Book of Common Prayer
Kushindwa kwa Shetani
7 Miaka elfu moja itakapokwisha, Shetani ataachiwa huru kutoka kwenye gereza lake. 8 Atatoka na kwenda kuwadanganya mataifa katika dunia yote, mataifa yajulikanayo kama Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya watu kwa ajili ya vita. Kutakuwa watu wengi wasiohesabika kama mchanga katika ufukwe wa bahari.
9 Nililiona jeshi la Shetani likitembea na kujikusanya ili kuizingira kambi ya watu wa Mungu na mji anaoupenda Mungu. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuliteketeza jeshi la Shetani. 10 Na Shetani, yule aliyewadanganya watu hawa, alitupwa kwenye ziwa la moto pamoja na mnyama na nabii wa uongo. Watateseka kwa maumivu usiku na mchana milele na milele.
Watu wa Dunia Wahukumiwa
11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe. Nikamwona aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha enzi. Dunia na anga vikamkimbia na kutoweka. 12 Na nikaona wale waliokufa, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi na vitabu vilifunguliwa. Na kitabu cha uzima kilifunguliwa pia. Watu walihukumiwa kwa yale waliyotenda, kama yalivyoandikwa katika vitabu.
13 Bahari ikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Mauti na kuzimu zikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Watu wote hawa walihukumiwa kutokana na matendo yao. 14 Mauti na kuzimu vilitupwa kwenye ziwa la moto. Ziwa hili la moto ni mauti ya pili. 15 Na yeyote ambaye jina lake halikuonekana limeandikwa kwenye kitabu cha uzima alitupwa kwenye ziwa la moto.
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mk 9:2-13; Lk 9:28-36)
17 Siku sita baadaye, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo na akapanda nao kwenye mlima mrefu. Walikuwa peke yao huko. 2 Wafuasi wake hawa walipokuwa wakimwangalia, Yesu alibadilika. Uso wake ukawa angavu kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. 3 Ndipo wanaume wawili waliozungumza naye wakaonekana wakiwa pamoja naye. Walikuwa Musa na Eliya.
4 Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tuko hapa. Ukitaka, nitajenga vibanda vitatu,[a] kimoja kwa ajili ya heshima yako, kingine kwa ajili ya heshima ya Musa na kingine kwa ajili ya heshima ya Eliya.”
5 Petro alipokuwa akizungumza, wingu jeupe liliwafunika. Sauti ikatoka katika wingu na akasema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda, ninafurahishwa naye. Mtiini yeye!”
6 Wafuasi waliokuwa na Yesu walipoisikia sauti hii waliogopa sana na wakaanguka chini. 7 Lakini Yesu akawaendea na kuwagusa. Akasema, “simameni, msiogope.” 8 Wafuasi wakatazama juu, wakaona kuwa Yesu yuko peke yake.
9 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru akisema: “Msimwambie mtu yeyote yale mliyoyaona mlimani. Subirini mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Ndipo mtaweza kuwaambia watu juu ya kile mlichokiona.”
10 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Kwa nini walimu wa sheria wanasema ni lazima Eliya aje[b] kabla ya Masihi kuja?”
11 Yesu akajibu, “Wako sahihi kusema ni lazima Eliya aje, na ni kweli kuwa Eliya ataweka mambo yote kama yanavyopaswa kuwa. 12 Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja. Watu hawakumjua yeye ni nani, na walimtendea vibaya, wakafanya kama walivyotaka. Ndivyo itakavyokuwa hata kwa Mwana wa Adamu. Watu hao punde tu watamletea mateso Mwana wa Adamu.” 13 Ndipo wafuasi wakaelewa kuwa Yesu aliposema kuhusu Eliya, alikuwa anazungumza juu ya Yohana Mbatizaji.
© 2017 Bible League International