Book of Common Prayer
Babeli Inaangamizwa
18 Kisha nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Malaika huyu alikuwa na nguvu kuu. Utukufu wa malaika ukaing'arisha dunia. 2 Malaika akapaza sauti akasema:
“Ameteketezwa!
Mji mkuu Babeli umeteketezwa!
Umekuwa nyumba ya mapepo.
Mji ule umekuwa najisi.
Mji uliojaa kila aina ya ndege najisi.
Ni mahali ambapo kila mnyama najisi
na anayechukiwa anaishi.
3 Watu wote wa dunia wamekunywa mvinyo
wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.
Watawala wa dunia walizini pamoja naye,
na wafanya biashara wa ulimwengu walitajirika
kutokana na utajiri wa anasa zake.”
4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:
“Enyi watu wangu, tokeni katika mji huo,
ili msishiriki katika dhambi zake.
Ili msiteseke kwa adhabu yoyote kuu atakayoipata.
5 Dhambi za mji huo zimerundikana na kufika mbinguni.
Mungu hajasahau makosa aliyotenda.
6 Upeni mji huo sawasawa na ulivyowapa wengine.
Mlipeni mara mbili kadiri ya alivyotenda.
Mwandalieni mvinyo ulio na nguvu mara mbili
ya mvinyo aliowaandalia wengine.
7 Alijipa utukufu mwingi na kuishi kitajiri.
Mpeni mateso mengi na huzuni nyingi.
Kama vile utukufu na starehe aliyoifurahia.
Hujisemea mwenyewe, ‘Mimi ni malkia nikaaye kwenye kiti changu cha enzi.
Mimi si mjane;
Sitakuwa na huzuni.’
8 Hivyo katika siku moja atateseka
kwa njaa kuu, maombolezo na kifo.
Atateketezwa kwa moto,
kwa sababu Bwana Mungu anayemhukumu ni mwenye nguvu.”
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mk 7:1-23)
15 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria kutoka Yerusalemu walimjia Yesu na kumwuliza, 2 “Kwa nini wafuasi wako hawatii desturi tulizorithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu walioishi hapo zamani? Wafuasi wako hawanawi mikono kabla ya kula!”
3 Yesu akajibu, “Na kwa nini mnakataa kutii amri ya Mungu ili muweze kuzifuata desturi zenu? 4 Mungu alisema, ‘Ni lazima umtii baba na mama yako.’(A) Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe.’(B) 5 Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu.’ 6 Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo. 7 Enyi wanafiki! Isaya alikuwa sahihi alipozungumza kwa niaba ya Mungu kuhusu ninyi aliposema:
8 ‘Watu hawa wananiheshimu kwa maneno tu,
lakini mimi si wa muhimu kwao.
9 Ibada zao kwangu hazina maana.
Wanafundisha kanuni za kibinadamu tu.’”(C)
10 Yesu akawaita watu. Akasema, “Sikieni na mwelewe nitakachosema. 11 Si chakula kinachoingia mdomoni kinachomtia mtu unajisi,[a] bali kile kinachomtoka mdomoni mwake.” 12 Kisha wafuasi wakamjia na kumwuliza, “Unajua kuwa Mafarisayo wamekasirika kutokana na yale uliyosema?”
13 Yesu akajibu, “Kila mti ambao haukupandwa na Baba yangu wa mbinguni utang'olewa. 14 Kaeni mbali na Mafarisayo. Wanawaongoza watu, lakini ni sawa na wasiyeona wanaowaongoza wasiyeona wengine. Na kama asiyeona akimwongoza asiyeona mwingine, wote wawili wataangukia shimoni.”
15 Petro akasema, “Tufafanulie yale uliyosema awali kuhusu kile kinachowatia watu najisi.”
16 Yesu akasema, “Bado mna matatizo ya kuelewa? 17 Hakika mnajua kuwa vyakula vyote vinavyoingia kinywani huenda tumboni. Kutoka huko hutoka nje ya mwili. 18 Lakini mambo mabaya ambayo watu wanasema kwa vinywa vyao hutokana na mawazo yao. Na hayo ndiyo yanayoweza kumtia mtu unajisi. 19 Mambo mabaya haya yote huanzia akilini: mawazo maovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, uongo, na matukano. 20 Haya ndiyo mambo yanayowatia watu unajisi. Kula bila kunawa mikono hakuwezi kuwafanya watu wasikubaliwe na Mungu.”
© 2017 Bible League International