Book of Common Prayer
Utunzeni Uhuru Wenu
5 Sasa tuko huru, kwa sababu Kristo alituweka huru ili tuweze kuishi tukiufurahia uhuru huo. Hivyo muwe imara katika uhuru huo. Msimruhusu mtu yeyote awaingize utumwani tena. 2 Sikilizeni! Mimi Paulo nawaambia kwamba ikiwa mtakubali kutahiriwa, basi Kristo hatakuwa na manufaa kwenu. 3 Tena, ninamwonya kila mtu atakayeruhusu atahiriwe, kwamba akifanya hivyo itampasa aifuate sheria yote. 4 Ikiwa utajaribu kufanyika mwenye haki mbele za Mungu kwa njia ya sheria, maisha yako na Kristo yamepotea, kwani umeiacha neema ya Mungu. 5 Ninasema hivi kwa sababu tumaini letu la kufanywa wenye haki mbele za Mungu huja kwa imani. Na kwa nguvu ya Roho kwa njia ya imani, tunangoja kwa utulivu na kwa matumaini yenye ujasiri hukumu ya Mungu inayotuweka huru. 6 Mtu anapokuwa wa Kristo Yesu, vyote kutahiriwa ama kutotahiriwa havina nguvu ya kuleta manufaa yoyote. Lakini kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu imani inatenda kazi kupitia upendo.
7 Mlikuwa mnapiga mbio vizuri sana. Ni nani aliyewafanya mkaacha kuitii kweli? 8 Hakika hakuwa yule aliyewachagua. 9 Mjihadhari! “Chachu ndogo tu hufanya mkate wote mzima uumuke.”[a] 10 Nimeridhika moyoni mbele za Bwana kuwa hamtafikiri vinginevyo. Mtu yule anayewasumbua atahukumiwa hata angekuwa nani?
11 Kaka na dada zangu, sifundishi kuwa ni lazima mwanaume atahiriwe. Kama nitaendelea kuwafundisha wanaume watahiriwe, kwa nini watu bado wanaendelea kunitesa? Ikiwa bado nafundisha tohara, basi ujumbe wangu kuhusu msalaba hautaendelea kuwa tatizo. 12 Natamani watu hao wanaowasumbua wangeongeza na kuhasi[b] juu ya tohara yao.
13 Ndugu na dada zangu, Mungu aliwaita ili muwe huru. Lakini msiutumie uhuru wenu kama udhuru wa kutimiza yale yote mnayoyapenda, badala yake, msaidiane ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Sheria yote imepewa muhtasari katika amri hii moja tu, “Mpende jirani yako[c] kama unavyojipenda mwenyewe.”(A) 15 Ikiwa mtaendelea kuumizana na kuraruana, muwe waangalifu, vinginevyo mtaangamizana ninyi kwa ninyi.
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-13; Lk 12:54-56)
16 Mafarisayo na Masadukayo walimjia Yesu. Walitaka kumjaribu, kwa hiyo wakamwomba awaoneshe muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu.
2 Yesu akawajibu, “Ninyi watu mnapoona jua limezama, mnajua hali ya hewa itakavyokuwa. Anga ikiwa nyekundu, mnasema tutakuwa na hali ya hewa nzuri. 3 Na asubuhi, ikiwa anga ni nyeusi na nyekundu, mnasema mvua itanyesha. Hizi ni ishara za hali ya hewa. Mnaziona ishara hizi angani na mnajua zinamaanisha nini. Kwa namna hiyo hiyo, mnaona mambo yanayotokea sasa. Hizi ni ishara pia, lakini hamwelewi maana yake. 4 Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu na si waaminifu kwa Mungu. Ndiyo sababu kabla ya kuamini mnataka kuona muujiza. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia kitu cho chote. Yona[a] ndiyo ishara pekee mtakayopewa.” Kisha Yesu akaondoka mahali pale.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mk 8:14-21)
5 Yesu na wafuasi wake wakasafiri kwa kukatisha ziwa. Lakini wafuasi wakasahau kubeba mikate. 6 Yesu akawaambia, “Mwe waangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
7 Wafuasi wakajadiliana maana ya hili. Wakasema, “Amesema hivi kwa sababu tumesahau kubeba mikate?”
8 Yesu alipotambua kuwa wanajadiliana hili, akawauliza, “Kwa nini mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Imani yenu ni ndogo. 9 Bado hamwelewi? Mnakumbuka mikate mitano waliyokula watu 5,000 na vikapu vingi mlivyojaza mikate iliyosalia? 10 Na mnakumbuka mikate saba waliyokula watu 4,000 na vikapu vingi mlivyojaza wakati ule? 11 Hivyo inakuwaje mnadhani kuwa mimi ninajali sana kuhusu mikate? Ninawaambia muwe waangalifu na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
12 Ndipo wafuasi wakaelewa Yesu alimaanisha nini. Hakuwa akiwaambia wajilinde na chachu inayotumika katika mikate bali wajilinde na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
© 2017 Bible League International