Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Old/New Testament

Each day includes a passage from both the Old Testament and New Testament.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Error: Book name not found: Judg for the version: Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Luka 6:1-26

Yesu ni Bwana Juu ya Siku ya Sabato

(Mt 12:1-8; Mk 2:23-28)

Wakati fulani siku ya Sabato, Yesu alikuwa akitembea kupitia katika baadhi ya mashamba ya nafaka. Wafuasi wake wakachukua masuke, wakayapukusa mikononi mwao na kula nafaka. Baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, “Kwa nini mnafanya hivyo? Ni kinyume na Sheria ya Musa kufanya hivyo siku ya Sabato.”

Yesu akawajibu, “Je, mmesoma kuhusu jambo alilofanya Daudi, wakati yeye na watu wake walipohisi njaa? Daudi alikwenda katika nyumba ya Mungu, akachukua mikate iliyotolewa kwa Mungu na kuila. Na kuwapa wenzake baadhi ya mikate hiyo. Hii ilikuwa kinyume na Sheria ya Musa, inayosema kuwa makuhani pekee ndiyo wanaoruhusiwa kula mikate hiyo.” Kisha Yesu akawaambia Mafarisayo, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato

(Mt 12:9-14; Mk 3:1-6)

Siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na kuwafundisha watu. Katika sinagogi hili alikuwemo mtu aliyepooza mkono wake wa kulia. Walimu wa sheria na Mafarisayo walikuwa wakimvizia Yesu. Walikuwa wanasubiri waone ikiwa ataponya siku hiyo ya Sabato. Walitaka kumwona akifanya jambo lolote lililo kinyume ili wamshitaki. Lakini Yesu alijua walilokuwa wanawaza. Akamwambia mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyenyuka na simama hapa ambapo kila mtu anaweza kukuona!” Yule mtu akanyenyuka na kusimama pale. Ndipo Yesu akawaambia, “Ninawauliza ninyi, Sheria inaturuhusu tufanye nini siku ya Sabato: kutenda mema au kutenda mabaya? Je, ni halali kuokoa uhai au kuuangamiza?”

10 Yesu akawatazama watu wote kila upande, kisha akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyosha mkono wake, na akaponywa. 11 Mafarisayo na walimu wa sheria wakakasirika sana kiasi cha kutofikiri sawasawa, wakashauriana wao kwa wao wamfanye nini Yesu.

Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili

(Mt 10:1-4; Mk 3:13-19)

12 Siku chache baadaye, Yesu alikwenda mlimani kuomba. Alikaa huko usiku kucha akimwomba Mungu. 13 Asubuhi iliyofuata aliwaita wafuasi wake, akachagua kumi na wawili miongoni mwao na kuwaita Mitume. Nao ni:

14 Simoni (ambaye Yesu alimwita Petro),

Andrea aliyekuwa kaka yake Petro,

Yakobo,

Yohana,

Filipo,

Bartholomayo,

15 Mathayo na

Tomaso,

Yakobo mwana wa Alfayo,

Simoni aliyeitwa Mzelote,

16 Yuda mwana wa Yakobo,

na Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu).

Yesu Afundisha na Kuponya Watu

(Mt 4:23-25; 5:1-12)

17 Yesu na mitume wakatelemka kutoka mlimani. Yesu akasimama mahali tambarare. Kundi kubwa la wafuasi wake lilikuwa pale. Walikuwepo pia watu wengi waliotoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu, na maeneo ya pwani karibu na Tiro na Sidoni. 18 Wote walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Aliwaponya watu waliokuwa wanasumbuliwa na mapepo. 19 Kila mtu alijaribu kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa unamtoka. Yesu aliwaponya wote.

20 Yesu akawatazama wafuasi wake na kusema,

“Heri ninyi mlio maskini.
    Maana Ufalme wa Mungu ni wenu.
21 Heri ninyi mlio na njaa sasa.
    Maana mtashibishwa.
Heri ninyi mnaolia sasa.
    Maana mtafurahi na kucheka.

22 Watu watawachukia kwa sababu ninyi ni wa milki ya Mwana wa Adamu. Watawabagua na watawatukana. Watajisikia vibaya hata kutamka majina yenu. Mambo haya yatakapotukia, mjue kuwa baraka kuu ni zenu. 23 Ndipo mfurahi na kurukaruka kwa furaha, kwa sababu mna thawabu kuu mbinguni. Baba zao waliwafanyia manabii vivyo hivyo.

24 Lakini ole wenu ninyi matajiri,
    kwa kuwa mmekwishapata maisha yenye raha.
25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,
    kwa kuwa mtasikia njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
    kwa kuwa mtalia na kuhuzunika.

26 Ole wenu watu wote wanapowasifu ninyi. Maana mababu zao waliwasifu manabii wa uongo vivyo hivyo daima.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International