Add parallel Print Page Options

Yakobo na Yohana Waomba Kutawala Pamoja na Yesu

(Mt 20:20-28)

35 Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu, wakamwambia, “Mwalimu tunataka utufanyie kile tunachokuomba.”

36 Yesu akawaambia, “Ni kitu gani mnachotaka niwafanyie?”

37 Nao wakamwambia, “Uturuhusu tuketi pamoja nawe katika utukufu wako, mmoja wetu aketi kulia kwako na mwingine kushoto kwako.”

38 Yesu akawaambia, “Hamjui mnachokiomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninachokinywea[a] mimi? Au mnaweza kubatizwa ubatizo ninaobatizwa?”

39 Wakamwambia, “Tunaweza.”

Kisha Yesu akawaambia, “Mtakinywa kikombe cha mateso ninachokunywa mimi, na mtabatizwa ubatizo[b] ninaobatizwa mimi. 40 Lakini kuhusu kuketi kulia kwangu ama kushoto kwangu siyo mamlaka yangu kusema. Mungu ameandaa nafasi hizo kwa ajili ya wale aliowateuwa.”

41 Wale wanafunzi kumi wengine walipoyasikia maombi haya, waliwakasirikia Yakobo na Yohana. 42 Na Yesu akawaita wale wanafunzi kumi na kusema, “Mnajua kuwa miongoni mwa mataifa watawala huwa na mamlaka makubwa juu ya watu, na viongozi wenye nguvu huwakandamiza watu wao. 43 Haipaswi kuwa hivyo miongoni mwenu. Kwani yeyote atakaye kuwa mkuu miongoni mwenu basi na awe mtumishi wenu. 44 Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima akubali kuwa mtumwa wenu wote. 45 Kwani hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa bali alikuja kuwatumikia wengine na kuyatoa maisha yake ili kuwaweka huru wengi.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 10:38 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.
  2. 10:39 ubatizo Neno hili ubatizo lina maana ya kutumbukiza majini, lakini pia lina maana maalumu hapa, ambayo ni kufunikwa, kuwekwa ndani ya ama kufunikwa au kuzikwa mwili wote.