Book of Common Prayer
15 Unajua kwamba kila mtu aliyeko Asia ameniacha. Hata Figelo na Hermogene nao wameniacha. 16 Ninaomba kwamba Bwana ataonesha rehema wa familia ya Onesiforo, amekuwa faraja yangu mara nyingi, na hakuona haya kwa ajili yangu kuwa gerezani. 17 Kinyume chake, alipofika Rumi, alinitafuta kwa bidii hadi aliponiona. 18 Bwana Yesu na amjalie kupata rehema kutoka kwa Bwana Mungu katika siku ile ya hukumu ya mwisho! Unafahamu vema ni kwa njia ngapi alinihudumia wakati nilipokuwa Efeso.
Askari Mwaminifu wa Kristo Yesu
2 Kwako wewe mwanangu, uwe hodari kwa njia ya neema inayopatikana kwa Kristo Yesu. 2 Yachukue mambo uliyoyasikia kwangu mbele za mashahidi wengi, na yakabidhi kwa watu waaminifu ambao watakuwa na uwezo wa kuwafundisha wengine pia. 3 Kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu, jiunge nami katika mateso. 4 Hakuna hata mmoja anayefanya kazi kama askari kisha akajishughulisha pia na mambo ya kiraia. Hii ni wa sababu anataka kumfurahisha kamanda wake. 5 Na kama kuna mtu anayeshiriki katika mashindano ya riadha, hawezi kushinda taji endapo hatashindana kwa kufuata sheria. 6 Mkulima mwenye juhudi anastahili kuwa wa kwanza kufurahia sehemu ya mavuno yake. 7 Nakutaka wewe kuyafikiri ninayokuambia na Bwana atakupa uwezo wa kuyaelewa mambo haya yote.
8 Endelea kumkumbuka Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, na ni kutoka ukoo wa Daudi. Na huu ndiyo Habari Njema ninayoihubiri. 9 Kwa sababu ya Habari Njema ninateseka, hadi hatua ya kufungwa kwa minyororo kama mhalifu. Lakini ujumbe wa Mungu haujafungwa. 10 Kwa hiyo nayavumilia yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili na wao waweze kuufikia wokovu unaopatikana katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.
11 Na hapa kuna usemi wa kuaminiwa:
Kama tumekufa pamoja naye,
tutaweza kuishi naye pia.
12 Kama tutastahimili, tutaweza pia kumiliki pamoja naye.
Kama tutamkana yeye, naye atatukana sisi.
13 Kama hatutakuwa waaminifu,
yeye anabaki kuwa mwaminifu,
kwa sababu hawezi kujikana mwenyewe.
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mt 19:1-12)
10 Naye aliondoka mahali pale, na kufika katika nchi ya Uyahudi ng'ambo ya Mto Yordani. Na makundi ya watu wakamjia tena na kama alivyofanya daima aliwafundisha.
2 Kisha baadhi ya Mafarisayo walimwendea na kumwuliza “Je, ni sahihi mtu kumtaliki mkewe?” Nao walimwuliza hivyo ili kumjaribu.
3 Yesu akawajibu, “Musa aliwapa amri mfanye nini?”
4 Wakasema, “Musa alimpa ruhusa mume kuandika hati ya kutangua ndoa[a] na kisha kumtaliki mke wake.”
5 Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia amri hii kwa sababu ninyi ni wakaidi na hamkutaka kuyapokea mafundisho ya Mungu. 6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji wake Mungu ‘aliwaumba mwanaume na mwanamke’.(A) 7 ‘Basi kwa sababu ya hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kujiunga na mkewe. 8 Na hao wawili wataungana pamoja na kuwa mwili mmoja.’(B) Nao si wawili tena bali ni mwili mmoja. 9 Kwa hiyo, mtu yeyote asitenganishe kile ambacho Mungu amekiunganisha pamoja.”
10 Walipokuwa ndani ya nyumba ile kwa mara nyingine, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu juu ya jambo hili. 11 Naye akawaambia, “yeyote atakayemtaliki mke wake na kuoa mwanamke mwingine, anazini kinyume cha mkewe. 12 Na ikiwa mke atamtaliki[b] mumewe na kuolewa na mume mwingine, basi naye anafanya zinaa.”[c]
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mt 19:13-15; Lk 18:15-17)
13 Nao watu wakawaleta watoto wadogo kwa Yesu, ili aweze kuwawekea mikono na kuwabariki. Hata hivyo wanafunzi wake waliwakemea. 14 Yesu alipoona hayo, alikasirika, na akawaambia, “Waruhusuni watoto hao waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao. 15 Ninawaambia kweli, Yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyoupokea hataweza kuingia ndani yake.” 16 Naye Yesu akawakumbatia watoto kifuani mwake na akaweka mikono yake juu yao na kuwabariki.
© 2017 Bible League International