Book of Common Prayer
Sisi Pia Tuufuate Mfano wa Yesu
12 Tunao hawa watu mashuhuri wakituzunguka kama mifano kwetu. Maisha yao yanatueleza imani ni nini. Hivyo, nasi pia, tunapaswa kufanya mashindano yaliyo mbele yetu na kamwe tusikate tamaa. Tunapaswa kuondoa katika maisha yetu kitu chochote kitakachotupunguzia mwendo pamoja na dhambi zinazotufanya tutoke kwenye mstari mara kwa mara. 2 Hatupaswi kuacha kumwangalia Yesu. Yeye ndiye kiongozi wa imani yetu, na ndiye anayeikamilisha imani yetu. Aliteseka hadi kufa msalabani. Lakini aliikubali aibu ya msalaba kama kitu kisicho na maana kwa sababu ya furaha ambayo angeiona ikimngojea. Na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mfikirie Yesu. Kwa uvumilivu alistahimili matusi ya hasira ya watenda dhambi waliokuwa wakiwapigia kelele. Mfikirie yeye ili usikate tamaa na kuacha kujaribu.
Mungu ni Kama Baba
4 Mnashindana na dhambi, lakini bado hamjamwaga damu hata kuutoa uhai wenu katika mashindano hayo. 5 Ninyi ni watoto wa Mungu, naye huzungumza maneno ya faraja kwenu. Labda mmeyasahau maneno haya:
“Mwanangu, wakati Mungu anapokurekebisha,
zingatia na usiache kujaribu.
6 Bwana humrekebisha kila anayempenda;
humpa adhabu kila anayemkubali kama mwana wake.”(A)
Yesu Azungumza Juu ya Roho Mtakatifu
37 Siku ya mwisho ya kusherehekea sikukuu ikafika. Nayo Ilikuwa siku muhimu zaidi. Katika siku hiyo Yesu alisimama na kusema kwa sauti kubwa, “Yeyote aliye na kiu aje kwangu anywe. 38 Kama mtu ataniamini, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka ndani ya moyo wake. Ndivyo Maandiko yanavyosema.” 39 Yesu alikuwa anazungumza juu ya Roho Mtakatifu ambaye alikuwa hajatolewa kwa watu bado, kwa sababu Yesu naye alikuwa bado hajatukuzwa. Ingawa baadaye, wale waliomwamini Yesu wangempokea huyo Roho.
Watu Wanabishana Juu ya Yesu
40 Watu waliposikia maneno aliyosema Yesu, baadhi yao wakasema, “Hakika mtu huyu ni nabii.”[a]
41 Wengine wakasema, “Huyu ni Masihi.”
Na wengine wakasema, “Masihi hawezi kutoka Galilaya. 42 Maandiko yanasema kwamba Masihi atatoka katika ukoo wa Daudi. Na wanasema kwamba atatoka Bethlehemu, mji alimoishi Daudi.” 43 Kwa jinsi hiyo watu hawakukubaliana wao kwa wao kuhusu Yesu. 44 Baadhi yao wakataka kumkamata. Lakini hakuna aliyejaribu kufanya hivyo.
Baadhi ya Viongozi wa Kiyahudi Wakataa Kuamini
45 Walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Makuhani na Mafarisayo wakawauliza, “Kwa nini hamjamleta Yesu?”
46 Walinzi wa Hekalu wakajibu, “Hatujawahi kumsikia mtu akisema mambo ya ajabu kiasi hicho!”
© 2017 Bible League International