Book of Common Prayer
11 Hivyo hebu na tujitahidi tuwezavyo kuingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu. Tunapaswa kujitahidi ili asiwepo miongoni mwetu atakayepotea kwa kufuata mfano wa wale waliokataa kumtii Mungu.
12 Neno la Mungu[a] liko hai na linatenda kazi. Lina ukali kupita upanga ulio na makali sana na hukata hadi ndani yetu. Hukata ndani hadi sehemu ambayo nafsi na roho huwa zimeunganishwa pamoja. Neno la Mungu hukata hadi katikati ya maungio na mifupa yetu. Linahukumu mawazo na hisia ndani ya mioyo yetu. 13 Hakuna chochote ulimwenguni mwote kinachoweza kufichika mbele za Mungu. Anaweza kuviona vitu vyote kwa uwazi kabisa. Kila kitu kiko wazi mbele zake. Na kwake tutapaswa kujieleza jinsi tulivyoishi.
Yesu Kristo Ndiye Kuhani Wetu Mkuu
14 Tunaye kuhani mkuu sana ambaye ameenda kuishi na Mungu kule mbinguni. Yeye ni Yesu Mwana wa Mungu. Hivyo tuendelee kuitamka imani yetu katika yeye. 15 Yesu, kuhani wetu mkuu, anaweza kuuelewa udhaifu wetu. Yesu alipoishi duniani, alijaribiwa katika kila njia. Alijaribiwa kwa njia hizo hizo tunazojaribiwa, lakini hakutenda dhambi. 16 Tukiwa na Yesu kama kuhani wetu mkuu, tunaweza kujisikia huru kuja mbele za kiti cha enzi cha Mungu ambako kuna neema. Hapo tunapata rehema na neema ya kutusaidia tunapokuwa tunahitaji.
Yesu na Yohana Mbatizaji
22 Baada ya hayo, Yesu na wafuasi wake wakaenda katika eneo la Uyahudi. Kule Yesu alikaa pamoja na wafuasi wake na kuwabatiza watu. 23 Yohana naye alikuwa akiwabatiza watu kule Ainoni, eneo karibu na Salemu mahali palipokuwa na maji mengi. Huko ndiko watu walipoenda kubatizwa. 24 Hii ilikuwa kabla ya Yohana kufungwa gerezani.
25 Baadhi ya wafuasi wa Yohana walikuwa na mabishano pamoja na Myahudi mwingine juu ya utakatifu.[a] 26 Ndipo wakaja kwa Yohana na kusema, “Mwalimu, unamkumbuka mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Mto Yordani? Yule uliyekuwa ukimwambia kila mtu juu yake.” Huyo pia anawabatiza watu na wengi wanaenda kwake.
27 Yohana akajibu, “Mtu anaweza tu kuyapokea yale ambayo Mungu anayatoa. 28 Ninyi wenyewe mlinisikia nikisema, ‘Mimi siye Masihi. Mimi ni mtu yule aliyetumwa na Mungu kutengeneza njia kwa ajili ya Masihi.’ 29 Bibi arusi siku zote yupo kwa ajili ya bwana arusi. Rafiki anayemsindikiza bwana arusi yeye hungoja na kusikiliza tu na hufurahi anapomsikia bwana arusi akiongea. Hivyo ndivyo ninavyojisikia sasa. Ninayo furaha sana kwani Masihi yuko hapa. 30 Yeye anapaswa kuwa juu zaidi yangu mimi, na mimi napaswa kuwa chini yake kabisa.”
Ajaye Kutoka Mbinguni
31 “Anayekuja kutoka juu ni mkubwa kuliko wengine wote. Anayetoka duniani ni wa dunia. Naye huzungumza mambo yaliyo ya duniani. Lakini yeye anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wengine wote. 32 Huyo huyasema aliyoyaona na kuyasikia, lakini watu hawayapokei anayoyasema. 33 Bali yeyote anayepokea anayoyasema basi amethibitisha kwamba Mungu husema kweli. 34 Na kwamba Mungu alimtuma, na yeye huwaeleza watu yale yote Mungu aliyoyasema. Huyo Mungu humpa Roho kwa ujazo kamili. 35 Baba anampenda Mwana na amempa uwezo juu ya kila kitu. 36 Yeyote anayemwamini Mwana anao uzima wa milele. Lakini wale wasiomtii Mwana hawataupata huo uzima. Na hawataweza kuiepuka hasira ya Mungu.”
© 2017 Bible League International