Revised Common Lectionary (Complementary)
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Yh 11:47-53)
22 Ilikuwa karibu ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, inayoitwa Pasaka. 2 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walitaka kumwua Yesu kwa siri kwa sababu waliogopa kile ambacho watu wangefanya.
Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu
(Mt 26:14-16; Mk 14:10-11)
3 Mmoja wa mitume kumi na wawili wa Yesu aliitwa Yuda Iskariote. Shetani alimwingia Yuda, 4 akaondoka, akaenda kuongea na viongozi wa makuhani na baadhi ya wakuu wa askari walinzi wa Hekalu. Aliongea nao kuhusu namna ya kumkabidhi Yesu kwao. 5 Makuhani walifurahia sana hili. Wakaahidi kumlipa Yuda pesa ikiwa angefanya hivi. 6 Akakubali, kisha alianza kusubiri muda mzuri wa kumkabidhi Yesu kwao. Alitaka kumkabidhi Yesu kwao wakati hakuna kundi la watu ambao wangeona.
Karamu ya Pasaka
(Mt 26:17-25; Mk 14:12-21; Yh 13:21-30)
7 Siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu[a] ilifika. Hii ni siku ambayo Wayahudi daima walichinja kondoo kwa ajili ya Pasaka. 8 Yesu aliwaambia Petro na Yohana, “Nendeni mkaandae mlo wa Pasaka ili tule.”
9 Wakamwambia, “Unataka tukauandae wapi?”
Akawaambia, 10 “Mtakapokuwa mnaingia mjini, mtakutana na mtu amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. Ataingia katika nyumba. 11 Mwambieni mmiliki wa nyumba, ‘Mwalimu anakuomba tafadhali utuoneshe chumba ambacho yeye na wafuasi wake wanaweza kulia mlo wa Pasaka.’ 12 Mmiliki atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilicho tayari kwa ajili yetu. Andaeni mlo humo.”
13 Hivyo Petro na Yohana wakaondoka. Kila kitu kilitokea kama Yesu alivyosema. Na hivyo wakauandaa mlo wa Pasaka.
© 2017 Bible League International