi.
14 Imenilazimu kuwatumikia watu wote; waliostaarabika na wasiostaarabika,[c] walioelimika na wasio na elimu. 15 Ndiyo sababu ninataka sana kuzihubiri Habari Njema kwenu ninyi pia mlio huko Rumi.
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mk 9:14-29; Lk 9:37-43a)
14 Yesu na wafuasi walirudi kwa watu. Mtu mmoja akamjia Yesu na kuinama mbele zake. 15 Akasema, “Bwana, umwonee huruma mwanangu. Anateswa sana na kifafa alichonacho. Anaangukia kwenye moto au maji mara kwa mara. 16 Nilimleta kwa wafuasi wako, lakini wameshindwa kumponya.”
17 Yesu akajibu, “Ninyi watu mnaoishi katika nyakati hizi cha kizazi kisicho na imani. Maisha yenu ni mabaya sana! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kijana hapa.” 18 Yesu akamwamuru pepo aliye ndani ya kijana, na pepo akamtoka na yule kijana akapona.
19 Kisha wafuasi wakamjia Yesu wakiwa peke yao. Wakasema, “Tulijaribu kumtoa pepo kwa kijana, lakini tulishindwa. Kwa nini tulishindwa kumtoa pepo?”
20 Yesu akajibu, “Mlishindwa kumtoa pepo kwa sababu imani yenu ni ndogo sana. Niaminini ninapowaambia, imani yenu ikiwa na ukubwa wa mbegu ya haradali mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ondoka hapa na uende kule,’ nao utaondoka. Nanyi mtaweza kufanya jambo lolote.” 21 [a]
© 2017 Bible League International