Old/New Testament
Yesu na Nikodemu
3 Alikuwepo mtu aliyeitwa Nikodemu, mmoja wa Mafarisayo. Yeye alikuwa kiongozi muhimu sana wa Kiyahudi. 2 Usiku mmoja alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa kutoka kwa Mungu. Hayupo mtu yeyote anayeweza kutenda ishara na miujiza unayotenda bila msaada wa Mungu.”
3 Yesu akajibu, “Hakika nakuambia, ni lazima kila mtu azaliwe upya.[a] Yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.”
4 Nikodemu akasema, “Yawezekanaje mtu ambaye tayari ni mzee akazaliwa tena? Je, anaweza kuingia tena katika tumbo la mama yake na kuzaliwa kwa mara ya pili?”
5 Yesu akamjibu, “Uniamini ninapokwambia kuwa kila mtu anapaswa kuzaliwa tena kwa maji na kwa Roho. Yeyote ambaye hakuzaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 6 Maisha pekee ambayo watu huyapata kutoka kwa wazazi wao ni ya kimwili. Lakini maisha mapya anayopewa mtu na Roho ni ya kiroho. 7 Usishangae kwa kuwa nilikuambia, ‘Ni lazima mzaliwe upya.’ 8 Upepo huvuma kuelekea popote unakopenda. Unausikia, lakini huwezi kujua unakotoka na unakoelekea. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kila aliyezaliwa kwa Roho.”
9 Nikodemu akauliza, “Je, haya yote yanawezekana namna gani?”
10 Yesu akasema, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Israeli, inakuwaje huelewi mambo haya? 11 Ukweli ni kwamba, tunaongea yale tunayoyafahamu. Tunayasema yale tuliyoyaona. Hata hivyo ninyi hamyakubali yale tunayowaambia. 12 Nimewaeleza juu ya mambo ya hapa duniani, lakini hamniamini. Vivyo hivyo nina uhakika hamtaniamini hata nikiwaeleza mambo ya mbinguni! 13 Sikiliza, hakuna mtu aliyewahi kwenda kwa Mungu mbinguni isipokuwa Mwana wa Adamu. Yeye pekee ndiye aliyekuja duniani kutoka mbinguni.”
14 Unakumbuka yule nyoka wa shaba ambaye Musa alimwinua kule jangwani?[b] Vivyo hivyo Mwana wa Adamu anapaswa kuinuliwa juu. 15 Kisha kila anayemwamini aweze kuupata uzima wa milele.[c]
16 Kweli, hivi ndivyo Mungu alivyouonyesha upendo wake mkuu kwa ulimwengu: akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu anayemwamini asiharibiwe na mauti bali aupate uzima wa milele. 17 Mungu alimtuma Mwanawe ili kuuokoa ulimwengu. Hakumtuma kuja kuuhukumu na kuuweka hatiani, bali kuuokoa kwa njia ya mwanawe. 18 Wote wanaomwamini Mwana wa Mungu hawahukumiwi hatia yoyote. Lakini wale wasiomwamini wamekwisha kuhukumiwa tayari, kwa sababu hawakumwamini Mwana pekee wa Mungu.
© 2017 Bible League International