Old/New Testament
19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka Yerusalemu.
Mtini na Imani, Maombi na Msamaha
(Mt 21:20-22)
20 Ilipofika asubuhi Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakitembea pamoja na wakauona ule mti wa mtini umekauka kuanzia kwenye mizizi yake. 21 Petro akakumbuka yale Yesu aliyosema kwa mti huo na kumwambia, “Mwalimu, tazama! Mti ule wa mtini ulioulaani umenyauka kabisa.”
22 Yesu akawajibu, “Mnapaswa kuweka imani yenu kwa Mungu. 23 Nawaambia kweli: Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ukajitupe katika bahari’; kama asipokuwa na mashaka moyoni mwake, Lakini akaamini kuwa kile anachokisema kitatokea, huyo atatendewa hayo. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia chochote mtakachoomba katika sala, muamini kwamba mmekipokea na haja mliyoiomba nayo itakuwa yenu, 25 Na wakati wowote mnaposimama kuomba, mkiwa na neno lolote kinyume na mtu mwingine, mmsamehe mtu huyo. Na Baba yenu aliye mbinguni naye atawasamehe ninyi dhambi zenu.” 26 [a]
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mt 21:23-27; Lk 20:1-8)
27 Yesu na wanafunzi wake walirudi Yerusalemu. Na walipokuwa wakitembea ndani ya viwanja vya Hekalu, viongozi wa makuhani, walimu wa Sheria na wazee walimjia Yesu 28 na kumwuliza, “Kwa mamlaka gani unafanya vitu hivi? Nani alikupa mamlaka ya kuvifanya?”
29 Yesu akawaambia, “Nitawauliza swali, na mkinijibu, ndipo nitawaeleza kwa mamlaka gani ninafanya vitu hivi. 30 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni ama ulitoka kwa watu? Sasa mnijibu basi.”
31 Walijadiliana wao kwa wao wakisema, “Tukisema ‘ulitoka mbinguni’, atasema, ‘Kwa nini basi hamumuamini?’ 32 Lakini kama tukisema kuwa ubatizo wa Yohana ulitoka kwa wanadamu, watu watatukasirikia.” Viongozi waliwaogopa watu, kwani watu wote waliamini kuwa Yohana kweli alikuwa nabii.
33 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.”
Hivyo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”
© 2017 Bible League International