Old/New Testament
Watu Wamtafuta Yesu
22 Siku iliyofuata watu wengi walikuwa wamekaa upande mwingine wa ziwa. Nao walijua kuwa Yesu hakwenda pamoja na wafuasi wake kwenye mashua. Kwani walifahamu kuwa wafuasi wake waliondoka na mashua peke yao. Walijua pia kuwa ile ilikuwa ni mashua pekee iliyokuwepo pale. 23 Lakini baadaye mashua zingine kutoka Tiberia zilifika na kusimama karibu na mahali walipokula chakula jana yake. Hapo ni mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kushukuru. 24 Watu wakaona kuwa Yesu na wafuasi wake hawakuwa hapo. Hivyo wakaingia katika mashua zao na kuelekea Kapernaumu kumtafuta Yesu.
Yesu, Mkate wa Uzima
25 Watu wakamwona Yesu akiwa upande mwingine wa ziwa. Wakamwuliza, “Mwalimu, ulifika huku lini?”
26 Akawajibu, “Kwa nini mnanitafuta? Ni kwa sababu mliona ishara na miujiza iliyotendeka? Ukweli ni kwamba, mnanitafuta kwa vile mlikula ile mikate mkashiba. 27 Lakini chakula cha kidunia kinaharibika na hakidumu. Ninyi msifanye kazi ili kupata chakula cha aina hiyo kinachoharibika. Isipokuwa fanyeni kazi ili mpate chakula kinachodumu na kinachowapa uzima wa milele. Mwana wa Adamu atawapa hicho chakula. Yeye ndiye pekee aliyethibitishwa na Mungu Baba kuwapa.”
28 Watu wakamwuliza Yesu, “Mungu anatutaka tufanye nini?”
29 Yesu akajibu, “Kazi anayoitaka Mungu muifanye ni hii: kumwamini yule aliyemtuma.”
30 Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je, utafanya nini? 31 Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’”(A)
32 Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. 33 Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34 Watu wakasema, “Bwana, kuanzia sasa na kuendelea tupe mkate wa aina hiyo.”
35 Kisha Yesu akasema, “Mimi ndiye mkate unaoleta uzima. Hakuna ajaye kwangu atakayehisi njaa. Hakuna anayeniamini atakayepata kiu kamwe. 36 Nilikwisha kuwaambia mapema kuwa mmeona kile ambacho naweza kufanya,[a] lakini bado hamuniamini. 37 Vyote anavyonipa Baba vitakuja kwangu hata hivyo yeyote Yule atakayekuja kwangu sitamkataa kabisa. Nami kwa hakika daima nitawapokea. 38 Nilishuka kutoka mbinguni kuja kufanya yale Mungu anayopenda, siyo ninayoyapenda mimi. 39 Nami sitampoteza hata mmoja wa wale alionipa Mungu. Bali nataka nimfufue katika siku ya mwisho. Haya ndiyo Baba yangu anayoyataka. 40 Kila anayemtazama Mwana na kumwamini anao uzima wa milele. Nami nitamfufua katika siku ya mwisho. Hayo ndiyo anayoyataka Baba yangu.”
41 Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?”
43 Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. 44 Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu.
© 2017 Bible League International