Book of Common Prayer
Watu Wamsifu Mungu Mbinguni
19 Baada ya hili nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu mbinguni. Walikuwa wakisema:
“Haleluya![a]
Ushindi, utukufu na nguvu ni vyake Mungu wetu.
2 Hukumu zake ni za kweli na za haki.
Mungu wetu amemwadhibu kahaba.
Ndiye aliyeiharibu dunia kwa uzinzi wake.
Mungu amemwadhibu kahaba kulipa kisasi cha vifo vya watumishi wake.”
3 Pia, watu hawa walisema:
“Haleluya!
Anaungua na moshi wake utasimama milele na milele.”
4 Ndipo wazee ishirini na nne na viumbe wenye uhai wanne wakaanguka chini kusujudu wakamwabudu Mungu, akaaye kwenye kiti cha enzi. Wakasema:
“Amina! Haleluya!”
5 Sauti ikatoka kwenye kiti cha enzi na kusema:
“Msifuni Mungu wetu,
ninyi nyote mnaomtumikia!
Msifuni Mungu wetu,
ninyi nyote mlio wadogo na wakubwa mnaomheshimu!”
6 Kisha nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu. Kilikuwa na kelele kama mawimbi ya bahari au radi. Watu walikuwa wakisema:
“Haleluya!
Bwana Mungu wetu anatawala.
Ndiye Mwenye Nguvu, Mungu Mwenyezi.
7 Tushangilie na kufurahi na
kumpa Mungu utukufu!
Mpeni Mungu utukufu, kwa sababu arusi ya Mwanakondoo imewadia.
Na bibi arusi wa Mwanakondoo amekwisha jiandaa.
8 Nguo ya kitani safi ilitolewa kwa bibi arusi ili avae.
Kitani ilikuwa safi na angavu.”
(Kitani safi inamaanisha mambo mazuri ambayo watakatifu wa Mungu waliyatenda.)
9 Kisha malaika akaniambia, “Andika hili: Heri ni kwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!” Kisha malaika akasema, “Haya ni maneno ya Mungu mwenyewe.”
10 Kisha nikaanguka chini mbele miguuni pa malaika ili nimwabudu. Lakini malaika akaniambia, “Usiniabudu! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako na dada zako walio na ushuhuda kuhusu Yesu Kristo. Hivyo mwabudu Mungu! Kwa sababu ushuhuda kuhusu Yesu ndiyo roho ya unabii.”
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-13; Lk 12:54-56)
16 Mafarisayo na Masadukayo walimjia Yesu. Walitaka kumjaribu, kwa hiyo wakamwomba awaoneshe muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu.
2 Yesu akawajibu, “Ninyi watu mnapoona jua limezama, mnajua hali ya hewa itakavyokuwa. Anga ikiwa nyekundu, mnasema tutakuwa na hali ya hewa nzuri. 3 Na asubuhi, ikiwa anga ni nyeusi na nyekundu, mnasema mvua itanyesha. Hizi ni ishara za hali ya hewa. Mnaziona ishara hizi angani na mnajua zinamaanisha nini. Kwa namna hiyo hiyo, mnaona mambo yanayotokea sasa. Hizi ni ishara pia, lakini hamwelewi maana yake. 4 Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu na si waaminifu kwa Mungu. Ndiyo sababu kabla ya kuamini mnataka kuona muujiza. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia kitu cho chote. Yona[a] ndiyo ishara pekee mtakayopewa.” Kisha Yesu akaondoka mahali pale.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mk 8:14-21)
5 Yesu na wafuasi wake wakasafiri kwa kukatisha ziwa. Lakini wafuasi wakasahau kubeba mikate. 6 Yesu akawaambia, “Mwe waangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
7 Wafuasi wakajadiliana maana ya hili. Wakasema, “Amesema hivi kwa sababu tumesahau kubeba mikate?”
8 Yesu alipotambua kuwa wanajadiliana hili, akawauliza, “Kwa nini mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Imani yenu ni ndogo. 9 Bado hamwelewi? Mnakumbuka mikate mitano waliyokula watu 5,000 na vikapu vingi mlivyojaza mikate iliyosalia? 10 Na mnakumbuka mikate saba waliyokula watu 4,000 na vikapu vingi mlivyojaza wakati ule? 11 Hivyo inakuwaje mnadhani kuwa mimi ninajali sana kuhusu mikate? Ninawaambia muwe waangalifu na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
12 Ndipo wafuasi wakaelewa Yesu alimaanisha nini. Hakuwa akiwaambia wajilinde na chachu inayotumika katika mikate bali wajilinde na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
© 2017 Bible League International