Book of Common Prayer
12 Ndugu zangu, naomba mniige mimi kama ambavyo mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunikosea kwa jambo lololote. 13 Mnajua kuwa nilikuja kwenu mara ya kwanza kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Ndipo nilipowaeleza ninyi Habari Njema. 14 Ugonjwa wangu uliwaelemea. Hata hivyo hamkunikataa kutokana na fadhaa ama hofu. Bali, mlinikaribisha kama vile nilikuwa malaika kutoka kwa Bwana. Mlinipokea kama vile nilikuwa Kristo Yesu mwenyewe! 15 Mlikuwa na furaha sana wakati huo. Nini kimetokea kwa imani yenu ya awali kwamba mimi nilikuwa mtu niliyebarikiwa kipekee na Mungu? Naweza kusema bila shaka yoyote kwamba mngeliweza kufanya kitu chochote kunisaidia. Kama ingeliwezekana, mngeliyang'oa hata macho yenu na kunipa mimi. 16 Je, nimekuwa sasa adui yenu kwa sababu nawaambia ukweli?
17 Watu hawa[a] wanajitahidi sana kuonesha kuvutiwa nanyi,[b] lakini hiyo siyo nzuri kwenu. Wanataka kuwashawishi ninyi ili mtugeuke sisi na kuambatana nao. 18 Inapendeza daima kuwa na mtu anayevutiwa nawe katika jambo lililo jema. Hivyo ndivyo nilivyofanya nilipokuwa pamoja nanyi. Siku zote inapendeza, na si pale tu mimi nikiwapo. 19 Watoto wangu wadogo, nasikia uchungu tena kwa ajili yenu, kama mama anayejifungua. Nitaendelea kusikia uchungu huu mpaka watu watakapofikia kumwona Kristo wawatazamapo ninyi. 20 Natamani ningekuwa nanyi sasa. Ndipo labda ninapoweza kubadilisha namna ninavyoongea nanyi. Sasa sielewi nifanye nini juu yenu.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000
(Mt 15:32-39)
8 Wakati mwingine katika siku zile kundi kubwa la watu lilikusanyika na halikuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake na kuwaambia, 2 “Nawahurumia watu hawa, kwa sababu hata sasa wamekuwa nami kwa siku tatu, na hawana kitu cha kula.”
3 Nikiwaacha waende majumbani mwao wakiwa na njaa, wataanguka njiani; na baadhi yao wametoka mbali.
4 Wanafunzi wake wakamjibu, “Wapi mtu yeyote atapata chakula cha kutosha mahali hapa jangwani cha kuwalisha watu hawa?”
5 Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakajibu, “Saba.”
6 Kisha Yesu akaliagiza kundi la watu kuketi chini ardhini Akachukua mikate ile saba, akashukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake waigawe. Nao wakaigawa kwenye kundi. 7 Kulikuwapo pia samaki wadogo wachache. Yesu akawabariki wale samaki na kuwaambia waigawe nayo pia.
8 Watu walikula na kushiba. Wakakusanya vikapu saba vilivyojaa mabaki. 9 Ilikuwa kama watu 4,000. Kisha Yesu akawaacha waende. 10 Mara Yesu akapanda katika mashua na wanafunzi wake, na akafika katika wilaya ya Dalmanutha.
© 2017 Bible League International