Revised Common Lectionary (Complementary)
Paulo Asimama Mbele ya Mfalme Agripa
26 Agripa[a] akamwambia Paulo, “Unaweza sasa kujitetea wewe mwenyewe.” Paulo akanyoosha mkono wake ili wamsikilize kwa makini na akaanza kusema. 2 “Mfalme Agripa, najisikia heshima kusimama hapa mbele yako leo ili nijibu mashitaka yote yaliyotengenezwa na Wayahudi dhidi yangu. 3 Ninafurahi kuzungumza nawe, kwa sababu unafahamu sana kuhusu desturi za Kiyahudi na mambo ambayo Wayahudi hubishana. Tafadhali uwe mvumilifu kunisikiliza.
4 Wayahudi wote wanafahamu maisha yangu yote. Wanafahamu namna nilivyoishi tangu mwanzo miongoni mwa watu mwangu na baadaye Yerusalemu. 5 Wayahudi hawa wamenifahamu kwa muda mrefu. Wakitaka wanaweza kukwambia kwamba nilikuwa Farisayo mzuri. Na Mafarisayo wanazitii sheria za dini ya Kiyahudi kwa uangalifu kuliko kundi lolote. 6 Na sasa nimeshitakiwa kwa sababu ninatumaini ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. 7 Hii ni ahadi ambayo makabila yote kumi na mbili ya watu wetu yanatumaini kuipokea. Kwa sababu ya tumaini hili Wayahudi wanamtumikia Mungu usiku na mchana. Ee Mfalme wangu, Wayahudi wamenishitaki kwa sababu ninatumaini ahadi hii hii. 8 Kwa nini ninyi watu mnadhani Mungu hawezi kuwafufua watu kutoka kwa wafu?
9 Huko nyuma nilidhani kuwa ninapaswa kufanya kinyume na Yesu kutoka Nazareti kwa kadri ninavyoweza. 10 Na ndivyo nilivyofanya, kuanzia Yerusalemu. Viongozi wa makuhani walinipa mamlaka ya kuwaweka gerezani watu wa Mungu wengi. Na walipokuwa wanauawa nilikubali kuwa lilikuwa jambo zuri. 11 Nilikwenda katika masinagogi yote na kuwaadhibu, nikijaribu kuwafanya wamlaani[b] Yesu. Hasira yangu dhidi ya watu hawa ilikuwa kali sana kiasi kwamba nilikwenda katika miji mingine kuwatafuta na kuwaadhibu.
Paulo Aeleza Alivyomwona Yesu
12 Wakati fulani viongozi wa makuhani walinipa ruhusa na mamlaka kwenda katika mji wa Dameski. 13 Nikiwa njiani, mchana, niliona mwanga kutoka mbinguni, unaong'aa kuliko jua. Uling'aa kunizunguka mimi pamoja na wale waliokuwa wanasafiri pamoja nami. 14 Sote tulianguka chini. Kisha nilisikia sauti iliyozungumza nami kwa Kiaramu. Sauti ilisema, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unanitesa? Unajiumiza wewe mwenyewe kwa kunipinga mimi.’
15 Nilisema, ‘Wewe ni nani, Bwana?’
Bwana alisema, ‘Mimi ni Yesu. Unayemtesa. 16 Simama! Nimekuchagua wewe kuwa mtumishi wangu. Utawaambia watu habari zangu, ulichoona leo na yale nitakayokuonesha. Hii ndiyo sababu nimekuja kwako. 17 Nitakulinda dhidi ya watu wako na dhidi ya watu wasio Wayahudi, ninaokutuma kwao. 18 Utawafanya waielewe kweli. Watatoka gizani na kuja kwenye mwanga. Watageuka kutoka kwenye mamlaka ya Shetani na kumgeukia Mungu. Ndipo dhambi zao zitasamehewa, na wataweza kupewa nafasi miongoni mwa watu wa Mungu, walifanywa watakatifu kwa kuniamini.’”
© 2017 Bible League International