Book of Common Prayer
Roho na Asili ya Kibinadamu
16 Hivyo ninawaambieni, ishini kama Roho anavyowaongoza. Hapo hamtatenda dhambi kutokana na tamaa zenu mbaya. 17 Utu wenu wa dhambi unapenda yale yaliyo kinyume cha Roho, na Roho anataka yale yaliyo kinyume na utu wa dhambi. Hao siku zote hushindana wao kwa wao. Kwa jinsi hiyo ninyi hamko huru kufanya chochote mnachotaka kufanya. 18 Lakini mkimruhusu Roho awaongoze, hamtakuwa chini ya sheria.[a]
19 Mambo mabaya yanayofanywa na mwili wa dhambi ni dhahiri: uasherati, tabia chafu, kufanya mambo yenye kuleta aibu, 20 kuabudu miungu wa uongo, kushiriki mambo ya uchawi, kuwachukia watu, kuanzisha mafarakano, kuwa na wivu, hasira ama choyo, kusababisha mabishano na kujigawa kimakundi na kuwatenga wengine, 21 kujawa na husuda, kulewa pombe, kushiriki karamu zenye ulafi na uasi mwingi na kufanya mambo yanayofanana na hayo. Ninawatahadharisha mapema kama nilivyowatahadharisha mwanzo: Watu wanaofanya mambo hayo hawatahesabiwa kama watoto watakaourithi ufalme wa Mungu. 22 Lakini tunda linalozaliwa na Roho katika maisha ya mtu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, na kiasi. Hakuna sheria juu ya mambo kama haya. 24 Wale walio wa Kristo Yesu wameusulubisha udhaifu wao wa kibinadamu pamoja na tamaa zake za dhambi na zile za mwili. Wameachana na utu wao wa kale wenye hisia za ubinafsi na uliotaka kufanya mambo maovu.
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mt 17:1-13; Lk 9:28-36)
2 Baada ya siku sita, Yesu akamchukua Petro, Yakobo na Yohana na kuwaongoza hadi mlima mrefu wakiwa peke yao tu. Na mwonekano wa Yesu ulibadilika mbele yao. Huko Yesu akabadilika sura nyingine akiwa mbele yao. 3 Mavazi yake yakiwa na mng'ao, na meupe kabisa kuliko mtu anavyoweza kufua nguo kwa sabuni na kuitakatisha. 4 Huko Eliya na Musa pia wakawatokea, na Yesu alizungumza na manabii hao wawili.
5 Petro akafungua kinywa chake na kumwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema tupo hapa. Tufanye basi vibanda vitatu; moja kwa ajili yako, moja kwa ajili ya Musa na moja kwa ajili ya Eliya.” 6 Petro aliyasema haya kwa sababu hakujua aseme nini, kwa sababu yeye na wenzake walikuwa wamepata hofu.
7 Ndipo wingu likaja na kuwafunika wote kwa kivuli chake. Na sauti ikatoka mawinguni, ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikilizeni yeye.”
8 Ndipo ghafula walipokuwa wakiangalia huku na huko, hawakuona mtu yeyote akiwa pamoja nao isipokuwa Yesu peke yake.
9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote kile walichokiona mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka katika wafu.
10 Hivyo hawakuwaeleza wengine juu ya jambo lile bali walijadiliana miongoni mwao wenyewe juu ya maana ya “kufufuka kutoka kwa wafu.” 11 Wakamwuliza Yesu, “kwa nini walimu wa sheria wanasema Eliya lazima aje kwanza?”
12 Yesu akawaambia, “Ndiyo, Eliya atakuja kwanza[a] kuja kuyaweka mambo yote sawa kama jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu[b] ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa? 13 Lakini ninawaambia, Eliya amekuja,[c] na walimtendea kila kitu walichotaka, kama vile ilivyoandikwa[d] kuhusu yeye.”
© 2017 Bible League International