Old/New Testament
Kuzaliwa kwa Yesu
(Mt 1:18-25)
2 Ulikuwa wakati ambapo amri ilitolewa na Kaisari Augusto kwamba watu wote wanaoishi katika utawala wote wa Rumi[a] wahesabiwe na kuorodheshwa[b] katika kumbukumbu za serikali. 2 Orodha hii ilikuwa ya kwanza tangu Kirenio alipokuwa gavana wa Shamu. 3 Kila mtu alikwenda katika mji aliozaliwa ili akahesabiwe na kuingizwa katika orodha hiyo.
4 Hivyo Yusufu alitoka Nazareti, mji uliokuwa katika jimbo la Galilaya na kwenda katika mji wa Bethlehemu uliokuwa katika jimbo la Uyahudi. Pia, mji huu ulijulikana kama mji wa Daudi. Yusufu alikwenda Bethlehemu kwa sababu alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Daudi. 5 Yusufu alijiandikisha akiwa pamoja na Mariamu kwani alikuwa tayari amemchumbia ili amwoe. Na Mariamu alikuwa mjamzito. 6 Yusufu na Mariamu walipokuwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu kujifungua ulifika. 7 Akamzaa mwanawe wa kwanza. Akamvingirishia nguo vizuri, kisha akamlaza katika hori la kulishia mifugo.[c] Walimweka humo kwa sababu chumba cha wageni kilikuwa kimejaa.
Wachungaji wa Mifugo Wajulishwa Kuhusu Yesu
8 Usiku ule, baadhi ya wachungaji walikuwa mashambani nje ya mji wa Bethlehemu wakilinda kondoo zao. 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukaangaza kuwazunguka, wakaogopa sana. 10 Malaika akawaambia, “Msiogope, kwa kuwa nimewaletea habari njema zitakazowafurahisha watu wa Mungu wote. 11 Kwa sababu leo katika mji wa Daudi amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo,[d] Bwana. 12 Na hivi ndivyo mtakavyomtambua: Mtamkuta mtoto mchanga amevingirishiwa nguo na amelala katika hori la kulishia mifugo.”
13 Kisha malaika pamoja na jeshi kubwa la mbinguni wakaanza kumsifu Mungu, wakisema:
14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
na amani iwepo duniani
kwa watu wote wanaompendeza.”
15 Malaika walipoondoka kurudi mbinguni, wale wachungaji wakaambiana wakisema, “Twendeni Bethlehemu, tukalione jambo hili lililotokea, ambalo Bwana ametujulisha.”
16 Wakaenda haraka, wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala katika hori la kulishia mifugo. 17 Wachungaji walipomwona huyo mtoto, walisimulia kile walichoambiwa na malaika kuhusu mtoto. 18 Kila aliyesikia maelezo ya wachungaji, alishangaa. 19 Mariamu aliendelea kuyatafakari mambo haya, na kuyaweka moyoni. 20 Wachungaji waliirudia mifugo yao, wakawa wanamsifu na kumshukuru Mungu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona. Ilikuwa kama walivyoambiwa na malaika.
21 Ilipofika siku ya nane mtoto alitahiriwa, akaitwa Yesu. Hili ndilo jina alilopewa na malaika kabla mama yake hajaibeba mimba yake.
Yesu Atambulishwa Hekaluni
22 Muda wa kutakaswa ulimalizika, kama ilivyotakiwa na Sheria ya Musa baada ya mtoto kuzaliwa.[e] Baada ya hapo walimpeleka Yesu Yerusalemu na kumweka mbele za Bwana. 23 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana: Mzaliwa wa kwanza akiwa mtoto wa kiume, atolewe wakfu kwa ajili ya Bwana.[f] 24 Pia Mariamu na Yusufu walikwenda Yerusalemu kutoa dhabihu kama Sheria ya Bwana inavyosema kuwa, “Ni lazima utoe dhabihu ya jozi moja ya hua[g] au makinda mawili wa njiwa.”
© 2017 Bible League International